The House of Favourite Newspapers

GlobalNews: Uwoya, Kelvina Hapatoshi!

0
Irene Uwoya.

 

SIFA ya ubuyu wenye rangi nyekundu ni kuacha rangi midomoni vivyo hivyo penzi ni kikohozi kulificha huwezi! Wamama wawili wa Bongo Muvi, Irene Uwoya na Kelvina John, wanadaiwa kuingia kwenye vita nzito ya penzi la msanii wa Bongo Fleva, Patrick Chrisopher ‘PCK’ na sasa hapatoshi, ni Ijumaa Wikienda pekee lenye ubavu wa kukupa ubuyu ulionyooka.

MAPENZI SHATASHATA

Chanzo makini cha ubuyu huo kililieleza Ijumaa Wikienda kuwa, kwa sasa PCK na Kelvina ni mahaba niue au mapenzi shatashata, jambo ambalo linamchukiza Uwoya ambaye anasemekana kwamba, aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume huyo anayesifika kwa kuwachanganya na kuwapanga kama mafungu ya nyanya mastaa wa kike Bongo.

“Hivi watu wa ubuyu mnajua kuwa kuna vita nzito kati ya Uwoya na Kelvina? Unaambiwa sasa hivi vita yao siyo ya nchi hii na wanaviziana kama Korea Kaskazini na Marekani, eti, kisa nasikia wanagombea penzi la PCK.

WAKUTANA BAA YA UWOYA

“Tukio bichi la Uwoya na Kelvina ni la juzikati ambapo walikutana kwenye sherehe ya ufunguzi wa baa ya Uwoya maeneo ya Mori (Sinza, Dar), lakini hawakusemeshana vizuri wakati awali walikuwa marafiki wakubwa.

“Uwoya amekuwa akimtukana sana Kelvina kupitia meseji anazomtumia PCK huku akimuita mzee na kumtaka mwanaume huyo aachane naye kwani anamuhitaji waendelee kuwa pamoja lakini mwanaume huyo amekuwa akikataa jambo linaloendelea kumpa hasira zaidi Uwoya,” kilidai chanzo hicho kwa sharti la kutochorwa jina gazetini.

Kelvina John.

 

WIKIENDA HALIACHI KITU

Baada ya kupata ubuyu huo, kama kawaida yake, Ijumaa Wikienda huwa haliachi kitu hivyo lilimtafuta Kelvina ambaye alikiri kuona meseji ambazo Uwoya amekuwa akimtumia PCK akimwambia kuwa yeye (Kelvina) ni mzee.

“Niliona hizo meseji kwenye simu ya PCK, lakini sina tatizo na Uwoya labda kwa upande wake mimi sijui.

“Yeah! Ni kweli nilikutana naye (Uwoya) na nakumbuka tulisalimiana kama kawaida.

“Huyo mwanaume ni rafiki yangu tu, sasa sijui hizo SMS zinatoka wapi! Ingawa nikiangalia naona namba ya Uwoya ndiyo imetuma hivyo nashindwa kumuuliza kwa sababu naona tupo sawa tu, sina la kusema zaidi,” alisema Kelvina.

PCK AKIRI KUTUMIWA SMS

Kwa upande wa PCK ambaye ndiye chanzo cha vita hiyo ya penzi, alipoulizwa kuhusu hilo alikiri kuwa, ni kweli Uwoya amekuwa akimtumia SMS za kumkashifu mpenzi wake wa sasa, Kelvina huku akitaka waachane.

Patrick Chrisopher ‘PCK’

 

Ijumaa Wikienda lilitaka kujiridhisha ambapo lilimuomba jamaa huyo kutuma ‘chating’ zake na Uwoya ambazo zilionesha akimwambia mwanaume huyo kuwa amekosa wanawake wa kuwa nao mpaka kwenda kuwa na Kelvina ambaye ni mzee.

Pia SMS hizo zilikuwa zikimtisha jamaa huyo kuwa, mtumaji ambaye namba ilisomeka ni ya Uwoya alimwambia atafanya juu chini ili amharibie na atahakikisha ameachana na Kelvina.

“Kelvina ni mpenzi wangu na nimeamua kuachana na Kibonge Sexy (video queen wa Bongo) kwa ajili yake maana ni mwanamke anayenipenda na kunikubali kwa kipindi hiki ambacho niko kwenye matatizo binafsi.

“Hivi karibuni tu nitapeleka posa nyumbani kwao. Huyo Uwoya aendelee tu kutukana wala hatuna habari naye,” alisema PCK.

UWOYA SASA

Alipotafutwa Uwoya, simu yake iliita mfululizo bila kupokelewa, lakini amewahi kuulizwa kuhusiana na kumfanyia fujo PCK mara anapomuona akiwa na mwanamke ambapo alisema kuwa, jamaa huyo aachane naye kwani akiendelea atampeleka mahakamani na kusisitiza kuwa hamjui.

NENO LA MHARIRI

Ni vyema mastaa hao wakakaa pamoja na kukubaliana kufanya mambo ya maendeleo na kukuza sanaa ya Bongo Muvi inayoelekea kufa kuliko kuendelea na malumbano yasiyo na tija.

Waandishi Wetu |Ubuyu|IJUMAA WIKIENDA | Dar

 

 

INSTALL GLOBAL PUBLISHERS APP sasa usipitwe na matukio
PAKUA HAPA==>GLOBAL PUBLISHERS APP

FULL VIDEO; Mapambano Ngumi za Global TV – Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Tanzania Bingwa

Leave A Reply