The House of Favourite Newspapers

Gomes Akabidhiwa Emmanuel Okwi

0

HABARI inayotikisa kwa sasa Bongo ni ile inayomuhusu mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi kurejea kwa mara nyingine kukitumikia kikosi hicho kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya kimataifa msimu uajo.

 

Okwi mwenye umri wa miaka 28, hivi sasa anakipiga Al Ittihad Alexandria Club inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri ambapo mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

 

Mshambuliaji huyo raia wa Uganda, wiki hii kupitia akaunti yake ya Mtandao wa Instagram, aliweka picha na ujumbe akionesha kwamba amechaguliwa kuwa nahodha mpya wa Uganda baada ya aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Denis Onyango kustaafu.

 

Baada ya kuweka picha hiyo, mastaa kibao wa Simba waliandika ujumbe unaoashiria kumuhitaji kurejea tena Simba msimu ujao, huku wakimpongeza kwa kuchaguliwa kuwa nahodha.Nahodha wa Simba, John Bocco, aliandika: “Hongera sana kaka, tunakusubiri msimu ujao.”Naye beki wa kati wa Simba, Erasto Nyoni, aliandika: “Hongera sana anko, fanya urudi Tanzania, tumekumisi sana.

 

Bocco na Nyoni wamefanya Wanasimba wengi kubaki na maswali kwamba kama kuna uwezekano wa Okwi kurejea au la, huku wakiamini kwamba kama akirejea, basi anaweza kuwa msaada kimataifa msimu ujao kutokana na yale mengi mazuri aliyoyafanya ndani ya kikosi hicho kabla ya mara ya mwisho kuondoka mwaka 2019.

 

Spoti Xtra lilimtafuta Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, kuzungumzia suala hilo, ambapo alisema: “Kwa sasa klabu yetu imeweka nguvu katika kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo yetu iliyosalia ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

 

“Kuhusu masuala ya usajili na hususani mchezaji Emmanuel Okwi, tunasubiri ripoti ya kocha mkuu, Didier Gomes juu ya mapendekezo yake ambayo tumejipanga kuhakikisha tunayatimiza.

 

Kwa mara ya kwanza, Okwi alijiunga na Simba mwaka 2010 akitokea SC Villa ya Uganda, akacheza hapo hadi 2013, akatimkia Étoile du Sahel ya Tunisia alipocheza kwa muda mfupi, akarudi SC Villa. Mara ya pili aliichezea Simba msimu wa 2014–2015, kabla ya hapo, alikuwa Yanga.

 

Kisha 2015 hadi 2017, akatiumikia SønderjyskE ya Denmark, akarejea SC Villa, kabla ya kutua Simba alipocheza 2017 hadi 2019 ambapo mkataba ulipoisha, akajiunga na Al Ittihad mwaka 2019 kwa mkataba wa miaka miwili unaomalizika mwishoni mwa msimu huu.

WAANDISHI: Joel Thomas, Marco Mzumbe na Hussein Msoleka

Leave A Reply