The House of Favourite Newspapers

Gari la mbunge latikisa TRA

0

4a547-1Mbunge wa Korogwe Vijijini Steven Hillary Ngonyani ‘Maji Marefu’.

Na Mwandishi Wetu
TRA ya Magufuli! Gari la Mbunge wa Korogwe Vijijini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Steven Hillary Ngonyani ‘Maji Marefu’ (pichani) linadaiwa kuzitikisa ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizopo Barabara ya Sokoine jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mtumishi mmoja kutoka ofisi hiyo, baadhi ya maofisa wanaamini gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser ‘Super Charger’ lina ukwepaji wa kodi jambo ambalo limesababisha watu kulisaka faili lake ofisini hapo.

MSIKIE HUYU
“Jamani nyie watu wa Uwazi kwanza mmeliona gari la Maji Marefu, yule mbunge wa Korogwe? Bonge la gari. Lina namba za jina lake la Maji Marefu. Ni Toyota Super Charger new model (muundo mpya).

MAJI MAREFUToyota Land Cruiser VX.

“Sasa kuna wasiwasi kwamba, jamaa hajalipa kodi. Maofisa wanalisaka faili lake. Nadhani kama ni kweli, siku mbili hizihizi mtasikia habari yake maana hii kasi ya Rais Magufuli ya kutumbua majipu ni balaa,” kilisema chanzo hicho.

THAMANI YA GARI
Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa, gari hilo linakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni mia mbili na hamsini (250,000,000).

“Kama ni kweli mheshimiwa huyo ambaye alitoka kuapa bungeni mwezi uliopita, atajikuta ndani ya matatizo makubwa. Anaweza kupata msukosuko kutoka TRA,” kilisema chanzo.

MAKAMISHINA WAPISHANA LUGHA
Hata hivyo, chanzo hicho kilisema kuwa, kumekuwa na lugha za kupishana kwa makamishina wa TRA ambapo kuna wanaosema gari hilo halina tatizo huku wengine wakisema lina tatizo.

“Sawa wanaosema halina tatizo wanatakiwa kuweka faili lake mezani kama kweli lipo lakini faili haliwekwi jambo ambalo wengine wanasema halipo,” kilisema chanzo.

UWAZI TRA
Ijumaa iliyopita, gazeti hili lilikwenda kwenye ofisi hizo na kuomba kuonana na msemaji au ofisa yeyote lakini ikasemekana kuwa wahusika wa kufafanua ishu hiyo wako mitaani wanakamata magari yasiyolipiwa kodi.

MAJI MAREFU ASAKWA
Jumapili, Uwazi lilimsaka kwa simu mbunge huyo na kumuuliza kuhusu madai ya gari lake kukwepa kodi ambapo alisema:

“Dah! Nani kasema? Hili gari sidaiwi na mtu aisee! Nimelinunua kwa uhalali na lipo kwangu kihalali. TRA nimewalipa kodi shilingi milioni 69,773. Hawanidai hata senti tano.

“Limeandikishwa tarehe 26, Novemba 2015. Kwa sasa ‘pleti namba’ imeandikwa Maji Marefu, nimelipia shilingi milioni 5. Inshuarensi (bima) nilikata kampuni ya UAD kwa shilingi milioni 8, 950 kupitia Benki ya CRDB. Huyo anayasema nadaiwa hajui lolote, anyamaze.

“Kabla ya pleti namba kusomekana Maji Marefu lilikuwa na namba za usajili T 666 DFS. Unasikia bwana. Mtu kama haamini aje kwangu (Korogwe) alione. Ukijumlisha malipo ya TRA na mambo mengine pamoja na bei ya kununulia gari ni kama shilingi milioni 300 hivi. Itakuwa imefikia milioni 290,” alisema mbunge huyo.

ASEMA LA KUSHANGAZA
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Ngonyani alisema aliamua kununua gari hilo ili kumjibu aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

“Unakumbuka kuna mwaka Amos Makala akiwa naibu waziri aliwahi kusema aliniazima gari nikawa simrudishii, akanichukua kama nililiiba na nikatoka kwenye gazeti? Ile iliniuma sana, sasa na mimi nimemjibu kwa kununua gari hili la kisasa. Ni Toyota Land Cruiser Super Charger,” alisema Maji Marefu.

Leave A Reply