The House of Favourite Newspapers

GLOBAL HABARI FEBR 19: Waziri Mkuu ‘ATUMBUA’ Hadharani Leo – VIDEO

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Kibondo, Thomas Chogolo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili za ubadhilifu wa makusanyo ya mapato ya halmashauri hiyo.

Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo leo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma na kuwataka watendaji wa halmashauri hiyo kumaliza haraka migogoro yao ya kiutendaji inayowakabili.

Mbali na fedha za makusanyo ya kodi Waziri mkuu Amesema matumizi ya fedha mbalimbali zinazopelekwa na Serikali katika halmashauri hiyo airidhishi.

Waziri Mkuu amesema uaminifu na uadilifu ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na watumishi wa umma, hivyo amewataka watumishi hao wasijiingize kwenye mambo ambayo hayana tija katika utumishi wao.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amelifunga soko la wakimbizi na wananchi lililoanzishwa nje ya kambi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma ambapo Hatua hiyo imekuja baada ya soko hilo kubainika kuwa chanzo cha wakimbizi kutoka nje ya kambi kiholela na kushiriki katika kufanya matukio ya kiharifu.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anaendelea na ziara yake mkoani kigoma kwa siku nne yenye lengo la kukagua miradi inayofanywa na Serikali huku akihamasisha kilimo cha zao la Mchikichi mkoani humo.

Comments are closed.