Grand P Arudiana na Eudoxie, Waanika Tena Penzi Lao Mitandaoni

Msanii maarufu kutoka Guinea, Moussa Sandiana Kaba maarufu kama Grand P, amerudiana na aliyekuwa mpenzi wake, mwimbaji na mwanamitindo mashuhuri wa Ivory Coast, Eudoxie, baada ya kipindi cha wao kutengana kilichozua gumzo kubwa mitandaoni.
Dalili za kurejea kwa penzi hilo zimeonekana wazi kupitia machapisho mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, ambapo wawili hao wameonekana wakifurahia muda pamoja katika maeneo tofauti, wakionekana wenye furaha na ukaribu mkubwa, hali iliyowafanya mashabiki wao kuamini kuwa wamerejesha rasmi mahusiano yao.

Hapo awali, kupitia ukurasa wake wa Instagram, Eudoxie aliweka wazi sababu za kuachana na Grand P, akieleza kuwa alishindwa kuvumilia tabia ya msanii huyo ya kuhusishwa na wanawake wengine. Alidai hali hiyo ilikuwa ikimnyima amani na raha katika uhusiano wao, jambo lililomfanya achukue uamuzi wa kuachana naye licha ya madai kwamba Grand P ana uwezo mkubwa kifedha.
Kurudiana kwao kumezua hisia mseto miongoni mwa mashabiki wapo wanaowapongeza kwa kutoa nafasi ya pili kwa mapenzi yao, huku wengine wakisubiri kuona kama safari hii uhusiano huo utadumu kwa muda mrefu. Hata hivyo, kwa sasa, Grand P na Eudoxie wameamua kuonyesha wazi furaha yao na kuacha picha zao zizungumza zaidi.


