The House of Favourite Newspapers

Gomes: Tukiifunga Yanga, Ubingwa ni Asilimia 100

0

 

KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes, ametamba kuwa ni lazima waibuke na ushindi katika mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Yanga, kwani wakifanikiwa kuifunga Yanga basi ubingwa kwa Simba ni asilimia 100.

 

Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana katika mchezo wa dabi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, utakaopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, ambapo Simba watakuwa wenyeji wa mchezo.

 

Timu hizo zitaingia katika mchezo huo zikiwa na kumbukumbu ya matokeo ya sare ya bao 1-1 waliyoipata katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Novemba 7, mwaka jana.

 

Mpaka sasa Simba ndiyo vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Bara ambapo wamejikusanyia pointi 61, wakifuatiwa na Yanga wenye pointi 57, licha ya kwamba wamecheza michezo miwili zaidi ya Simba.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Gomes alisema: “Tumefurahi kwa ushindi ambao tuliupata katika mchezo wetu wa Jumamosi dhidi ya Kagera Sugar katika michuano ya Kombe la FA, kwa sasa tunajua tuna ratiba ya kucheza michezo mikubwa dhidi ya Yanga na michezo ya robo fainali ya mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs.

 

“Lakini mawazo yetu yote tumeyaelekeza kwenye mchezo wetu ujao dhidi ya Yanga, kwa kuwa ni mchezo mgumu wa dabi, nafurahi kuona kuelekea mchezo huo tupo katika hali nzuri ya kujiamini kutokana na kupata ushindi katika michezo yetu sita iliyopita.

 

“Narudia tena tunajua wazi utakuwa mchezo mgumu, lakini tunataka kushinda mchezo huo kwani ni wazi kama tutashinda mchezo huo basi kwa asilimia 100 tutakuwa mabingwa msimu huu.

 

“Kuhusu kiwango bora cha Morrison, nadhani kila mmoja anajua kuwa ni mchezaji mzuri na anatufaidisha kwa vitu vingi uwanjani, kwenye michezo miwili iliyopita ametimiza vizuri majukumu yake ya kuhakikisha anatoa presha kwa wapinzani, siwezi kuhakikisha uwepo wake katika mchezo dhidi ya Yanga lakini tunamhitaji hata tunapokutana na safu ngumu ya ulinzi.”

JOEL THOMAS, Dar es Salaam

Leave A Reply