The House of Favourite Newspapers

Geita: Vilio, Huzuni Vyatawala Mgodi wa Imalanguzu

MAJONZI na huzuni vimetawala kwenye mgodi wa wachimbaji wadogo wa dhahabu mgodi wa Imalanguzu Wilaya ya Geita kata ya Lwamgasa katika Kijiji cha Imalanguzu, mara baada ya kuwasili Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, mgodini hapo akiwa na viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Madini, uongozi wa mkoa na viongozi wa dini kwa ajili ya kwenda kusitisha shughuli za uokoaji wa wachimbaji wadogo wawili, Karos Msukuma Paulo,  mwenyeji wa Chato na Kulwa Joseph Mahungija mwenyeji wa Busolwa Nyangh’wale waliofukiwa kifusi Oktoba 1, 2019.

 

Usitishaji wa zoezi hilo umefanyika Novemba 9, 2019 ikiwa ni siku 39 tangu wachimbaji hao wafukiwe na kifusi kutokana na uwepo wa changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika kipindi chote cha uokoaji. Ripoti maalam ya timu ya wataalam wa uokoaji imeeleza kuwa kumekuwa na changamoto nyingi wakati wote wa uokoaji zilizosababisha kuwa na ugumu wa kuwaokoa wachimbaji hao.

 

Akiwasilisha taarifa ya wataalam wa uokoaji iliyoishauri serikali kusitisha  zoezi hilo la uokoaji kwa Nyongo, Mkuu wa Wilaya ya Geita,  Josephat Maganga,  amemwambia waziri huyo kuwa miongoni mwa changamoto zilizojitokeza wakati wa uokoaji ni pamoja na uwepo wa maji chini ya mgodi, mwingiliano wa magogo mbalimbali chini ya shimo la mgodi, na kutokuwa na usalama katika eneo hilo hata kwa vyombo vya uokoaji.

 

Maganga aliongeza kuwa kulikuwa na wataalam wa makundi mbalimbali ya uokoaji na vifaa vya kutosha kutoka kwa jeshi la uokoaji, mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM), na makampuni mengine kutoka kwenye migodi mbalimbali, lakini pamoja na juhudi zote hizo imeshindikana kupatikana kwao.

 

Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa siku ya tukio hilo, kwenye shimo hilo kulikuwa na wachimbaji watano ambapo watatu kati yao waliokolewa siku hiyohiyo na wawili hawakupatikana hadi zoezi hilo la uokoaji linasitishwa.

 

Kwa upande wake, akiongea kwa masikitiko na majozi kwenye hadhara hiyo, Nyongo amesema kwanza lililotokea ni bahati mbaya na kwamba serikali imesikitishwa na tukio hilo na kwamba iko pamoja wafiwa na wachimbaji wote.

 

Ameongeza kuwa, serikali inathamini sana hata uhai wa mtu mmoja kuliko dhahabu au madini yote yaliko chini na ndiyo maana inasisitiza wachimbaji kuchimba kwa kufuata utaratibu na sheria ili wazingatie usalama na kuepukana na majanga kama hayo.

 

Pia ametoa kauli ya serikali ya kuhitimisha shughuli za uokoaji na kutoa maelekezo kuhusu eneo hilo ambalo wachimbaji hao wamefukiwa na kifusi.

 

“Na sasa tunakwenda kufanya ibada ya kwenda kuwazika wenzetu, viongozi wetu wa dini wako hapa watatuongoza katika ibada hiyo kwa ajili ya maombi. Natamka kuwa shughuli zote za uchimbaji katika eneo ambalo tunaamini kuwa ndipo wezentu hawa wapo,  litambuliwe rasmi kuwa ndiyo kaburi lao na kama kuna undelezaji wa shughuli ya uchimbaji utaendelea katika eneo lingine na kwa utaratibu mwingine,” alisema.

 

Alitoa maagizo kwa Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Geita na timu yake kusimamia usitishwaji wa shughuli za uchimbaji katika eneo hilo mpaka pale hatua za uzingatiaji usalama ziwe zimefuatwa ili kuepusha ajali nyingine.

 

Kwa upannde wake,  Mchungaji Nuhu Suleman aliyeongoza ibada hiyo ya kuwaombea marehemu alisema, hapana budi kumshukuru Mungu kwa kila jambo na kila jambo hukusudiwa na Mungu. Amewakumbusha waumini wote kumuelekea Mungu kwani yeye ndiye mwenye upekee wa ufalme na kwamba maisha ya binadamu yana ukomo hivyo ni vyema kila mmoja akajiandaa na safari hiyo.

Comments are closed.