FUNDI ASIYEONA AIBUA MAPYA YA MENGI

K UMBUKUMBU ya maisha aliyoishi mfanyabiashara bilionea marehemu Dk. Reginald Abrahamu Mengi haijatoka miongoni mwa jamii; fundi mlemavu wa macho aitwaye Abdalah Nyangario (59) ameibuka na mapya kumhusu tajiri huyo aliyezikwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Nyangario mkazi wa Mbagala jijini Dar, aliliambia Ijumaa Wikienda katika mahojiano maalumu yaliyofanyika hivi karibuni kuwa, kabla mfanyabishara huyo hajafariki dunia, kuna kazi ya kushonewa shati aliiacha kwa fundi huyo. “Pamoja na ulemavu wangu, nimemshonea nguo kadhaa marehemu Mengi, hata kabla hajaondoka kwenda Dubai, katika Nchi za Falme za Kiarabu alikofia, aliniambia nimshonee shati, akirudi angekuja kulichukua,” alisema fundi huyo.

Nyangario ambaye alipoteza uono wa macho miaka 30 iliyopita aliongeza kusema kwa masikitiko kuwa mzee Mengi alikuwa ni mtu muhimu kwenye maisha yake na kwamba kifo chake kimeacha pengo lisilozibika.

NYANGARIO NA MENGI WALIVYOKUTANA

Nyangario anaendelea kueleza kwamba, alikutana na Dk. Mengi miaka kadhaa iliyopita katika hafla ya chakula cha mchana alichokiandaa mfanyabiashara huyo kwa ajili ya kushiriki upendo na watu mbalimbali wenye ulemavu ambao alikuwa akila nao chakula kila mwaka. “Nakumbuka kwa mara ya kwanza nilikutana na mzee Mengi katika chakula hicho,

baada ya hapo aliniita ofisini kwake nikaenda tukaongea mambo mengi na mwisho akanipa oda ya kumshonea shati. “Nadhani alikuwa anataka kunijaribu aone kama naweza, nilipomshonea shati akalipenda na kunipa kazi nyingine ya kushona suti ambayo nayo niliifanya.

“Siku za mwishomwisho  nilikutana naye tena akaniambia nimshonee shati ambalo angekuja kulichukua akirudi, lakini kabla hata hajaja ndiyo nikapata taarifa za kifo chake, niliumia sana,” alisema fundi huyo ambaye amekuwa akiwashonea nguo watu mbalimbali maarufu nchini.

AOMBA NDUGU WAKALICHUKUE SHATI

Kutokana na ukweli kwamba kazi ya ushonaji wa shati hilo ilikuwa imekamilika mlemavu huyo anawaomba ndugu au watoto wa marehemu Mengi waende wakalichukue.

“Siwezi kuendelea kukaa nalo kama kumbukumbu, mimi nililishona kwa mapenzi yangu, hivyo naomba watoto wa marehemu Abdiel na Regina waje walichukue halafu watajua wao sehemu ya kulipeleka,” alisema Nyangario.

MENGI ALIKUWA AKIMLIPA SHILINGI NGAPI?

Fundi huyo mlemavu alisema kwamba mara zote alipopewa oda na mzee Mengi hawakuwa wakipatana bei lakini yeye alikuwa akishona kwa mapenzi na kuwa tayari kulipwa au kutolipwa. “Nilikuwa simshonei nguo marehemu Mengi kwa malipo, nilikuwa namshonea bure, lakini nilikuwa nikimaliza kazi yeye ananipa hela ambazo nilikuwa

nashindwa kuzikataa. “Nilipomshonea shati la kwanza na kumpelekea alinipa shilingi laki moja na nusu akaniambia ni za nauli, mara ya pili nilipomshonea suti alinipa shilingi laki tano akaniambia niende kununua vifaa kwa ajili ya ufundi wangu,” alisema Nyangario. ANAWEZAJE KUSHONA WAKATI HAONI? Najua kila mtu lazima atakuwa anajiuliza swali kama ambalo hata mimi nimekuwa nikijiuliza; lakini ukweli ni kwamba fundi huyo mlemavu ana uwezo mkubwa wa ajabu wa kushona nguo kwa kutumia cherehani bila tatizo lolote.

“Naweza kushona vizuri tu bila matatizo; wewe mwenyewe si unaona,” alisema mlemavu huyo ambaye mwandishi wetu alipata nafasi ya kumtembelea ofisini kwake kujionea stadi yake ya ufundi. Aidha, aliongeza kusema: “Watu wengi wa hapa mtaani kwetu hawaniamini na wengi wao hawaleti nguo zao hapa niwashonee kwa kudhani kwamba nitawaharibia, kitu ambacho si kweli. “Nguo nyingi ninazoshona zinatoka mbali sana siyo hapa mtaani kwangu,” Nyangario alisema huku akiwaomba watu waache kumtazama kama mlemavu bali fundi mwenye uwezo mkubwa pengine kuwashida hata wanaoona.

CHANGAMOTO ZAKE NI ZIPI?

Fundi huyo anasema mbali nakutoaminiwa na baadhi ya watu lakini pia changamoto kubwa anazokumbana nazo kila siku ni pamoja na kujikatakata na vitendea kazi vyake ambavyo ni mikasi na sindano.

“Napitia changamoto nyingi sana, mfano nimeshawahi kukatwa na mkasi, pia kuchomwa na sindano mara kwa mara.

 WATU MAARUFU ALIOWASHONEA NGUO

Pamoja na ulemavu wake fundi huyo anasema kwamba mbali na kumshonea marehemu Mengi pia ameshawahi kumshonea Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete. “Ukiacha huyo mwingine ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya Nasibu Abdul ‘Diamond’ na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka” alisema.

AOMBA MSAADA

Kutokana na changamoto anazokabiliana nazo, fundi huyo amesema anawaomba wasamaria wema wajitokeze kumsadia ili naye aweze kuboresha maisha kupitia ujuzi wake. “

Nimekuwa na tabia ya kuwashonea nguo watu maarufu bure kama njia ya kujitangaza, kwa mfano Diamond nilimshonea akaipeda na kuniambia atanitafuta; lakini hajanitafuta hadi leo. “Hii nyumba ninayoishi hapa siyo yangu ni ya urithi, hata mazingira yangu ya kazi siyo rafiki sana natamani nipate maeneo ya Kariakoo au Makumbusho ya Taifa ili niweze kufanya kazi vizuri kwa sababu huku niliko nimejificha hivyo inakuwa ngumu wateja kunipata kwa urahisi,” alisema fundi huyo na kutaja namba zake za simu kuwa ni 0717 315 011/ 0687 350 132, ambazo wasamaria wema wanaweza kumtafuta kwa msaada wowote.

Loading...

Toa comment