visa

GARI LA PESA LAZUA BALAA

MOROGORO: Gari linalodaiwa kusafirisha pesa kutoka Hazina na kuzisambaza kwenye mabenki mjini Morogoro mwanzoni mwa wiki hii likiwa katika mwendo kasi, linadaiwa kumgonga mwendesha baiskeli eneo la Juwata katikati ya mji na kumsababishia balaa majeruhi baada ya kuumia sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kwenye paji la uso.

 

Baada ya kutokea kwa ajali hiyo mwandishi wetu aliyekuwa mtaani akisaka matukio alishuhudia umati ukiwa eneo la tukio huku majeruhi huyo akigaragara chini kwa maumivu.

 

Mara baada ya ajali, kundi la wananchi walizua balaa kwani walilivamia gari hilo la pesa jambo lililosababisha askari polisi aliyekuwa akilisindikiza kushuka kwenye gari akiwa na silaha ya moto na kuwatawanya watu hao huku akimuamuru dereva kuondoa gari kwa usalama wa  pesa hizo.

 

Baadaye askari huyo aliwapigia simu polisi wenzake wanaofanya doria mtaani kwa pikipiki ambao walifika ‘fasta’ eneo la tukio na kumpakia majeruhi huyo kwenye pikipiki yao na kumkimbia hospitali.

Hata hivyo, askali polisi hao walijikuta katika wakati mgumu kufanya kazi hiyo baada ya kutupiwa maneno makali na wananchi ambapo askari mmoja maarufu kwa jina la Afande Pinto naye aliwajibu kistaarabu wananchi hao huku akimpakia majeruhi huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja.

 

“Namuwahisha majeruhi hospitali, dereva wa gari akishashusha mzigo huo wa pesa atakuja hospitali kulipa gharama za matibabu,” alisema askari huyo. Juhudi za mwandishi wetu za kutaka kuzungumza na majeruhi huyo ziligonga mwamba kwani alipokuwa akiulizwa swali hakuwa anajibu chochote badala yake alikuwa akilalamika kuwa anasikia maumivu kichwani.

 

Wakizungumza na Gazeti la Amani mashuhuda wa tukio hilo walionekana kugawanyika ambapo baadhi walimlaumu polisi aliyekuwa kwenye gari la pesa kwa kutendo chake cha kuamua kuondoa gari hilo bila kujali hali ya majeruhi, huku wengine wakimpongeza wakionesha kuwa amesalimisha fedha.

“Polisi hayuko juu ya sheria; gari hili la mshahara likiwa mwendo kasi limemgonga mwendesha baiskeli aliyekuwa kwenye saiti yake. “Cha ajabu wakati dereva akishuka kwa lengo la kutoa msaada kwa majeruhi askari huyo akamuamuru kuondoa gari na kumtelekeza majeruhi huyo,”alilalamika Joseph Damasi.

 

Naye Msimbe Augostine alikuwa na haya ya kusema: “Mimi nawashangaa wanaomlaumu yule polisi; binafsi naona alichofanya ni sahihi, wote tumeshuhudia walipofungua mlango tumeona gari imejaa pesa huku kundi la watu wakiizingira, wengine walianzisha vurugu wakijifanya wana hasira kumbe lengo lao ni kutaka kuiba zile pesa. Polisi kafanya kazi yake sawasawa.”

 

INSTALL  +255 GlobalRadio ====> rebrand.ly/255GlobalRadioApp
Toa comment