visa

Global Publishers Yaanzisha Shindano Kusaka Vipaji Vya Wazungumzaji Bora Kitaifa

Meneja wa Global Publishers, Abdallah Mrisho (wa kwanza kushoto),  na waratibu wa shindano la ‘National Public Speaking Competition’ wakizungumza na vijana waliojitokeza kushiriki shindano hilo linalofanyika katika ofisi za kampuni hiyo.

KAMPUNI inayoongoza kwa uchapishaji magazeti nchini, Global Publishers imezindua rasmi shindano maalum la kusaka vipaji vya vijana wazungumzaji bora mbele ya hadhara kitaifa lenye lengo la kuwajengea uwezo wa kuzungumza kwa ufasaha mbele za hadhara bila kuogopa.

 

Shindano hilo lililopewa jina la ‘National Public Speaking Competition’ limezinduliwa rasmi Februari 10, mwaka huu baada ya washiriki kujaza na kurejesha fomu za ushiriki walizopatiwa kwa kupitia mawakala wa kampuni hiyo na wadau mbalimbali nchini.

Baadhi ya washiriki wa shindano hilo. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mmoja wa waratibu wa shindano hilo, Pacific Ibrahim alisema mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu ambao ulianza Novemba mwaka jana, ulidumu kwa muda wa miezi mitatu kabla ya shindano hilo kuanza rasmi wiki hii.

 

Alisema kwa muda mrefu, kampuni ya Global Publishers imetoa nafasi kwa watu wa kada mbalimbali kutoa mawazo yao na kuonyesha vipaji vyao kwa kupitia magazeti saba inayoyachapisha.

 

“Lakini sasa tumeona kuna umuhimu wa kutoa nafasi ya kuwanoa vijana kuonyesha vipaji vyao vya kuzungumza mbele ya hadhara kwa kujiamini na kwa ufasaha ili waweze kunufaika zaidi kwa kupitia vipaji hivyo,” alisema.

Mratibu wa shindano hilo, Pacific Ibrahim, akizungumza na baadhi ya washiriki ambao ni vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini waliofiki ofisi za Global Publishers.

Alisema baada ya mchakato wa kugawa na kurejesha fomu zaidi ya 400 za ushiriki wa shindano hilo kukamilika, zaidi ya vijana 300 wamerejesha fomu hizo na kujitokeza kushiriki katika awamu hiyo ya kwanza.

 

“Vijana hao tunawafanyia usaili kwa muda wa siku tano kuanzia Februari 10 hadi 15, mwaka huu, kwa kupitia majaji wetu ambao tumewateua kwa kuzingatia weledi, ufanisi na uwezo wao katika nyanja hiyo,”  alisema.

 

Aidha, alitaja mojawapo ya vigezo ambavyo vinazingatiwa katika zoezi hilo la mchujo awamu ya kwanza ni kuhakikisha mzungumzaji anazungumza kwa ufasaha bila kukwama kutamka maneno, kuiangalia hadhara, kuwa sehemu ya hadhara anapozungumza, kutumia lugha ya mwili kwa usahihi na kuzungumza kwa sauti ya kutosha.

 

“Katika mchujo wa awamu ya pili watabaki vijana 30 ambao watapatiwa mafunzo zaidi na majaji wabobevu na watu wa kada mbalimbali waliofanikiwa katika tasnia hiyo kama vile Eric Shigongo na Chriss Mauki ili kuwajengea uwezo thabiti wa kuwawezesha vijana hao kuvitumia vipaji vyao ipasavyo,” alisema.
Toa comment