HABARI mpenzi msomaji, nikualike tena kwa upendo wa dhati kabisa katika somo letu linalojieleza hapo juu. Kupata nafasi hii ya kukupatia somo haimanishi mimi ni bora kuliko wewe, la hasha!Inawezekana wewe ni bora zaidi kuliko mimi.
Dhamira ya somo tajwa nikukufanya ubadilike katika mtazamo mzima wa kufikiri na kuamua katika maisha yako.
Leo hii mwanafunzi yoyote ambaye anasoma ukimuuliza swali, je, unasoma ili iweje?
Bila shaka majibu ya walio wengi watakwambia, mimi nataka kuwa mwalimu, mwingine anataka kufanya kazi benki au urubani, yote ni sawa! lakini, je, masomo au elimu anayoisoma moja kwa moja inampeleka kuwa rubani, mwalimu, askari, mwandishi, mwanamuziki na fani zingine? Utakuta hamna.
Watu wengi wanaamini baada ya masomo kuna ajira na siyo KUJIAJIRI, wengi wanaamini wakimaliza chuo kwa masomo au mchepuo aliochukua basi atapata kazi fasta lakini kwenye uhalisia wa maisha hauko hivyo.
Somo la leo likubadilishe, uwaze namna ya kujiajiri na siyo kuajiriwa, hata kama una ndugu yako unamsomesha, msomeshe kujiajiria na si kuajiriwa, kwa kwa wanachuo hao ninaowaona baada ya kuhitimu vyuo mbalimbali sioni ajira zao zinazoweza kukidhi wingi wao.
Bila KUFIKIRIA, KUSOMA AU KUSOMESHA mwanao au mpenzi wako kwa lengo la kuja kujiajiri basi kila siku utaendelea kulalamika kuwa serikali haijatoa ajira mpya.
Binafsi sina elimu kubwa sana ya kuajiriwa ila ninaelimu kubwa zaidi ya kujiajiri.
Kuna wakati nauchukilia vibaya mfumo mzima wa elimu yetu kwa sababu tu ni kama unampotezea mtu malengo yake, muda na mambo mengine, kwani mwanafunzi anasoma akijua anakuja kuajiriwa.
Katika uhalisia hizo ajira ambazo unazifikiria hazipo, na ni ujinga kusoma ukiamini utaajiriwa na kupata maisha mazuri.
Kama una mtazamo huo, umeula wa chuya, katika uhalisia wa maisha nje ya shule ni tofauti sana. Kuna kuzunguka na vyeti weeee na kazi hakuna, kuna kuombwa rushwa za pesa au ngono, kuna upungufu wa ajira zenyewe.
Lakini kama mfumo ungekuwa unakuandaa kujiajiri bila shaka kila mtu angekula mazao yake.
Fikiria zaidi kuhusu kujiajiri hata kama uko kwenye ajira, pamoja na kwamba haiwezekani wote tukajiajiri lakini wewe ambaye umebahatika kupata fursa ya kujiajiri basi fanya hivyo.
Msomeshe mwanao kwa kile anachokipenda, mtengenezee mazingira ya kujiajiri, kuwa mzalishaji wa bidhaa ili akimaliza masomo yake ajue anachofanya.
Kama unasoma, soma kwa kujiajiri na siyo kukalia vimbweta kwa kuamini kuwa unasoma ukaajiriwe.
Ninachoamini mabadiliko yanaanza na wewe muhusika kwa kujitambua kisha kufanya yale ambayo unahisi yanastahili kufanywa na wewe au mtu yeyote anayejitambua.
Acha kuifanya akili yako kuwa tegemezi, akili yako kuiegemeza kwenye kuajiriwa. Kwani huwezi kufanya japo jambo dogo la kujiajiri angalau kwa kufungua kibanda cha pipi, machungwa au genge kwa sababu tu una amini una tuzo unayostahili baada yakuhitimu chuo.
Hii siyo nchi ya hivyo, hata huko kwingine ambako unahisi kuna ajira kibao, napo kuna shida kama huku, ila kwa kuwa mfumo wao wameufanya kujiajiri zaidi na si kuajiriwa, ndiyo maana leo hii wametuacha mbali kimaendeleo.
Kwa maoni zaidi jiunge na M&U WhatsApp kwa Na. 0657486745, Insta:mimi_na_uhusiano au tembelea ukurasa wetu kwenye Facebook; https://www.facebook.com/Mimi-na-Uhusiano-1584071311866497/
Comments are closed.