The House of Favourite Newspapers

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 22

0

ILIPOISHIA:

Nilijifungua ile sanda, na mimi nikabaki kama Rahma, nikasogea pale kwenye bomba, maji yakawa yanatumwagikia, chini damu zikawa zinaendelea kutiririka kuelekea kwenye bomba la kutolea maji machafu. Nilimshika mikono Rahma, nikamvutia kwenye kifua changu, tukawa tunatazamana huku maji yakiendelea kutumwagikia, nikajikuta nikitamani kumbusu mdomoni.

SASA ENDELEA…

“Mbona najisikia hivi?”

“Unajisikiaje?”

“Hata sijui nisemeje lakini najisikia raha ya ajabu ndani ya moyo wangu,” alisema Rahma na kabla hata sijafanya kile nilichokuwa nakitamani, yeye alinianza akanibusu kwa midomo yake milaini huku akinikumbatia kwa nguvu, na mimi nikamuonesha ushirikiano.

“Kwa nini ulitaka kujiua?” nilimuuliza, akafumbua macho yake ambayo kwa muda wote alikuwa ameyafumba, akanitazama usoni bila kusema chochote, akajiinamia. Niligundua kwamba hakulipenda swali hilo, nikaamua kubadilisha mada lakini bado hakuzungumza chochote.

Nilimsaidia kumsafisha mwili wake wote mpaka damu zote zikaisha kwenye miili yetu, nikafunga maji na kumpa khanga yake lakini aliikataa kwa sababu nayo ilikuwa na damu.

“Vaa tu kwanza tutaoga tena kwa mara nyingine, inabidi tukafanye usafi chumbani kwako,” nilimwambia, akakubali. Tulichukua ndoo za maji na vifaa vya kufanyia usafi, tukaelekea chumbani kwake ambako kila sehemu ilikuwa imechafuka kwa damu.

*Usiache kutembelea Simulizi za Majonzi

Tukaanza kufanya usafi lakini bado Rahma hakuzungumza chochote, muda wote alikuwa kimya kabisa na pale alipohitaji kunielekeza jambo, alikuwa akitumia zaidi ishara.

“Mbona umebadilika ghafla? Nisamehe kama kuna kitu nimekukwaza,” nilimwambia, akanitazama tena.

“Kwani nini kilitokea?”

“Wewe unakumbuka nini?”

“Nakumbuka niliamua kunywa sumu ili nife.”

“Kwa nini?”

“Kwa sababu nakupenda.”

“Sasa ukimpenda mtu ndiyo ujiue?”

“Kwa sababu walituambia kwamba sisi ni ndugu,” alisema Rahma huku akiacha kila alichokuwa anakifanya, machozi yakaanza kumtoka.

“Kumbe walisema vile kututishia kwamba tusije tukaanza kufanya mapenzi lakini siyo kweli, hatuna undugu ila baba yangu na baba yako ni marafiki tangu wakiwa vijana wadogo kwa hiyo ni kama ndugu tu,” nilimwambia.

Hata mimi maneno hayo niliwasikia mama na mama yake Rahma wakiongea kule hospitalini, wakilaumiana kwa maneno waliyotuambia ambayo ndiyo yaliyosababisha Rahma achukue uamuzi wa kuyakatiza maisha yake.

Nilipomueleza maneno hayo, alinitolea macho akiwa ni kama haamini, akanisogelea na kunishika mkono, akawa ananitingisha kwa nguvu akitaka nimhakikishie kwamba ni kweli. Nikarudia tena kumueleza vilevile, jambo lililosababisha anikumbatie na kuanza upya kulia.

“Nisamehe! Niliona bora nife tu kuliko kuishi bila wewe, nimejikuta nikikupenda mno mwenzako, utafikiri tulijuana miaka mingi nyuma,” alisema huku akiendelea kulia.

*Usiache kutembelea Simulizi za Majonzi

“Na hizi damu imekuwaje?” aliniuliza, kama nilivyokuwa nikimjibu mwanzo, nikamwambia asiwe na haraka atajua kila kitu kilichotokea. Alinibusu tena, tukaendelea kufanya usafi. Ilibidi nguo zote zilizokuwa zimechafuka kwa damu, tuzikusanye kwa ajili ya kwenda kuzifua, tulitoa kuanzia mashuka mpaka foronya.

Tukasaidiana kupiga deki kwa kutumia sabuni maalum, chumba chote kikawa kisafi kabisa. Baada ya kumaliza, tulibeba furushi la nguo chafu kwa ajili ya kwenda kuzifua kule bafuni lakini wakati tukitoka, baba alikuja kutuambia kwamba nguo hizo hazikutakiwa kwenda kufuliwa bali inabidi zikachomwe moto.

Itabidi mvue hata hizo mlizovaa, zote hizi ni za kuchoma moto, tena inabidi nyie wenyewe kwa mikono yenu. Tulifanya kama baba alivyotuelekeza na muda mfupi baadaye, tulikuwa tumemaliza kila kitu, ikabidi tukaoge tena na safari hii, kila mtu alienda kuoga peke yake. Rahma alinipa fulana yake moja niivae kwani sikuwa na nguo zozote za maana nilizobeba kutoka kule kijijini.

“Baba yako amenipa hii pesa anasema muende sehemu yoyote nzuri mkatembee na Togo, hata kama ni ‘beach’ ila msichelewe kurudi,” alisema mama yake Rahma huku akitoa noti mbili nyekundu na kumpa Rahma.

“Lakini mama, naomba unisamehe!”

“Usijali, tumeshakusamehe Rahma, tunamshukuru Mungu kwa kukuokoa kutoka kwenye bonde la mauti. Jioni mtapenda kula nini?” alisema mama yake Rahma kwa upole wa ajabu.

Hata mimi nilishangaa sana, nilitegemea kwamba baada ya kila kitu kutulia, lazima mimi na Rahma tulikuwa na kesi ya kujibu lakini mambo yakawa tofauti kabisa.

“Nataka tule pilau, si ndiyo Togo,” alijibu Rahma, na mimi nikatingisha tu kichwa. Kule kijijini kwetu, pilau lilikuwa likipikwa sikukuu tu, tena Krismasi, nikajikuta nikijilamba midomo yangu kwa uchu. Baada ya hapo, mama yake Rahma alitoka na kututakia matembezi mema.

“Twende wapi kutembea,” alisema Rahma huku akinikumbatia na kunibusu, nikamwambia mimi sijui sehemu yoyote kwa hiyo yeye ndiyo aniongoze, akacheka sana na kunipiga mgongoni. Yaani kama kuna mtu alimuona Rahma saa chache zilizopitahali aliyokuwa nayo, asingeamini kwamba ndiye yeye.

Harakaharaka alianza kujiandaa, akaenda tena kuoga na kurudi chumbani kwake, mimi nikawa nimekaa kwenye kiti cha pembeni. Niweke wazi kwamba safari hii sikuwa naogopa chochote ikwa sababu baba na baba yake Rahma ndiyo walioniruhusu kuwa karibu na Rahma wakihofia kwamba kama wataendelea ukali juu yetu, anaweza kujidhuru tena.

Na waliniambia natakiwa nisimuache peke yake kule chumbani kwake kwa hiyo nilikuwepo pale kihalali kabisa ingawa waliniambia kwamba sitakiwi kufanya chochote naye kwa sababu kulikuwa na mambo yasiyo ya kawaida wameyabaini na chanzo cha yote ilikuwa ni mimi kufanya naye mapenzi.

“Hebu niambie Togo, unanipenda kweli kama mimi ninavyokupenda?”

“Nakupenda tena sana,” nilimwambia, nikamuona akiachia tabasamu pana, akanisogelea pale nilipokuwa nimekaa, akanishika mkono na kunivuta ili nisimame, nikatii, alinivutia kifuani kwake na kunibusu kimahaba, na mimi nikafanya kama yeye.

*Usiache kutembelea Simulizi za Majonzi

“Kama kweli unanipenda nataka unioe,” alisema Rahma kwa sauti ya kunong’ona, akanibusu tena.

“Usijali kabisa, kwako nipo tayari kwa chochote,” nilimwambia. Kiukweli nilimjibu tu kwa lengo la kumfurahisha maana niliambiwa sitakiwi kumuudhi kwa chochote. Baada ya hapo, aliniachia na kwenda kufungua kabati, akaniambia nimsaidie kuchagua nguo ya kuvaa.

Kwangu ulikuwa mtihani mkubwa sana kwani wakati mwingine alikuwa akiiachia ile khanga aliyotoka nayo bafuni na kuufanya mwili wake wenye mvuto wa kipekee ubaki wazi, nikawa na kazi ya ziada. Baadaye aliipata nguo aliyoitaka mwenyewe, akavaa gauni zuri lililompendeza na kujitanda ushungi.

Kwenye suala la mavazi, Rahma alikuwa akijitahidi sana, alikuwa akivaa mavazi ya heshima tofauti na wasichana wengi wa mjini. Mimi sikuwa na cha kubadilisha, vilevile nilivyokuwa nimevaa, tulitoka, nikataka kuvaa mabuti yangu lakini akaniambia kuna raba nzuri huwa anafanyia mazoezi, akaingia tena ndani na kutoka nazo.

Zilinipendeza vizuri, nikawa nachekacheka tu, tulienda sebuleni na kuaga, ndugu zangu waliokuwa wamenogewa na tivii, walinitazama kwa macho ya wivu, tukatoka mpaka nje ambapo Rahma alipunga mkono upande kulipokuwa kumepaki Bajaj, ikaja moja, tukaingia na kukaa.

“Tupeleke Coco Beach, kule wanakouza mihogo,” alisema Rahma, safari ikaanza lakini mita chache mbele, nilishtuka baada ya kusikia mtu akiliita jina langu kwa nguvu, tena sauti yenyewe ilikuwa ya kike, ilibidi Rahma amwambie dereva asimame, tukageuka nyuma kutazama ni nani aliyekuwa ananiita kwa sababu mimi nilikuwa mgeni na hakuna mtu yeyote aliyekuwa akilifahamu jina langu zaidi ya wale tuliokuwa tukiishi pamoja.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya Simulizi za Majonzi.

Leave A Reply