GLOBAL HABARI FEBR 12: Tamko la Mkuu wa Majeshi Kuhusu Mauaji Njombe – VIDEO

Mkuu wa Majeshi Nchini CDF Venance Mabeyo amewataka watanzania kuwa watulivu katika kipindi hiki ambapo Vyombo vya usalama vinafanya uchunguzi juu ya wale waliohusika katika sakata la kuwateka watoto na kuwaua kinyama mkoani Njombe.

CDF Mabeyo ameyasema hayo baada ya kufika mkoani Njombe kutembelea mahala palipotokea tukio hilo na kuwapa pole wale wote waliofiwa na watoto wao huku akiwa ameambatana na baadhi ya maafisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania JWTZ Kutoka makao makuu ya Jeshi hilo.

Aidha CDF Mabeyo amesema akiwa kama mwenyekiti wa vyombo vya ulinzi na usalama atahakikisha vyombo vyote vya usalama vinashirikiana kuwabaini wote waliohusika kutekeleza tukio hilo pamoja na mbinu walizozitumia ambazo yeye anadai ni za kawaida hazihitaji Jeshi la wananchi (JWTZ) kuingilia kati.

Tukio hili la kutekwa kwa watoto na kuuawa kinyama kwa kunyofolewa viungo vyao vya mwili lilizua simanzi kubwa kwa watanzania na kuzua sintofahamu Bungeni hali iliyopelekea Spika wa Bunge Job Ndugai kuitaka serikali kutoa tamko juu ya hatima ya matukio hayo yaliyohusishwa na imani za kishirikina.

Toa comment