The House of Favourite Newspapers

Giza Nene Harmonize Atakiwa Kufanya Kafara Kiapo cha Diamond

0

DAR: Kwa wale ambao walikwishasahau, habari iwafikie kwamba, staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ au ‘Harmo’ alikula kiapo cha kuchora ‘tattoo’ ya Nasibu Abdul ‘Diamond’ kwamba ataishi nayo muda wote wa maisha yake, sasa giza limetanda baada kuvunja kiapo hicho, Gazeti la IJUMAA linakupa mchapo kamili.

 

Iko hivi, Januari 5, 2016, saa tano asubuhi, Harmo alisema kwamba hajawahi kuwaza kuwa siku moja ataheshimika kama alivyokuwa na akachora tattoo (mchoro mwilini) akiapa kuwa hawezi kumsahahu Diamond au Mondi katika maisha yake na tattoo hiyo ataishi nayo hadi atakapoingia kaburini.

 

TAARIFA ZA HIVI KARIBUNI

Hata hivyo; taarifa za hivi karibuni zinaeleza kuwa, Harmo ameamua kuifuta tattoo hiyo ya Mondi aliyoichora na kuzua gumzo ambapo baadhi ya watu wanasema kuvunja kiapo ni kitu kibaya katika maisha.

 

“Aliapa kwa kuandika na maandishi yapo kwamba picha ya Mondi aliyojichora ataishi nayo hadi anakwenda kaburini, leo kafanikiwa, ameifuta, ile ni kujitafutia balaa,” kilieleza chanzo makini na kuongeza;

“Sasa sijui itakuwaje maana ninavyomuona Harmo ni kama amepotezea tu hivi na kuendelea na maisha yake. Sijui nini kitamtokea.”

TUMSIKILIZE MTAALAM

Gazeti la IJUMAA lilimtafuta mtaalam wa unajimu (astrologer), Maalim Hassan Yahya Hussein na kumuuliza kama kuna ubaya wowote wa kuvunja kiapo kama hicho, naye akafafanua;

 

“Kuna aina tatu za viapo. Kiapo cha kwanza ni cha ahadi au miadi (contractual oath); hiki ni kiapo kinachohusu wakati ujao. Kisipotimizwa, lazima ifanyike kafara.

 

KIAPO CHA PILI

“Kiapo cha pili ni cha fungasho (enveloping oath); hiki ni kiapo kinachohusu wakati uliopita ambapo mtu anayeapa hujua kuwa anaongopa. Hii ni moja ya dhambi kubwa kabisa.

 

“Kinaitwa kiapo cha fungasho kwa sababu mtu anayekula kiapo hiki hufunganishwa na dhambi katika dunia hii na hufunganishwa na moto wa Jehanam katika maisha ya akhera. Hakuna kafara ya kiapo hiki. Mtu akitenda dhambi hii, hutakiwa kutubu mara moja.

 

KIAPO CHA TATU

“Cha tatu ni kiapo chepesi. Hiki kina aina mbili. Ya kwanza ni ile ya mtu kufikiri kuwa jambo fulani ni kweli na huapa hivyo, lakini baadaye akaja kugundua kuwa kumbe ni uongo. Hakuna dhambi katika kiapo hiki na hakuna fidia au kafara inayohitajika kuifuta. Vya pili ni viapo vinavyokuja kwenye ndimi za watu katika mazungumzo ya kawaida au maandishi.”

 

Maalim Hassan alisema ni wajibu kutimiza kiapo cha ndimi au maandishi kama alivyoapa Harmo na ni haramu kukitupa kiapo hicho.

AJIKITA KWA HARMO

Akizungumzia kiapo hicho cha Harmo, Maalim Hassan alisema kwa kuwa amevunja kiapo, lazima atimize masharti yafuatayo; Mosi; afanye kafara ya kulisha chakula maskini zaidi ya 10 au awanunulie nguo.

Aliongeza kwamba Harmo pia atatakiwa kufunga siku tatu mfululizo; hapo ndipo hatapata matatizo yoyote katika maisha yake, vinginevyo balaa zitamuandama siku zijazo.

 

AZIDI KUFAFANUA

Akifafanua zaidi, Maalim Hassan alisema kabla ya mtu kula kiapo, kuna masharti ambayo ni lazima yatimizwe, nayo ni mosi; mtu anayekula kiapo lazima avuke umri wa utu uzima, awe na akili timamu na lazima aape kwa kumtaja Mwenyezi Mungu, awe amekula kiapo bila kushurutishwa, jambo ambalo anasema Harmo itakuwa alitimiza hayo kabla ya kuandika waraka wake huo wa kiapo.

 

Hata hivyo, Maalim Hassan alisema ni wajibu kwa mtu kuvunja kiapo kama aliapa kufanya jambo la haramu, kama vile mtu anayeapa kutosema na nduguye, kuua mtu, kumfitinia jambo mtu na kadhalika na akasema viapo vya aina hiyo havina kafara kwani ni haramu kwa Mungu.

 

MADHARA KUVUNJA KIAPO NI NINI?

Gazeti la IJUMAA lilipomuuliza adhabu au kitu ambacho kitampata mtu aliyekula kiapo akavunja bila kufuata masharti hayo alisema atakuwa amemchukiza Mungu na adhabu ataitoa yeye aliyemchukiza.

 

“Kuvunja kiapo ni haramu. Ni hatari kuvunja kiapo cha heri kwa sababu utaonekana umemdhihaki Mungu ambaye hadhihakiwi, Harmo nasoma hapa amemtaja Mungu, hii ni hatari sana kwake,” alisema Maalim Hassan.

Gazeti hili lilimtafuta Harmo ili kuweza kumsikia kama ameshafanya kafara au la, simu yake iliita bila kupokelewa.

 

TUJIKUMBUSHE

Januari 5, 2016 saa 5:00 asubuhi, Harmo aliandika hivi katika ukurasa wake wa Instagram;

“Katika maisha yangu sikuwahi kuwaza kuwa itatokea siku nikajichora tattoo but Diamond ni mtu mwenye mchango mkubwa sana katika maisha yangu.

 

“Leo hii mimi ninathaminika kutoka kwenye kunyanyasika, ninaheshimika; kutoka kwenye kudharaulika, nimekuwa maarufu na kupata uthamani mkubwa kupitia yeye (Diamond) siyo tu kwa kipaji nilicho nacho kwani wangapi wana vipaji…?

 

“Naisaidia familia yangu kwa kile nikipatacho si haba akiwa na mchango wake mkubwa sana……Lakini mwisho wa siku haya ni maisha na hii ni dunia ina mambo mengi sana hasa sisi vijana ambao ni wepesi wa kujisahau.

 

“Inaweza kutokea kitu kidogo sana ukasahau wema na fadhila ulizotendewa, lakini pia Mungu ndiye katukutanisha na karibu watu wengi wanajua tumekutanaje (na Diamond) kwa kuwa nimekuwa nikiulizwa katika vyombo vya habari tofautitofauti so watu wengi wanajua tulivyokutana but hakuna anayejua tutaachana vipi.

 

“Kwa maana sisi ni binadamu kuna kifo leo na kesho, huwezi kujua ya wanadamu, ni mengi siamini kuwa binadamu wote duniani wanafurahia mahusiano na ukaribu wetu (na Diamond).

 

“Huwezi kushindana na binadamu, ukijua ya mbele, wenzio wanajua ya nyuma, ndiyo maana ya kujichora hii picha yake (Diamond) ambayo haitafutika hadi naingia kaburini.

 

“Hata ikitokea hatupo pamoja (na Diamond), nikiitazama hii picha itabaki kama kumbukumbu na heshima yangu kwake hadi siku yangu ya mwisho. Haya ni maamuzi yangu binafsi…”

Leave A Reply