The House of Favourite Newspapers

Flora: Mungu Amenipa Nguvu Ya Kunyamaza

0

 

 

MIONGONI mwa watu waliofanya kazi kubwa ya kuukuza muziki wa Injili Bongo, lazima jina la Flora Mayalah almaarufu Madam Flora ambaye huko nyuma alijulikana kama Flora Mbasha litatajwa.

Flora anasema ameamua kunyamaza kwa kipindi kirefu kwa sababu si kila jambo ni la kuzungumza.

Anasema hata kama utapigwa na adui yako kwa kiasi gani, kunyamaza ni tiba.

Anasema silaha kubwa aliyomuomba Mungu siku zote ni busara ya kunyamaza.

Flora anazungumza hayo kutokana na misukosuko aliyopitia miaka kadhaa iliyopita na kusababisha kuvunjika kwa ndoa yake na mwimbaji Emmanuel Mbasha ambaye walidumu pamoja kwa zaidi ya miaka kumi.

Kwenye Injili, Flora amesikika katika nyimbo nyingi zilizogusa mioyo ya wengi kama Jipe Moyo, Aliteseka, Maisha ya Ndoa, Hakuna Tatizo Kuu, Ukimwi, Tunaye Bwana, Majaribu, Asante Yesu, Kila Jambo, Tanzania, Unifiche, Faida Gani, Twende kwa Yesu, Yatima Tuwasaidie, Kwa Kupigwa Kwake, Alale kwa Amani, Tupendane na nyingine nyingi.

Kama ilivyo desturi ya Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, limefanya mahojiano maalum (exclusive) na Flora ambapo amefunguka mambo mengi juu ya ukimya wake baada ya tukio lile la kuvunjika kwa ndoa yake na kuolewa na mwanaume mwingine aitwaye Daud Kusekwa;

IJUMAA WIKIENDA: Flora umekuwa kimya kwa muda mrefu, nini kimetokea?

FLORA: Ni kweli nimekuwa na muda mwingi wa kukaa na kutafakari mambo mengi, lakini sasa nimerudi kwa kishindo na wimbo wangu mpya wa Mwenye Majibu ambao nimeshirikiana na Goodluck Gozbert.

IJUMAA WIKIENDA: Kwenye Injili kuna wanamuziki wengi, kwa nini umemchagua Goodluck Gozbert?

FLORA: Nimefanya na Good (Goodluck Gozbert) kwa sababu siku zote huwa napenda kazi zake na jinsi anavyojituma na nilitamani siku moja kufanya kazi tu pale Bwana atakapotoa kibali, hivyo wakati wa Bwana umefika na nimefanikiwa.

IJUMAA WIKIENDA: Wimbo huu una ujumbe gani ulioamua kuufikisha?

FLORA: Ni Mungu pekee ndiye mwenye majibu ya kila tatizo. Inapofika mahali unaona umekwama, hakuna jawabu lingine zaidi ya Mungu. Wimbo huu ukiusikiliza, hakika utaona ukifunguliwa kutoka mahali ulipokwama, yupo mwenye majibu, huwezi kupata majibu kwa mganga wa kienyeji au rafiki, isipokuwa majibu ya kweli yapo kwa Mungu pekee.

IJUMAA WIKIENDA: Huko nyuma ulikuwa kwenye familia ya waimbaji wawili, vipi kwenye familia yako hii mpya mumeo naye ni mwimbaji?

FLORA: Mume wangu siyo mwimbaji, lakini anapenda sana muziki wangu. Hivyo, ananisapoti kwa asilimia kubwa.

IJUMAA WIKIENDA: Kuna vitu vingi sana vilizungumzwa juu yako kipindi cha nyuma ulipopata matatizo, lakini mara nyingi ulikuwa ukinyamaza tu, ni kwa nini ulikuwa kimya?

FLORA: Siyo kila kitu ni cha kujibu na hata ukijibu huwezi ukabadilisha mtazamo wa kila mtu kwa majibu yako. Hivyo, niliona ni bora kunyamaza na kuomba ili Mungu ajibu kwa wakati. Mungu huwa hatumii nguvu kubwa, ni vitendo tu, lakini ukilazimisha wewe kujibu unaweza ukauza hata nyumba ili ulipe watu wa ‘media’ wakuandike kila siku. Lakini wakati wa Bwana ukifika, kila kitu kinajibiwa bila gharama. Ni maombi tu. Hivyo kukaa kimya ni hekima.

IJUMAA WIKIENDA: Huko nyuma ulikuwa ukiimba na aliyekuwa mumeo Mbasha kwa kunogesha vionjo vya hapa pale, hivyo kutengana kwenu pia kulishusha muziki wako, unazungumziaje hilo?

FLORA: Siku zote maswali ambayo yanahusu maisha yangu ya nyuma, huwa sipendi kuyajibu kabisa sababu tayari nina maisha mengine tofauti. Sioni manufaa kwangu na kwa jamii pia.

IJUMAA WIKIENDA: Ila hiyo ni kwa ajili ya muziki wako wa huko nyuma na kutaka kujua tofauti iliyopo.

FLORA: Nikitaka kuzungumza lolote kuhusu familia, basi litahusu maisha yangu mapya na siyo ya zamani. Sipendi kuzungumzia maisha mengine tofauti na huduma yangu.

IJUMAA WIKIENDA: Binti yako Elizabeth au Lizy uliyezaa na Mbasha mara nyingi anaonekana na baba yake wakiwa sehemu tofauti na watu kuanza kuzungumza vibaya, hilo unazungumziaje?

FLORA: Yule ni baba yake, hivyo ana haki, siwezi kumzuia kwa hilo.

IJUMAA WIKIENDA: Siku hizi muziki wa injili umepoa siyo kama zamani, unafikiri tatizo ni nini?

FLORA: Kila jambo lina wakati wake. Sasa hivi waimbaji ni wengi siyo kama kipindi chetu tulipokuwa wachache. Huwezi kuwasikia wote kwa wakati mmoja. Lakini ni jambo zuri maana Injili inahubiriwa kupitia muziki.

IJUMAA WIKIENDA: Baada ya wimbo wako mpya, tutarajie kuwa kutakuwa hakuna kupumzika?

FLORA: Nategemea kutoa nyimbo nyingine na nyingine hadi nikamilishe album hadi kieleweke.

MAKALA: IMELDA MTEMA

 

Leave A Reply