Forbes Yamtaja Rais Samia Orodha ya Wanawake 100 Wenye Nguvu Duniani

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametajwa na Jarida maarufu duniani la takwimu na ripoti la Forbes katika orodha ya wanawake 100 wenye nguvu zaidi duniani kwa mwaka 2021.

 

Orodha hiyo inayojumuisha wanawake waliopo kwenye nyadhifa mbalimbali za juu duniani, wakiwemo marais, wafanyabiashara wakubwa na watu mashuhuri, imetangazwa leo, Desemba 7, 2021 na Jarida hilo kupitia tovuti yao ya www.forbes.com.

 

Rais Samia ambaye aliingia madarakani Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ametajwa kuwa katika nafasi ya 94 ya wanawake wenye nguvu zaidi ulimwenguni, huku uongozi wake imara na mapambano dhidi ya Corona, zikiwa ni sifa zilizompaisha zaidi pamoja na umahiri wake katika uongozi tangu alipoingia madarakani, hotuba aliyoitoa katika Baraza la Umoja wa Mataifa (UN) na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona.

 

Nafasi ya kwanza katika orodha hiyo inayojumuisha wanawake wanaofanya vizuri dunia nzima katika nyanja mbalimbali kama uongozi, biashara, ubunifu na burudani, imeshikwa na mwanamama bilionea, MacKenzie Scott (Mtalaka wa Jeff Bezos), raia wa Marekani ambaye pia yupo kwenye nafasi ya tatu ya wanawake mabilionea duniani.

 

Nafasi ya pili imeshikwa na Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris huku nafasi ya tatu ikishikiliwa na Rais wa Benki ya Ulaya, Christine Lagarde wa Ufaransa.

 

Mwanamama Ozlem Tureci, mwanzilishi mwenza wa Kampuni ya BioNTech naye ametajwa kuingia katika orodha hii kwa mara ya kwanza kutokana na umaarufu alioupata kwa kugundua chanjo ya Corona ya Pfizer.

 

Wanawake wengine waliopo kwenye orodha hiyo, ni pamoja na Malkia Elizabeth II wa Uingereza, Rais Tsai Ing-wen wa Taiwan na viongozi wengine wengi wa mataifa mbalimbali duniani.

 

Kwa upande wa tasnia ya habari, michezo na burudani, mwanamama Oprah Winfrey ameendelea kung’ara sambamba na wasanii kama Beyonce Knowles, Rihanna, Taylor Swift na Serena Williams wameng’ara kwenye tuzo hizo.

Imeandaliwa na Aziz Hashim kwa msaada wa mitandao.

 


Toa comment