The House of Favourite Newspapers

Godbless Lema Aitwa Polisi

MBUNGE wa Arusha Mjini (CHADEMA) na Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Godbless Lema ameitwa na Jeshi la Polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini humo ambapo amedai kuwa wito huo umeonekana ni wa haraka na ni wa lazima.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Lema ameandika; “Nimepigiwa simu na Polisi kwamba natakiwa kuripoti kituo kikuu cha Polisi Arusha leo bila kukosa,sijaelezwa sababu lakini wito unaonekana kuwa wa lazima sana,lakini nafikiri kupigania haki ndio linaweza kuwa kosa langu kubwa. MSIOGOPE,” amesema Lema.

Baada tukio la kutekwa kwa siku 9 mfanyabiashara Mohammed Dewji ambaye alipatikana juzi Jumamosi, awali Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi walitoa taarifa kwa umma na kueleza kwamba wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kuhakikisha MO anapatikana akiwa hai na watekaji wanatiwa mbaroni.

 

Siku chache baadaye, Lema alizungumza na wanahabari na kulitaka jeshi hilo kuita wachunguzi wa Kimataifa kufanya upelelezi wa tukiohilo na matukio mengine ya utekaji nchini. Hata hivyo Serikali ilisema haihitaji wachunguzi wa nje kwa sababu jeshi hilo linao uwezo mkubwa na wataalam wa kufanya uchunguzi na kuwabaini wahusika.

 

Licha ya hivyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro alitoa maelezo kwa umma kuhusu uchunguzi uliyofanywa kwa kufuatilia kamera za CCTV ambazo zilinasa gari lililohusika kumteka MO na kuonyesha picha na namba ya gari hilo, Lema na baadhi ya wanasiasa na wananchi kupitia mitandao ya kijamii walidai gari hilo halijapigwa kwa kamera za CCTV.

 

Baada ya Mo kupatikana kufuatia watekaji kutelekeza eneo la Gymkhana jijini Dar, Sirro alizungumza na wanahabari na kueleza hatua ambayo jeshi hilo lilikuwa limefikia huku akibainisha endapo watekaji wangechelewa kumwachia MO wangetiwa mbaroni.  Pia, Sirro aliwaonya wanasiasa na baadhi ya wananchi wachache wanaobeza kazi inayofanywa na jeshi hilo huku wakijifanya wao wanafahamu kila kitu na kulifundisha jeshi hilo namna ya kufanya uchunguzi wa makosa ya jinai.

Hata hivyo, jana jioni Mbunge huyo aliahidi kutii wito huo huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng’azi akiahidi Kutoa taarifa zaidi leo.

TBC1: IGP atoa ‘ONYO’ kali, Zitto, Lema Linawahusu!

Comments are closed.