The House of Favourite Newspapers

Gadiel anusuru usajili wa rasta Yanga

USAJILI wa beki wa pembeni, Gadiel Michael Simba umemnusuru kiraka rasta wa Yanga, Jaffari Mohammed kuendelea kubakia kuichezea timu hiyo.

 

Kiungo huyo, awali hakuwepo kwenye orodha ya wachezaji iliyotolewa na Yanga ambao wamewasajili kwa ajili ya msimu mpya wa ligi utakaoanza Agosti 23, mwaka huu.

 

Kiraka huyo aliondolewa katika usajili huo baada ya kupendekezwa kuachwa au kuondolewa kwa mkopo.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, Kocha Mkuu wa timu hiyo Mkongomani, Mwinyi Zahera amesitisha mipango ya kumuacha kiraka huyo baada ya Gadiel kusaini Simba.

 

Mtoa taarifa huyo alisema, Jaffari amebakishwa kutokana na umahiri wake wa kucheza nafasi zaidi ya moja ndani ya uwanja ikiwemo kiungo mshambuliaji, mkabaji na nafasi zote za beki wa pembeni namba 2 na 3.

 

Aliongeza kuwa, licha ya kumsajili beki mpya wa kushoto, Muharami Salum ‘Marcelo’ aliyetokea Singida United aliyekuja kuchukua nafasi ya Gadiel aliyetimkia Simba, bado Zahera aliona umuhimu wa kumbakiza Mohammed ili wasaidiane.

 

“Kocha alipendekeza kila nafasi tusajili wachezaji wawili wote kwa kuanzia golini, mabeki, viungo na washambuliaji na lengo ni kuwa na kikosi kipana katika timu.

 

“Jaffari tumemrejesha kikosini katika kuiimarisha safu yetu ya ulinzi ya pembeni ambayo ni namba tatu baada ya Gadiel kuondoka na kutokana na umahiri wake mkubwa wa kucheza nafasi zaidi ya moja.

 

“Hivyo, Jaffari tayari yupo kambini tangu jana (juzi) mara baada ya kupewa taarifa hizo, ”alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh kuzungumzia hilo alikiri kuwepo kwa kiraka huyo kambini kwa kusema: “Jaffari yupo kambini tangu jana (juzi) hapa mkoani Morogoro. Kama yupo kambini huku Yanga, basi ujue ni mchezaji halali wa Yanga hivyo tunatarajia kuwa naye katika msimu mwingine.”

Comments are closed.