The House of Favourite Newspapers

FUMANIZI LA DENTI, RAIA WA KIGENI LAFYATUKA

AMA kweli duniani kuna watu wasiosikia ambao kwa hapa nchini wanamchezea sharubu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli, Uwazi linafichua!

NI DENTI WA FORM ONE

Denti wa kidato cha kwanza (form one) katika Shule ya Mwembetogwa Manispaa ya Iringa, amefumaniwa gesti akiwa chumbani akidaiwa kumfuata mwanaume, raia wa kigeni kutoka nchini Uganda baada ya mtego kufyatuka.

POLISI WATINGA

Tukio hilo lililonaswa na Uwazi lilijiri majira ya saa 3:00 asubuhi mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye gesti moja iliyopo eneo la Veta katika Manispaa ya Iringa ambapo Polisi walilazimika kutinga na silaha kufuatia kuibuka kwa timbwili. Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo liliacha maswali mengi kuliko majibu kwa wakazi wa Mji wa Iringa na Polisi walifanya kazi ya ziada kutuliza ghasia za wananchi ambao walitaka kutembeza kichapo kwani hawakufurahishwa na tabia hiyo.

WATAKA KUCHOMA MOTO

Wakizungumza na Uwazi, wananchi hao walisema kuwa walitaka kuchoma moto nyumba hiyo kabla ya Polisi kufika na kufanya kazi yao ya kuhakikisha kunakuwa na usalama wa raia na mali zao.“Inaumiza sana maana wazazi wanahangaika mno kulipa ada ili watoto wasome, lakini anatokea mtu ambaye anawakatisha masomo kwa kufanya ngono na watoto kama hawa ambao ni chini ya miaka 20.

“Tulitaka kuonesha tuna hasira, kama siyo kutembeza kichapo, basi kuiteketeza nyumba kwa moto,” alisema Zainab Ally, mmoja wa wananchi hao na kuongeza: “Hata wenye gesti hii wana makosa makubwa kuruhusu mtoto kama huyu kuingia chumbani kuvunja amri ya sita wakati sheria ipo wazi kabisa, inakataza watoto kama hao kuingia maeneo ya starehe ikiwemo gesti kwa lengo la kufanya ngono.”

HUYU HAPA MHUDUMU

Kwa upande wake, mhudumu wa gesti hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Zuhura alisema kuwa, mwanafunzi huyo alifika eneo hilo majira ya saa 3:00 asubuhi akimuulizia raia huyo wa kigeni. Ilidaiwa kwamba, baada ya kumuulizia mwanaume huyo aliyedai kuwa ni mpenzi wake bila kupewa jibu, aliendelea kuzurula ndani ya gesti hiyo.

AINGIA CHUMBANI

“Baada ya kutompa ushirikiano, niliendelea na usafi kabla ya kubaini kuwa binti huyo alikuwa ameingia chumbani. “Kumbe yule denti alikuwa amewekewa mtego baada ya kufuatiliwa na mjomba wake.

“Ghafla nilipigwa na butwaa baada ya kuona nyumba imevamiwa na mjomba mtu na wananchi ambao walikuwa na lengo la kumkamata huyo mwanaume aliyemrubuni mwanafunzi huyo. Baadaye polisi nao wakaitwa maana kulikuwa na dalili za amani kupotea.”

Katika maelezo yao baada ya kumkosakosa mwanaume huyo ambaye alifanikiwa kuwatoroka, walielezwa kwamba, jamaa huyo ni mgeni ambaye alipanga kwenye gesti hiyo siku nyingi akiwa anafanya kazi ya kuendesha gari la watalii katika hifadhi mbalimbali za mkoani Iringa.

AFUMANIWA LAIVU

Hata hivyo, mhudumu huyo alisema kuwa, wakati polisi wakifika hapo ndipo yule mwanaume alipotoka nduki na kumwacha binti huyo chumbani ambapo alifumaniwa laivu.

Kwa upande wake, mwanafunzi huyo ambaye jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili alisema kuwa, katika nyumba hiyo ya kulala wageni alimfuata mpenzi wake ambaye ni Mganda waliyekubaliana wakutane mahali hapo. “Alipita nyumbani kwetu, akaniambia nimfuate bila kujua mjomba alikuwa ananifuatilia,” alisema denti huyo na kuongeza: “Ni kweli ni muda wa kuwa shuleni, lakini nilirudishwa nyumbani na walimu.”

Kwa upande wa mama mzazi wa denti huyo ambaye hakupenda jina kuandikwa gazetini alisema: “Baada ya kurudishwa nyumbani alivua sketi ya shule na kuvaa kikoi na shati la shule kisha kuja huku gesti na kwa kuwa tulikuwa tukijua kuwa huwa anakuja huku, mjomba wake alianza kumfuatilia hadi hapa.

“Huyu mwanangu hapa alipo mbali na kujifunga kikoi ndani hajavaa chochote na ninahisi ni tabia yake siku zote kwani mwenendo wake si mzuri na nasema leo atanitambua, haiwezekani nipoteze pesa na maisha yalivyo magumu hivi, yeye anaacha masomo na kuja kufanya ufuska huku gesti,” aliwaka mama wa denti huyo akionesha kuwa na hasira.

UCHUNGUZI ZAIDI

Hata hivyo, baada ya kushindwa kumkamata mwanaume huyo polisi walilazimika kumkamata rafiki wa mtuhumiwa huyo ambaye naye ni raia wa Uganda kwa uchunguzi zaidi huku wakimtaka bosi wake (Mzungu) kuhakikisha anampeleka polisi mfanyakazi wake huyo.

KAMANDA WA POLISI

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, ACP Juma Bwire alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa bado wanaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo.

STORI: FRANCIS GODWIN, IRINGA

Comments are closed.