The House of Favourite Newspapers

Ghafla tu, Corona Imegeuka Bonge la Dili!

0

MGENI kwetu ameingiaa…

Mgeni…mgeniii… mgeni…

Mgeni huyu Ukimwiii..!

“Mgeni chumbani ameingiaaa…

Chumbani kwa baba na mamaaa…

Mgeni…

mgeniii, mgeni huyu balaa…!”

Hii ni sehemu ya mashairi yenye ujumbe mzito kutoka kwenye Wimbo wa Mgeni Kaingia wa marehemu Kepteni John Komba (RIP) akitahadharisha juu ya janga la Ukimwi ulipoingia nchini kwetu miaka mingi iliyopita na kusababisha vifo vingi vya ndugu zetu, jamaa na marafiki zetu.

 

“Mtaani kwetu ameingia nyambizi, tujihadhari tutauawaaa… nyambiizi waa…waaa… nyambizi asimnase mtu…” Hiki ni kiitikio cha Wimbo wa mwanamuziki wa dansi Bongo, Mwinjuma Muumini, naye alikuwa akitahadharisha juu ya janga hilo la Ukimwi.

 

Huu ni utamaduni wa miaka mingi ambapo wanamuziki hutumia nafasi zao kutunga ngoma za kutahadharisha juu ya janga fulani kwenye jamii kama vita dhidi ya ugonjwa fulani, njaa, umuhimu wa amani na mengine mengi.

 

NI ZAMU YA CORONA

Hiki ndicho kinachotokea kila kona kwa sasa kwenye sayari hii ya Dunia. Kuanzia barani Asia, Ulaya, Amerika, Australia na sasa Afrika, inasikika midundo na melodi nyingi zinazosindikizwa na sauti za hisia kali za mastaa wa muziki duniani wakitahadharisha juu ya kusambaa kwa Virusi vya Mafua ya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.

 

Ripoti za Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi wikiendi iliyopita, zilionesha kuwa zaidi ya watu 9,000 wamefariki dunia na zaidi ya 220,000 wameambukizwa Virusi vya Corona duniani kote.

Hili si jambo la mzaha hata kidogo kama wanavyofanya komediani wa Kibongo, Idris Sultan na Steve Nyerere!

Ni janga kubwa na wapo wanaoamini kwamba, Sayari ya Dunia siyo mahali salama tena pa kuishi!

 

Katikati ya janga hili, ghafla tu ngoma za kuhamasisha watu kuchukua tahadhari juu ya Virusi vya Corona, zimekua biashara kubwa kwenye mitandao inayouza muziki.

Ngoma za Corona sasa, zimeteka soko la muziki duniani kwani ndizo zinazosikilizwa zaidi. Kama ikitokea msanii akaachia ngoma ya cherekochereko, mapenzi au kuruka klabu, atashangaza ulimwengu.

Kibongobongo, zimesikika ngoma kadhaa. Mbali na kibwagizo cha King Kiba na Abdu Kiba cha Tanzaniaaa… Corona…coronaaa… coronaaaa…zipo ngoma mbili-tatu za Corona ambazo zinatrendi kwa sasa.

 

RAYVANNY – MAGUFULI-CORONA

Miongoni mwa wanamuziki waliotoa ngoma iliyokamilika ya Bongo Fleva inayokimbiza kwenye mitandao ya kijamii, ni Rayvanny, inayokwenda kwa jina la Magufuli-Corona.

Ngoma hii inahamasisha Watanzania kumuomba Mwenyezi Mungu atuepushe na janga hili kwani wengi wetu ni watu wa hali ya chini.

Ndani ya siku mbili, ngoma hii imetazamwa zaidi ya mara milioni 1.2 kwenye Mtandao wa YouTube.

 

BEKA FLAVOUR – CORONA

Beka ambaye ni zao la iliyokuwa Yamoto Band, ameungana na mastaa wengine duniani kuelezea ni jinsi gani Virusi vya Corona vinaua nchi mbalimbali duniani.

Pamoja na kwamba hajaachia video, lakini hata audio inakimbiza kwenye mitandao ya kijamii na kumfanya kusikika kuliko wengine.

 

MACKAY FANTA – CORONA

Kutoka kwenye muziki wa dansi Bongo, imesikika sauti ya mwanamuziki wa kitambo, Mackay Fanta akieleza namna ambavyo Watanzania wanapaswa kujihadhari na janga hili.

Nje ya Bongo, huko ndiyo usiseme kwani ngoma kadhaa za mastaa wakubwa zinasikika;

 

CARD B – CORONAVIRUS

Ngoma ya Coronavirus ya staa huyu mkubwa wa muziki wa Marekani, inaongoza kusikilizwa na kununuliwa na mamilioni kwenye mitandao ya kijamii.

Ngoma hii inatoa tahadhari juu ya namna ya kujikinga na Virusi vya Corona na namna ambavyo ni janga kubwa duniani.

Ngoma hii imeungwa mkono na mastaa wenzake wakubwa wa muziki duniani kama Ariana Grande, Tylor Swift, Lady Gaga, Katy Perry na wengine wengi.

 

THE NDLOVU YOUTH CHOIR – CORONAVIRUS

Kutoka nchini Afrika Kusini, kwaya hii inakimbiza kwenye mitandao ya kijamii na Ngoma yao ya Coronavirus.

Pamoja na kutoa tahadhari juu ya kujilinda na virusi hivi, lakini jamaa hawa wanajizolea watazamaji na wanunuaji wa ngoma yao kwenye mitandao ya kijamii ikishereheshwa na namna ya uchezaji wao unao-saundi kiasili.

 

SKHUMBUZO MBATHA – CORONAVIRUS

Tukisalia hapo Afrika Kusini, unakutana na kwaya hii nyingine ambayo video yao imesambaa kwenye mitandao ya kijamii wakicheza na kuimba kwa hisia juu ya janga hili. Video yao imejizolea views (watazamaji) wengi kwenye mitandao ya kijamii na sasa watu wana-download.

 

PERCY AKUETTEH – CORONAVIRUS

Kutoka Ghana, inasikika michano matata ya rapa huyu ambaye amejizolea umaarufu na ngoma yake hiyo akielezea dalili za mtu aliyepata Virusi vya Corona na jinsi ya kujikinga. Ngoma hii imemfanya kuwa juu kuliko wengine.

 

ASA – CORONAVIRUS

Kutoka Nigeria, inasikika ile midundo na melodi zao za Kinigeria kutoka kwa mwanamuziki Asa akieleza umuhimu wa kunawa mikono kila unaposhika kitu ili kujikinga na virusi hivi.

Hata hivyo, mbali na kuhamasisha, lakini muziki huo unatazamwa na kuuza zaidi kwenye mitandao ya kijamii nchini humo na umemfanya kuwa juu kwa kipindi hiki kuliko hata mastaa wakubwa wa muziki nchini humo.

 

Kutokana na taharuki ilivyo kubwa duniani kote ambapo Virusi vya Corona vimesambaa takriban nchi 125, wasanii hawa wamefanya kazi kubwa ya kuhamasisha kupitia muziki na dansi, lengo likiwa ni watu kuchukua tahadhari.

Pamoja na tahadhari, lakini nyimbo hizi zimegeuka kuwa faraja na biashara kubwa duniani.

MAKALA: OVER ZE WEEKEND

Leave A Reply