The House of Favourite Newspapers

Gomes Aiona Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika

0

KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes raia wa Ufaransa, amefunguka kuwa malengo yao ni kuvuka hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kufika mbali zaidi, hivyo wapo tayari kwa ajili ya kupambana na Kaizer Chiefs.

 

Kauli ya kocha huyo imekuja siku chache baada ya Simba kupangiwa kucheza dhidi ya Kaizer Chiefs katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao wataanzia ugenini.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Gomes alisema: “Kwenye hatua ya robo fainali hakuna timu nyepesi, Kaizer Chiefs ni timu nzuri ambayo wapo vizuri katika kila idara, tunawaheshimu sana, lakini tupo tayari kwa ajili ya kupambana nao.

 

“Itakuwa mechi ngumu kwa sababu timu zote ambazo ziko kwenye mashindano haya ni ngumu, tunawaheshimu sana lakini shabaha yetu ni kufika mbali katika michuano hii na tuko tayari kwa ajili ya kupambana katika mechi hiyo.

 

“Kama tutafuzu kwenda nusu fainali basi tunatarajia kukutana na Wydad Casablanca au MC Algers, wote utagundua kuwa ni timu nzuri, hivyo kwa kuwa malengo yetu msimu huu ni kufika mbali basi tunatakiwa kujiandaa kwa ajili ya timu yoyote.”

 

MO DEWJI ATIA NENO

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’, ametia neno kuhusu ratiba hiyo ambapo alitumia ukurasa wake wa Instagram kusema: “Hongera sana Simba kwa kupata nafasi ya kuchuana na timu ya Kaizer Chiefs kwenye hatua ya robo fainali za Kombe la CAF, nina imani kubwa tutafanya vizuri kwenye mechi hii.

 

KOCHA KAIZER CHIEFS AWACHAMBUA SIMBAA

kizungumza na Spoti Xtra moja kwa moja kutoka Afrika Kusini, Kocha wa Kaizer Chiefs, Gavin Hunt, aliichambua Simba kwa kusema: “Hautokuwa mchezo rahisi kwa sababu Simba ni timu ngumu na imefanya vizuri katika hatua ya makundi mbele ya Al Ahly na AS Vita.“Kitu ambacho tunapaswa kukiangalia ni kwa jinsi gani tutapata matokeo mazuri kwa kuangalia ubora wa wachezaji wao pamoja na kufuatilia mechi zao, tunahitaji kufika fainali safari hii.”

STORI: MARCO MZUMBE, IBRAHIM MUSSA NA SAID ALLY

Leave A Reply