The House of Favourite Newspapers

GIGY KATOKA KIGUMU, ANAWAINGIZA CHAKA WENGINE !

Gift Stanford ‘Gigy Money’

KIPINDI kile mwanadada Gift Stanford ‘Gigy Money’ anaanza kujulikana, hakuna aliyejua kwamba alikuwa na lengo la kuja kuwa mwanamuziki. Wengi waliamini kuwa aliyokuwa akiyafanya yalilenga kujipatia umaarufu tu. 

 

Kwa wanaokumbuka vizuri wanajua kuwa wakati jina lake linaanza kutamba, sifa yake kubwa ilikuwa kupiga picha za nusu utupu. Hakuna alichobakiza kukionesha kwenye mwili wake ila hakufikia hatua ya kuvua ‘kufuli’ lake kabisa.

 

Kwa kifupi alikuwa mcharuko. Alikuwa msichana ambaye hakujali kufanya lolote ilimradi tu azungumziwe na kuandikwa. Na kweli alivuma sana kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari.

 

Ukitembelea ukurasa wake wa Instagram utakuta picha chafu na watu kibao wame-like, wengine wamekomenti kumtukana, lakini wala hakujali. Ni kama aliamini kuwa kwa kuzungumziwa vibaya au vizuri ndivyo angeweza kujulikana zaidi.

 

Ndivyo ilivyokuwa! Mara tukasikia amekuwa mtangazaji kwenye vituo mbalimbali vya TV na redio, lakini huko hakudumu maana kwa tabia zake ingekuwa vigumu kuvumiliwa, akapigwa chini. Hapo ndipo alipoamua kuingia kwenye muziki, tukajua anarusha ndoano aone kama anaweza kuvua mafanikio kupitia kazi hiyo.

 

Kwenye muziki kilicho mbeba sana ni ile figa yake na jinsi alivyokuwa akiitumia kuwadatisha mashabiki. Ikawa akipanda stejini hata kama kuimba hajui kivile, watu walikuwa wakiamsha shangwe za kufa mtu.

Nadhani shangwe zile ndizo zilizompa stimu ya kuona akomae na muziki kigumugumu. Akawa anakula mashavu ya shoo. Gigy akawa mtamu kuliko watu walivyofikiria. Lakini sasa, alikopita Gigy hakuna tofauti na wasanii wengine wa kike.

 

Hata ukiangalia historia ya wasanii kama Shilole, Lulu Diva, Amber Lulu, nao waliibukia kwenye muziki baada ya kufanya vibweka na vimbwanga vya kila aina.

Skendo za ngono, kuanika misambwanda yao bila aibu ndiko kulikowafanya wajulikane. Baadaye wakaona watumie umaarufu wao kwenye kufanya muziki.

 

Leo hii ndiyo hao unawasikia wanakula shoo, wanalamba mkwanja na maisha yao yanaendelea. Yawezekana kabisa wana dili nyingine wanazofanya, lakini muziki ndiyo unawa weka mjini.

 

GIGY NA WENZAKE WANATUPA FUNDISHO GANI?

Ninachokiona hapa ni kwamba, mastaa hawa wanataka kuwaaminisha wasichana wengine kwamba wakitaka kuwa maarufu, wawe micharuko, wasiogope skendo. Na hicho ndicho kinachoonekana kwa sasa kwa baadhi ya wasanii wa kike wanaochipukia.

 

Kuna mdada mmoja ambaye anajiita Queen Latty ambaye kiukweli amejaliwa kuwa na shepu matata. Alipokuwa akifanyiwa interview na moja ya TV za mtandaoni alisema kuwa, ndoto zake ni kuwa mwanamuziki mkubwa. Akasema msanii aliyemshawishi kuingia kwenye kuimba ni Gigy, kwamba anavutiwa naye kwa kila kitu na siku moja anataka kuwa kama yeye.

 

Alivyokuwa amevaa huyo Queen Latty ni kimtego kuliko maelezo. Kimsingi sehemu kubwa ya mwili wake ilikuwa wazi na wala hakuonesha hata chembe ya aibu. Nikashawishika kumtafuta kwenye Instagram. Huko nilichokutana nacho ni balaa. Mrembo huyo alikuwa ameposti picha mbaya kuliko hata zile ambazo alikuwa akiposti Gigy.

 

Hapo ndipo nilipoielewa ile sentesi yake kwamba anataka kuwa msanii mkubwa kama Gigy na kwamba na yeye anataka kupita kulekule alikopita staa huyo. Ukijiuliza ni kwa nini anapiga picha hizo chafu huku akiwa na ndoto za kuwa msanii, utapata jibu kuwa amekuwa na ile imani kwamba ili awe msanii ni lazima awe mcharuko, asione aibu kufanya yale ambayo yatawafanya watu wengine wapigwe butwaa.

Hili ni janga na ni vyema wale mabinti wanaotamani kuwa wasanii wakajua kwamba, ili uwe staa, siyo lazima ufanye mambo ambayo ni kinyume na maadili. Wajue kwamba enzi zile wakati kina Shishi, Gigy na wengineo wanapiga picha chafu kisha kuzisambaza ile wawe maarufu, Serikali haikuwa macho kivile, lakini jaribu sasa hivi uone.

 

Ukitaka kutafuta ustaa kwa njia ambazo wamepitia mastaa kama vile kina Amber Lulu, Amber Ruthy, Gigy na wengine, mwisho wake unaweza kujikuta uko gerezani ukitokwa na machozi na asitokee wa kukuonea huruma.

 

Ni kweli kina Shishi, Gigy na wasanii wengine waliotoka kiskendoskedo sasa hivi wanapiga pesa, lakini hao wasikuingize choo cha kike, pambana kwa njia nyingine utoke na amini unaweza kushaini bila kutegemea skendo ambazo baadaye zinaweza kuwa na madhara makubwa kwako.

Comments are closed.