Fiston Adaiwa Kutelekeza Familia, Mkewe Amfuata Dar

 

KIMEUMANA kwa staa wa Yanga, Fiston Abdulrazak, baada ya taarifa kutoka kwa mtu wa karibu na staa huyo kudai kuwa mke na watoto wake wawili wametua Dar kuja kudai haki ya malezi ya watoto baada ya kutelekezwa nchini Burundi.

Mtoa taarifa huyo alisema mwanamke huyo yupo nchini kwa siku kadhaa sasa, akiwa ameambatana na mwanasheria wake, ambapo anataka kumchukua staa huyo na kwenda naye Mahakama ya Burundi ili kudai haki yake na watoto.

Chanzo hicho kililiambia Championi Jumatatukuwa viongozi wa Yanga wameshapata taarifa hiyo na huenda kesho (jana) wakafanya kikao kizito na mchezaji huyo ili kujua nini wanafanya na ikidaiwa baadhi ya viongozi wa juu hawajaridhishwa na kitendo hicho cha kutelekeza familia.

 

“Mke wa Fiston yupo Dar hapa kwa muda sasa, amekuja na watoto wake wawili na mwanasheria wake kuja kudai haki za malezi yake na watoto baada ya kudai Fiston aliwaacha bila msaada wowote wala kutuma fedha kwa ajili ya matumizi ya watoto wake,” kilisema chanzo chetu.

 

Championi lilifanya jitihada za kumtafuta Fiston kwa namba yake ya simu, ambayo muda mwingi ilishindwa kuunganishwa na hata alipotumiwa ujumbe haukujibiwa.Naye Mwenyekiti wa Yanga, Dkt Mshindo Msolla alipotafutwa alisema: “Mimi siwezi kuzungumzia chochote kwenye hilo suala.

 

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Mashindano wa klabu hiyo Thabiti Kandoro naye alipopigiwa ili kupata chochote simu yake iliita bila kupokelewa.

 

Fiston alitua Yanga wakati wa dirisha dogo la usajili akiwa mchezaji huru na aliingia kandarasi ya miezi sita ya kuitumikia klabu hiyo, tangu ametua kwenye timu hiyo, amefunga mabao mawili, moja kwenye ligi na lingine kwenye mechi ya Azam Sports Federation Cup dhidi ya Ken Gold FC.

Waandishi: Wilbert Molandi, Issa Liponda na Marco MZUMBETecno


Toa comment