Gadiel: Nimesaini Simba Miaka Miwili – EXCLUSIVE

GADIEL Michael amelitumia Spoti Xtra kuwaweka wazi mashabiki kuhusiana na utata wa usajili wake. Beki huyo aliyeng’ara Yanga msimu uliopita, ameweka wazi kwamba amesaini mkataba wa miaka miwili na anaamini atafanya kazi kubwa Msimbazi katika ligi ya ndani na michuano ya kimataifa.

 

Gadiel alikuwa na mvutano wa muda mrefu juu ya kuongeza mkataba Yanga baada ya ule wa awali kufikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu lakini hatimaye ametua Simba. Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla juzi alitamka kwamba; “Hatuwezi kubabaishwa na mchezaji kama anataka kuondoka aondoke.”

 

Beki huyo anakuwa mchezaji wa tatu kutua Simba akitokea Yanga kwa mkataba wa miaka miwili kwa dau la milioni 60. Wengine ni kipa mahiri Beno Kakolanya na mkali wa asisti, Ibrahim Ajibu.

Gadiel ameliambia Spoti Xtra linalotoka kila Alhamisi na Jumapili kuwa, anakwenda Simba kwa kazi moja tu ya kuhakikisha anapambana ili kufanya vizuri. “Ndiyo nimesaini Simba mkataba wa miaka miwili na ninakwenda huko kwa ajili ya kupambana ili kufanya vyema katika timu yangu hiyo mpya,” alisema mlinzi huyo.

 

“Mimi ni mchezaji ninachoangalia ni maslahi zaidi na nimekwenda huko kutokana na kuvutiwa na Simba,” alisema Gadiel ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Taifa Stars.

 

Beki huyo kisiki mwenye umbo la wastani sasa anakwenda kuwania namba mbele ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye ni nahodha msaidizi Simba.

 

YANGA NA SONSO Yanga wamekiri kwamba kuondoka kwa Gadiel kutamlazimu Ally Mtoni ‘Sonso’ kubeba mzigo mkubwa mpaka wakati wa dirisha dogo la mwezi Desemba.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla amesema; “Sisi kitu tunachosikitika ni kuona ametucheleweshea muda tu wa kutuambia kama hatasaini kwetu, lakini tayari tumeshamuandaa Sonso kuwa mbadala wake kwa muda huu ligi itakapoanza.”

“Lakini Desemba, katika usajili mdogo tutamchukua mbadala wake ambaye atakuja kuongeza nguvu katika kikosi chetu,”

KHADIJA MNGWAI NA SAID ALLY, DAR

KONGAMANO LA NABII NATASHA TABATA LIWITI MUDA HUU

Loading...

Toa comment