The House of Favourite Newspapers

Fiston Mayele Aichambua Simba

0

PENGINE mabeki wa Simba kwa sasa hawataki kulisikia jina la mshambuliaji mpya wa Yanga, Fiston Mayele kutokana na kuwaumiza katika mchezo ambao bao lake lilipelekea kilio Msimbazi kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, uliochezwa Septemba 25, mwaka huu wakati Yanga ikishinda 1-0.

 

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Mkapa, Dar, Mayele alifunga bao pekee dakika ya 11 akipokea pasi kutoka kwa winga, Farid Musa, kisha akawazidi ujanja mabeki wa Simba ambao walianza katika mchezo huo, Pascal Wawa na Joash Onyango.

 

Kutokana na hilo, Mayele amewachambua mabeki wa Simba pamoja na wale wa timu pinzani ndani ya Ligi Kuu Bara ambao amefanikiwa kucheza dhidi yao katika michezo miwili msimu huu dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Mayele ameuchambua ukuta wa Simba na kusema kuwa licha ya kufunga bao, lakini ni ukuta mzuri ambao kama asingekuwa mjanja basi angepata shida kuwapa raha Yanga. Mayele aliongeza kwamba, anatamani kuwafunga tena Simba pindi watakapokutana katika michezo ijayo.

 

“Mabeki wa Simba ni wazuri, nakumbuka nilicheza nao mechi mbili wakati nikiwa AS Vita na nikashindwa kuwafunga, lakini wakati nipo Yanga nilifanikiwa kuwafunga, nashukuru hilo.

“Licha ya kufunga, lakini haikuwa rahisi, kama usingekuwa ujanja basi pengine nisingeweza kufanikiwa kupata bao dhidi yao.

 

“Hata ukiangalia lile bao ambalo nilifunga utaona ule uharaka wa kufunga nliotumia, nafahamu kuna michezo mingine huko mbele dhidi yao, natamani kuwafunga tena na nitajitahidi nafanikisha hilo jambo.

“Kwa upande wa timu za ligi kuu, kuna mabeki wazuri ambao kama mshambuliaji hautakuwa mjanja basi itakuwa ngumu kufunga.

 

“Tayari nimelitambua hilo baada ya michezo miwili ambayo nimecheza ya ligi kuu, nipo tayari kwa mapambano. Wajiandae tu,” alisema mshambuliaji huyo raia wa DR Congo ambaye ndani ya Ligi Kuu Bara bado hajafunga bao.

 

KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes, amemtabiria makubwa straika mpya wa timu hiyo, Kibu Denis kwa kusema anaamini atafunga mabao mengi msimu huu kutokana na uwezo mkubwa alionao licha ya kwamba atakabiliwa na upinzani wa namba.

 

Kibu amesajiliwa na Simba msimu huu akitokea Mbeya City, ambapo ujio wake kikosini hapo umeifanya timu hiyo kuwa na washambuliaji wanne ambao ni nahodha John Bocco, Chris Mugalu, Meddie Kagere na Kibu mwenyewe.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Gomes alisema: “Tangu msimu uliopita tulikuwa na safu bora sana ya ushambuliaji na mara zote nimekuwa nikisema navutiwa na washambuliaji wangu kutokana na uwezo mkubwa walionao. Msimu huu tumemsajili Kibu ambaye kwangu ni miongoni mwa washambuliaji bora zaidi hapa Tanzania.

 

“Najua atakutana na changamoto kubwa ya kupata nafasi mbele ya Mugalu, Bocco na Kagere, lakini ninaamini atakapoanza kupata nafasi ya kucheza atafunga mabao mengi na kuwa mchezaji muhimu zaidi ndani ya Simba kutokana na uwezo mkubwa alionao.”

JOEL THOMAS, DAR

Leave A Reply