FREEMASON, UCHAWI VYATEKA MAKANISA BONGO

DAR ES SALAAM: SIKU za mwisho watatokea manabii wengi wa uongo! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na maandiko yaliyopo kwenye Biblia takatifu kwani kwa sasa hali ni mbaya makanisani, Amani limedokezwa. 

 

Madai mazito ni kwamba kuna vita mpya katika ya shetani na kanisa la Mungu ambapo jamii ya siri inayohusishwa na imani za kishetani na uchawi vinadaiwa kuteka makanisa mengi Bongo. Chanzo makini ambacho kiliomba hifadhi ya jina kililieleza Amani kuwa, kuna makanisa mengi kwa sasa Bongo ambayo yanatumia nguvu za giza ili kuvuta waumini ambapo yamejaa kila kona na yana waumini wengi.

ISHU NI MIUJIZA

Ndani ya makanisa hayo kuna yanayotumia na kusujudu nembo za Freemason wakiamini kwamba ndiyo Mungu wao ambaye anawatendea miujiza kama kuwaponya magonjwa, kuwafanya wawe matajiri na miujiza mingine mingi.

 

Chanzo hicho ambacho ni mtumishi wa Mungu kiliendelea kueleza kuwa, pamoja na hayo yanayotumia nguvu za Freemason yapo mengine yanayotumia uchawi ambapo yanagawa maji, mafuta, chumvi, mchanga na vinginevyo ambapo waumini wanajikuta wakiamini katika vitu hivyo.

 

UTAPELI MTUPU

“Wapo watu wamejikuta wakitapeliwa kwenye makanisa haya kwani hasa ukionekana wewe ni tajiri kuna hao wanaojiita manabii wanakwambia upeleke fedha kanisani akaziombee, ukishapeleka unaziacha ziombewe, lakini kila ukienda kuzidai hupewi hapo unakuwa umeshatapeliwa tayari.

 

“Licha ya utapeli huu na nguvu hizo za kichawi, lakini bado waumini hawashtuki, wanaendelea tu kuabudu kwenye makanisa haya, jambo ambalo linaendelea kuwapoteza zaidi kiimani na kiuchumi kwani wapo wanaojikuta wanawajengea nyumba za kifahari watumishi wao huku wenyewe wakiwa hawana hata kiwanja, tuwe macho jamani,” kiliweka nukta chanzo hicho.

MCHUNGAJI ANENA

Kufuatia habari hizo, Amani lilifanikiwa kuzungumza na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Mbezi- Beach jijini Dar, Christosiler Kalata ambaye alifunguka mazito.

 

Mchungaji Kalata alikiri kuwa, kwa sasa kila kona kumejaa madhehebu yanayopinga kweli ya Mungu kama ambavyo imeandikwa kwenye Biblia, Mungu alitahadharisha kwamba siku za mwisho watatokea manabii wengi wa uongo.

 

Akaendelea kusema kuwa katika Mathayo 24:24 Bwana Yesu alitahadharisha kuwa watatokea manabii wa uongo au watumishi ambao wanapinga ile kweli ya Mungu, sasa haya yanayotokea ni mambo ambayo Bwana Yesu aliyasema.

 

“Sasa hivi mpinga Kristo ambaye tunasoma kwenye Kitabu cha Ufunuo yupo kazini na siyo kwamba ameshafunguliwa aje duniani, bali yale mambo ambayo yanapinga kazi ya Mungu yameshaanza kutokea na kila mtu anayaona kwa hiyo roho wa shetani anamwingia mwanadamu anafanya yaliyo kinyume na neno la Mungu.

 

“Kwa hiyo sasa hivi yapo madhehebu yanayopinga kazi ya Mungu, yanajifanya yanaanzisha makanisa kumbe yanaanzisha shughuli ambazo zinapinga kweli ya Mungu, hivyo kwa wakati huu ambao watu wanasema ni soko huria na ulimwengu wa utandawazi, watu waachwe huru kufanya mambo yao, shetani anatumia huo uhuru kufanya mambo ambayo ni kinyume na mapenzi ya Mungu.

 

“Wanaopinga kweli ya Mungu hawaonekani waziwazi kwa kuwa wanatumia neno la Mungu kwa kisingizio kwamba katika Mathayo 28:18-19 wameambiwa kwamba waenende wakahubiri Injili duniani kote, wanatumia neno hilo kuwadanganya waumini wao,” alisema Mchungaji Kalata. Hata hivyo, aliwataka waumini kuwa macho na kumuomba Mungu awaoneshe tofauti ya roho wa Mungu na wa shetani.

ATAHADHARISHA SERIKALI

Mchungaji huyo aliitahadharisha Serikali kuwa isiangalie watu wakiendelea kuumizwa huku makanisa yakiachwa bali hawa wahusika washughulikiwe kwani ni wahalifu hivyo wachukuliwe hatua kama wahalifu wengine.

 

“Mfano ni wale wachungaji waliokuwa wanalaza wagonjwa kanisani kule Bukoba na kuwachapa huku wengine wakipoteza maisha pamoja na kupata madhara makubwa na Serikali kuwanusuru waumini wale kama isingekuwa hivyo ingekuwa ni madhara makubwa, hivyo naomba Serikali iangalie makanisa au madhehebu haya yanayoanzishwa kila kona,” alisema Mchungaji.

 

NABII NYAKIA

Akizungumzia ishu hiyo, Nabii wa Kanisa la Jerusalemu lililopo Wilaya ya Ilala eneo la Nyantira Mtaa wa Kiyombo jijini Dar, Nabii James Nyakia alisema kuwa, kuna makanisa yapatayo 15 nchini, yanayoendekeza imani za kishetani za Freemason, uchawi na kufuga misukule.

 

Nabii Nyakia alisema muda ukifika atayataja makanisa hayo, huku pia akibainisha kuwa kuna wachungaji wengi wanajaza waumini makanisani mwao, lakini wanatumia nguvu za giza.

 

NABII MKUU GEORDAVIE

Hivi karibuni, Nabii Mkuu wa Kanisa la Ngurumo ya Upako jijini Arusha, Dk Geordavie alifanikiwa kumrejesha kijana aliyedaiwa kuingia mkataba na Freemason ambapo aliichoma mikataba hiyo kanisani kwake. Katika tukio hilo, Dk Geordavie alikiri makanisa mengi Bongo kuvamiwa na jamii hiyo huku akisema kuwa kanisa la Mungu lina kazi kubwa ya kufanya ili kukomboa watu wa Mungu.

 

KAULI YA SERIKALI

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, aliagiza uhakiki wa makanisa na misikiti nchi nzima ili kuzifuatilia taasisi za dini kujua utendaji wake wa kazi unaendana na sheria za usajili.


Loading...

Toa comment