Kartra

Gomez: Hii Ndiyo Simba ya Msimu Huu

KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomez, amevutiwa na alichokiona mazoezini msimu huu na kutamba; sasa nina machaguo mengi nah ii ndiyo Simba ninayoitaka.

 

Simba ipo mkoani Arusha kwa ajili ya kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imejichimbia eneo la Karatu nje kidogo ya jiji.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu kutokea jijini Arusha ambako Simba imeweka kambi, Gomez alisema amefurahi kuwa msimu huu timu ina wachezaji wengi watakaofanya acheze kwa mifumo tofauti kulingana na mahitaji ya mchezo husika.

 

Alisema msimu uliopita, alikuwa analazimika kutumia staili zinazofanana za kucheza kwa sababu ya aina ya wachezaji aliowakuta walikuwa wanamlazimisha kufanya hivyo, lakini kwa sasa mambo yatakuwa mazuri sana na mashabiki watapata wanachotaka.

 

“Msimu huu tumesajili wachezaji vizuri na nina machaguo ya kutosha. Naweza kutumia mifumo tofauti ya kucheza kwa sababu wachezaji wa kufanya hivyo ninao,” alisema Gomez.

 

Alisema mmoja wa walimu wake waliomfundisha ukocha aliwahi kumwambia kwamba kama una wachezaji bora kwenye timu ni lazima wacheze ili timu iwe nzuri.

 

“Kama una wachezaji bora watano kwenye ngome ya ulinzi, itabidi utafute namna bora ya wote kucheza. Kama una washambuliaji au viungo wengi wazuri tafuta namna ya wote kucheza hii ndiyo maana halisi ya kuwa na kikosi kipana,” alisema Gomes ambaye msimu uliopita aliipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

 

Katika mazungumzo yake hayo ya kwanza na chombo cha habari tangu kuanza kwa msimu huu, Gomez alisema changamoto kubwa aliyonayo sasa ni kutafuta namna ya kutengeneza timu imara kutoka katika machaguo aliyo nayo ili wakiingia uwanjani wawe na uhakika wa kupata matokeo mazuri kwa kuwa anafahamu kuwa ligi msimu ujao itakuwa ni ngumu sana.

 

Amesema kuna vitu ameviona mazoezini na katika baadhi ya mechi za kirafiki katika siku za karibuni ambavyo vimeanza kumpa picha kuhusu nini hasa anaweza kufanya kukifanya kikosi kiwe kizuri zaidi.

 

Alisema kuondoka kwa Luis Miquissone na Clatous Chama ni jambo la kawaida katika soka kwa sababu hata yeye amefundisha timu tofauti barani Afrika na wachezaji au makocha kuhama kutoka timu moja kwenda nyingine ni jambo la kawaida kabisa na wala yeye halimsumbui.

 

“Kuhama kwa makocha au wachezaji ni jambo la kawaida kabisa, hilo wala halinisumbui kwa kuwa nimekaa kwenye timu nyingi sana na naona jinsi ambavyo wachezaji wamekuwa wakiondoka na klabu zinasajili wengine.

 

“Kwangu hili ni jambo la kawaida sana, nafikiri ni wakati wa mashabiki kuamini kuwa tutafanya vizuri zaidi msimu huu,” alisema Gomes mwenye uwezo wa juu wa kufundisha soka la kasi.

 

Alisema jambo la msingi ni kwa timu kujipanga na kujijenga upya kutokana na wachezaji waliopo. Simba wanatarajiwa kurejea Dar wiki hii kwa ajili ya kumalizia maandalizi ya kucheza nchezo wa Simba Day ambao utapigwa Septemba 19 mwaka huu.

 

Simba imefanikiwa kufanya vizuri kwa miaka minne mfululizo ambapo imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo, huku ikifika robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara mbili. Msimu uliopita mbali na ubingwa wa Bara, Gomes pia aliiongoza Simba kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika.

 

ZARITA ALLY, Arusha


Toa comment