Gaidi alivyojirusha ghorofani

Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam chini ya Kamishna Suleman Kova wameachwa midomo wazi baada ya mtuhumiwa wa ugaidi, Ali Mohamed Uletule (65) kujirusha kutoka ghorofa ya tatu na kudondoka chini kwa lengo la kutaka kutoroka, Uwazi lina mkanda kamili.

Mtuhumiwa huyo akiwa hoi baada ya kujirusha.

Tukio hilo lilijiri wiki iliyopita wakati Uletule akihojiwa katika Ofisi ya Upelelezi Kanda Maalum jijini Dar ambayo ipo katika ghorofa ya tatu kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar (central) kilichopo Barabara ya Sokoine.
Katika tukio hilo lililozua taharuki, baadhi ya polisi waliokuwepo katika jengo hilo siku ya tukio walisimulia:

“Kwa kweli tukio kama hili halijawahi kutokea kwenye ofisi yetu. Ni hatari sana na hatukutarajia kama hali kama hii ingetokea, inabidi kuwa makini sana na watu kama hawa na hapa alitegemea kwamba angeruka na kuondoka bila kukamatwa.”


MBINU ALIZOTUMIA

Duru za kihabari ndani ya jeshi hilo zilinyetisha kwamba, siku ya tukio, mtuhumiwa huyo alikuwa akihojiwa lakini kuna muda alijifanya kushika chini ya tumbo huku akidai tumbo linamkata na alijisikia kuharisha hivyo aliomba apelekwe maliwato asije akajichafua kwenye nguo mle ofisini.

Hata hivyo, taarifa hizo zilidai kwamba, baada ya kuwa katika hali hiyo ilibidi polisi wamruhusu kwenda kujisaidia akiwa chini ya ulinzi.Ilielezwa kuwa ghafla polisi walishtuka kumuona jamaa huyo ameshawaacha na kuruka chini jambo lililoibua mshtuko mkubwa.

Ilisemekana kwamba baada ya kudondoka chini, mtuhumiwa huyo alishindwa kukimbia kwa sababu alidondokea katika pikipiki zilizoegeshwa chini hivyo akapoteza fahamu.Habari zilieleza kwamba, polisi waliokuwa chini la jengo hilo walipata hofu hivyo walikuwa wakikimbia huku na kule kwa lengo la kumkamata.

Mshangao huo haukuwa kwa askari tu waliokuwa juu bali hata waliokuwa chini kwa sababu walisikia kishindo kikubwa ambapo walijiweka sawa kisha wakamchukua mtuhumiwa huyo na kumkimbiza kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Uwazi lilimfuatilia mtuhumiwa huyo Muhimbili na kumkuta akiwa amelazwa katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa (Moi) akiendele na matibabu chini ya ulinzi wa polisi.

MUHIMBILI WANASEMAJE?
Kaimu Afisa Uhusiano wa Moi, Patrick Mvungi alipoulizwa juu ya mgonjwa huyo alikiri kuwepo kwake na kwamba alifikishwa hospitalini hapo na polisi akiwa na maumivu sehemu mbalimbali za mwili wake.Afisa huyo alisema kwamba, mtuhumiwa huyo alivunjika mkono na mguu wa kushoto ambapo alitibiwa na kesho yake aliruhusiwa akiwa na polisi.

Habari za kina zinaeleza kwamba, mtuhumiwa huyo ni mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya Uletule ambapo wa kwanza ni Seleman Shaban Uletule ambaye naye anasakwa na polisi.

Imefahamika kwamba, polisi na vyombo vyote vya usalama chini ya Kamishna Kova wanafanya msako mkali dhidi ya watu wanaoshukiwa kuwa ni magaidi mara baada ya tukio la kuvamiwa kwa Kituo cha Polisi cha Stakishari na kuuawa kwa polisi watatu na raia wanne.

Hivi karibuni katika mazungumzo na waandishi wa habari, Kamishna Kova (pichani) alisema kwamba, mtuhumiwa huyo alijirusha baada ya kutumia mbinu ya kijasusi ya kuomba aruhusiwe kwenda maliwatoni kwa kisingizio cha kuvurugikiwa na tumbo.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!


Loading...

Toa comment