FIGO ZINAVYOHARIBIKA KWA KISUKARI

UGONJWA wa figo unaotokana na kuharibiwa na kisukari hujulikana kitaalam kwa jina la Diabetic Nephropathy.  Moja ya madhara ya ugonjwa wa kisukari katika mwili wa binadamu ni ugonjwa wa figo (Diabetic Nephropathy). Ugonjwa huu ambao huwapata watu wenye kisukari, hutokea muda mrefu baada ya mtu kugunduliwa kuwa ana kisukari.Si vibaya kufahamu kuwa, figo zinaundwa na mamia kwa maelfu ya vijiumbo vidogovidogo viitwavyo kitaalam Nefroni (Nephrons).

Kazi ya Nefroni hizi ni kuchuja damu na kutoa uchafu mwilini kwa njia ya mkojo. Kwa watu wenye kisukari, Nefroni huwa na tabia ya kukakamaa, kuzeeka na kuwa na makovu kadiri miaka inavyopita. Baada ya muda fulani, hushindwa kabisa kazi yake ya kuchuja uchafu, matokeo yake, protini ambazo kwa kawaida huwa haziwezi kufanyiwa kazi, huchujwa na kutoka katika mkojo. Chanzo hasa cha kuzeeka, kukamaa na kuwa na makovu huku kwa Nefroni hakijulikani.

Hata hivyo, udhibiti mbaya wa sukari husababisha uharibifu wa figo na madhara huongezeka maradufu kwa watu wenye shinikizo la damu lisilodhibitiwa pamoja na kisukari. Ifahamike kuwa si kila mwenye kisukari hupata ugonjwa wa figo. Kwa baadhi ya watu, hali hii ya kisukari ina uhusiano mkubwa na historia ya ugonjwa huo katika familia zao na kuwa wa kurithi.

Wagonjwa wa kisukari ambao pia ni wavutaji wa sigara na wale wenye aina ya kwanza ya kisukari yaani Type 1 Diabetes Mellitus ambao walianza kabla hawajafikia umri wa miaka 20, wana hatari kubwa ya kupata matatizo ya figo. Kwa kawaida, mtu mwenye tatizo hili anaweza asioneshe dalili zozote katika miaka ya mwanzo ya ugonjwa. Mara nyingi dalili huanza kujitokeza miaka mitano hadi kumi baada ya figo kuathirika.

DALILI

Dalili huanza taratibu kabla ya kudhihirika. Dalili kwa watu waliopata madhara makubwa katika figo hujumuisha kukosa hamu ya kula, kuhisi uchovu na kwa jumla kutojihisi vizuri. Dalili nyingine ni kuumwa kichwa, kichefuchefu na kutapika, kuvimba miguu pamoja na dalili nyingine kama zile zinazotokea mtu anapokuwa na ugonjwa sugu wa figo.

Kwa watu wenye kisukari, ni vyema kufanya uchunguzi wa figo zao walau mara moja kwa mwaka. Daktari kwa kawaida kwanza huchunguza kama mgonjwa ana dalili zozote zinazoashiria matatizo ya figo. Kipimo kimojawapo ni kuchunguza mkojo kwa ajili ya kuangalia kiwango cha protini iitwayo Albumin au Microalbuminuria katika mkojo.

Kuwepo kiasi kingi cha protini hiyo katika mkojo ni moja ya dalili za kuwepo tatizo katika figo. Vipimo vingine ni pamoja na kiasi cha Urea Nitrogen katika damu (BUN), kiwango cha creatine katika damu, kiasi cha protini katika mkojo wa saa 24, kiasi cha madini ya phosphorus, calcium, bicarbonate, PTH na potassium katika damu, kiasi cha wingi wa damu (Hemoglobin) na wakati fulani kufanya biopsy ya figo kwa ajili ya uthibitisho wa tatizo.

TIBA

Matibabu ya ugonjwa wa figo unaosababishwa na kisukari, lengo kuu ni kuzuia figo zisiendelee kuathirika. Mojawapo ya njia bora kabisa za kusaidia suala hilo ni kudhibiti kiwango cha shinikizo la damu ili kiwe chini ya 130/80 mmHg.

Dawa ambalimbali hutumika katika matibabu kama vile Captopril pamoja na zile zenye uwezo mkubwa wa kushusha shinikizo la damu na wakati huohuo kudhibiti kasi ya kuharibika figo kutokana na kisukari. Kula lishe yenye kiwango kidogo cha mafuta, matumizi ya dawa za kudhibiti kiasi cha mafuta mwilini na kufanya mazoezi mara kwa mara pia husaidia sana kuzuia au kupunguza kasi ya kuathirika figo.

Aidha, udhibiti wa kiwango cha sukari kwa kubadilisha aina ya chakula unachokula, kutumia dawa za kisukari kama inavyoshauriwa na daktari na kuchunguza kiwango cha sukari mara kwa mara, husaidia pia katika kuzuia tatizo hili.

Kwa mtu mwenye maambukizi katika njia ya mkojo au UTI ni vyema atibiwe kwa kutumia dawa za antibiotics. Ifahamike kuwa, ugonjwa wa figo unaotokana na kisukari ni moja ya sababu kuu za kuugua na vifo kwa wagonjwa wa kisukari. Hata hivyo, iwapo tatizo litagunduliwa katika hatua zake za awali, kuna uwezekano mkubwa wa kuzuia na kudhibiti uharibifu wa figo.

Mara baada ya protini kuonekana katika mkojo, uharibu wa figo huanza kuwa mkubwa na wa kutisha kiasi cha kuhitaji kufanyiwa dialysisau kubadilishwa figo. Hali kadhalika, watu wenye ugonjwa wa figo unaotokana na kisukari huwa wana magonjwa mengine kama vile shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo pamoja na magonjwa ya macho.


Loading...

Toa comment