GARI aina ya Nissan lenye namba za usajili, T 949 BLV limetumbukia mtaroni asubuhi ya leo eneo la Bamaga-Mwenge jijini Dar, baada ya kugongana na Bajaj.
Mashuhuda wa tukio hilo waliozungumza na mtandao huu wamesema ajali hiyo ilitokea majira ya saa moja asubuhi, ambapo dereva wa gari hilo alikuwa akitokea mjini kuelekea Bunju ndipo Bajaj iliyokuwa ikitokaa Mwenge kuelekea Bamaga ilikata kona ghafla upande wa kulia kuingia katika uchochoro.
Jitihada za kulinasua gari hilo.
Kitendo hicho kilimfanya dereva wa gari kumkwepa na kupoteza mweleke na gari lake kutumbukia mtaroni baada ya kuikwangua Bajaj hiyo upande wa kushoto.
Dereva wa Bajaj aliyejitambulisha kwa jina moja la Juma, alipata majeraha kidogo usoni na kwenye mkono wa kulia huku dereva wa gari akiwa hana jeraha lolote, licha ya gari lake kuharibika vibaya.
Akizungumza na mwandishi wetu, dereva wa Bajaj alisema alikuwa akitokea Mwenge kumfuata abiria wake maeneo ya Bamaga, lakini alipofika sehemu ya tukio aliamua kukata kona li;oa ili akaingilie upande wa Chuo cha Ustawi wa Jamii ndipo alipoparamiwa na gari hilo.
Dereva wa gari hakutaka kuzungumzia chochote, huku baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo wakidai dereva wa Bajaj alikata kona pasipo kuwa makini.
NA DENIS MTIMA/GPL