KAMPUNI ya Global Group kupitia gazeti namba moja la michezo Tanzania, Championi limetoa zawadi za tiketi kwa wateja wake ili waweze kushuhudia mtanange wa leo kati ya Simba na Yanga.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa leo saa 1:00 usiku Uwanja wa Mkapa unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na utani wa jadi wa timu hizi mbili.
Ni mashabiki wa Simba na Yanga ambao walikutwa na timu ya usambazaji wakisoma gazeti la Championi Jumamosi waliweza kupewa zawadi ya tiketi ya mchezo huo.
Anthon Adam, Mkuu wa Kitengo cha Usambazaji kutoka Global Group amesema kuwa ni kawaida ya kampuni hiyo kurudisha fadhila kwa wasomaji wake kwa kuwapa tiketi hizo ikiwa ni pamoja na zawadi mbalimbali ambazo kampuni hiyo imekuwa ikizitoa.
“Hii imekuwa desturi yetu kurudisha fadhila kwa wasomaji wetu kwani wamekuwa wakituunga mkono, hivyo ni jambo jema kuwarudishia kile tunachokipata kutoka kwao, kwa kuwa sote ni familia ya Championi.
“Wasomaji wetu tuliowakuta wakiwa na nakala ya gazeti la Championi Jumamosi tumewapa tiketi ya kwenye mechi ya Simba dhidi Yanga, hii imekuwa ni kawaida yetu kuwapa tiketi wasomaji wetu wanaokutwa wakiwa na nakala ya gazeti,” amesema.