The House of Favourite Newspapers

Gomes Aleta Mashine Nne za CAF

0

KATIKA kuhakikisha msimu ujao wanafanya vema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes amewaambia mabosi wake kuwa anahitaji wachezaji wanne pekee kutoka nje ya nchi.

 

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo iondolewe na Kaizer Chiefs ya nchini Afrika katika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

 

Simba imeondolewa na Kaizer Chiefs baada ya kufungwa jumla ya mabao 4-3 ambapo ugenini ilifungwa 4-0, kabla ya juzi kurejeana kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na kufanikiwa kupata ushindi wa 3-0.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, Gomes ametoa mapendekezo hayo ya usajili baada ya kukutana na mabosi, akitaka beki wa kati, kiungo mchezeshaji, winga na mshambuliaji.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa usajili wa wachezaji kutoka nje ya nchi kwa lengo la kutengeneza kikosi chenye ubora kitakachofanya vema katika michuano ya kimataifa baada ya msimu huu kutolewa hatua ya robo fainali.

 

Aliongeza kuwa, jukumu hilo la usajili ameachiwa Gomes atakayefanya kazi pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Simba chini ya mwenyekiti, Mohamed Dewji ‘Mo’ katika kufanikisha kukisuka kikosi kitakchokuwa imara na tishio zaidi ya msimu huu.“Msimu ujao tarajia kuiona Simba imara na bora zaidi ya msimu huu ambayo imefika hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa rekodi nzuri ya kutofungwa nyumbani.

 

“Hiyo ni kutokana na mipango ya usajili iliyopangwa na kocha Gomes ambaye tayari amewaambia mabosi wake kuwa anahitaji wachezaji wanne kutoka nje ya nchi wenye uzoefu na uwezo mkubwa wa kucheza michuano ya kimataifa.

 

“Katika kuhakikisha anakifanyia maboresho kikosi chake, Gomes ametoa mapendekezo yake ya usajili akiomba wachezaji wanne wapya wa kigeni watakaocheza nafasi ya beki, kiungo mchezeshaji, winga na mshambuliaji wenye viwango bora,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Gomes hivi karibuni alizungumzia mipango yake ya usajili na kusema kuwa: “Muda wa usajili bado, hivyo ni vema tukasubiria, hivi sasa akili zetu tumezielekeza katika kuutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.”

STORI: WILBERT MOLANDI, Dar

Leave A Reply