The House of Favourite Newspapers

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 41

0

ILIPOISHIA:

Nikiwa bado nashangaa, mwili ukiwa unatetemeka kwa hofu, nilishtukia wale watu wakikimbilia pale kwenye moto na kujipanga foleni, yule babu akasogea kwenye zile nyama, akawa anagawa, kila mmoja anapita na kupewa kipande chake kisha anatafuta sehemu ya kwenda kukaa na kuanza kula. Nilihisi kama nipo ndotoni lakini haikuwa hivyo.

“Hongera, umekuwa sasa,” alisema baba huku akinikumbatia, akanishika mkono na kunipeleka kwenye foleni, akaniingiza kwenye foleni.

SASA ENDELEA…

“Hapana baba, siwezi! Siwezi…” nilisema huku nikitaka kutoka kwenye foleni lakini baba alinishika mkono kwa nguvu. Nilikuwa natafuta upenyo ili nijitie vidole mdomoni kujitapisha ile nyama lakini ni kama baba alinishtukia.

Hakunipa upenyo hata kidogo, nikawa naendelea kutetemeka kwa hofu kubwa, nikiwa sielewi hatima ya yote yale itakuwa nini. Tofauti na mimi, watu wengine wote waliokuwepo eneo lile, akiwemo baba, baba yake Rahma na wale watu wengine wote, walikuwa na furaha kubwa ndani ya mioyo yao.

Kingine kilichonishangaza na kuniacha na maswali mengi, kila mtu aliyekuwa akifika pale mbele kwa yule babu aliyekuwa akigawa nyama, akikabidhiwa yake alikuwa akifurahi sana na kwenda kukaa pembeni na kuanza kuila bila wasiwasi wowote.

Nimewahi kusikia sana kuhusu stori za watu wanaokula nyama za watu lakini siku zote nilikuwa naona kama ni mambo ya kutunga, iweje mtu amle mwenzake? Ni hapo ndipo nilipoelewa kwamba kumbe siyo stori za kusadikika tu bali ni mambo ambayo yapo na yanafanyika kwa wingi.

Nilijiuliza sana, wale waliokuwa wakiliwa nyama ni akina nani? Walifanya makosa gani mpaka waliwe? Walikuwa wanaishi wapi na nyama zao zilifikishwaje pale? Je, walikuwa wanaume au wanawake, wakubwa au wadogo? Sikuwa na majibu.

Foleni ikawa ikazidi kusogea mbele, mwili wangu ulikuwa na maumivu sehemu mbalimbali, hasa yale maeneo ambayo yule babu alikuwa amenichanja lakini huwezi amini, kwa jinsi nilivyokuwa na hofu, wala sikuwa nasikia chochote.

Foleni iliendelea kusogea mbele, hofu ikazidi kunijaa lakini sikuwa na cha kufanya. Mara nilipata wazo, kwamba nikifika na kupewa nyama yangu, nijifanye naenda pembeni kuila lakini nikifika pembeni niitupe na tukirudi nyumbani, nitoroke na kurudi Chunya maana sikuwa tayari kwa kile kilichokuwa mbele yangu.

>>> Usikose kutembelea Simulizi za Majonzi

Ni kweli mara kadhaa nilijikuta nikitamani kuzijua mbinu mbalimbali za kichawi, kama kuweza kujilinda kwenye nyakati za hatari au kumuadhibu anayekuudhi lakini sikuwa tayari kuona nakuwa sehemu ya jamii hiyo iliyokuwa na mambo ya kutisha kiasi hicho.

Hatimaye zamu yangu iliwadia, yule mzee mgawaji, huku akijitafuna na damudamu zikiwa zimelowanisha mdomo wake, alinitazama usoni huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.

Kuna kipande alikuwa amekishika mkononi lakini alipoona ni mimi, nilimuona akikirudisha pale chini palipokuwa na nyama nyingine nyingi, zikiwa zimewekwa juu ya majani ya migomba, akachaguachagua na muda mfupi baadaye, aliibuka na mnofu mkubwa wenye damudamu, akanipa huku akiinamisha kichwa kama ishara ya heshima.

Huku nikitetemeka nilipokea, macho yangu yakiwa hayatulii, nilikuwa nikilichunguza kwa umakini lile rundo la nyama pale chini ambalo sasa lilikuwa limepungua sana. Nilichokiona awali ndicho nilichokiona tena, kulikuwa na miguu iliyokatwa, viganja vya mikono na viungo vingine vya mwili.

Nikiri kwamba moyo wangu haujawahi kupatwa na hofu kama niliyoipata siku hiyo na kilichonitisha zaidi, ni pale nilipogundua kwamba katika rundo lile, kulikuwa na miguu na mikono ya watoto wadogo kabisa. Maskini… hawakuwa na hatia yoyote!

Baba naye alipewa kipande chake, akanishika mkono huku akiniongelesha kwa sauti ya chini. Aliniambia kwamba nina bahati sana kupewa heshima kubwa kama hiyo na mzee huyo ambaye baba aliniambia huwa wanamuita Mkuu kwa sababu ndiye kiongozi wao wa kanda. Akaniambia kwamba kitendo cha yeye kuinamisha kichwa chake tu, ilikuwa ni ishara kwamba amenikubali mno.

Hatukwenda mbali, tulikaa chini huku baba akinielekeza namna ya kukaa. Haukuwa ukaaji wa kawaida, mguu wa kushoto ulikuwa ukitangulia chini, kisha unakuja wa kulia halafu unakaa juu ya vifundo vya miguu yote miwili huku ukiwa umeikunja na kutengeneza alama ya V mbili.

Nilijaribu lakini miguu ikawa inaniuma sana, nilipowatazama watu wengine, wote walikuwa wamekaa kwa mtindo huo na wala hakukuwa na aliyekuwa akibabaika kama mimi, walikuwa wakiendelea kupiga stori za hapa na pale huku wakifurahia ‘kitoweo’, baba akaniambia atanifundisha taratibu.

Lile wazo langu la kwenda kuitupa ile nyama liliyeyuka kutokana na baba alivyonibana, ambapo muda mfupi baadaye, baba yake Rahma naye alikuja na kuungana na sisi pamoja na wanaume wengine watatu ambao sikuwa nawafahamu.

Kwa muda wote huo nilikuwa nikizugazuga tu kwani kiukweli sikuwa tayari kuila ile nyama ambayo ilikuwa ikichuruzika damu, mara kwa mara nilikuwa nikiitazama kwa woga, nikitamani hata niirushe mbali na kupiga kelele kwa hofu lakini haikuwezekana.

“Kula, muda unaenda,” baba aliniambia kwa kunihimiza, wale watu wengine ambao sikuwa nawafahamu, wakawa wanamuuliza baba mimi ni nani.

“Ni mwanangu, hamuoni tunavyofanana,” aliwajibu na wote wakawa wanampongeza kwa hatua ya kunisajili rasmi, wakawa wananipongeza na mimi wakiniambia kwamba sitajuta kujiunga na jamii yao. Kwa kuwa wote sasa walikuwa wakinitazama huku wakiendelea kunisifia, ilibidi nijikaze kiume maana baba alikuwa akinitazama kwa jicho kama la kunidharau hivi au kuonesha kwamba zile sifa nilizokuwa napewa sistahili.

>>> Usikose kutembelea Simulizi za Majonzi

“Umekua sasa si ndiyo?” baba yake Rahma aliniambia huku akinipigapiga begani na mkono wake uliokuwa na damu, mdomoni akiendelea kujitafuna. Nadhani aliongea hivyo kama kunikumbusha kile tulichokuwa tukitofautiana mara kwa mara na baba, akidai kwamba mimi bado nina akili za kitoto.

“Ndiyo,” nilimjibu kwa msisitizo, nikafumba macho na kupeleka ule mnofu mdomoni, nikaziba pua ili nisisikie hata harufu nikaanza kutafuna huku nikijikaza kisawasawa, sikuwa nataka kuonekana bado nina akili za kitoto kwa hiyo nilijikuta nikifanya kitu nisichopenda kukifanya ilimradi tu nimdhihirishie baba na baba yake Rahma kwamba sikuwa mtoto tena.

Mara kadhaa nilikuwa nikitaka kutapika lakini mwisho, hatimaye nilifanikiwa kuitia yote tumboni mwangu na kuufanya mwili wangu usisimke sana.

“Tafuna hii,” alisema baba yake Rahma huku akinipa vitu kama mizizi fulani hivi, nikavitafuna haraka na kuvimeza. Cha ajabu, mpaka muda huo, kumbe mimi ndiye niliyekuwa wa mwisho kumaliza ‘shea’ yangu, watu wote walikuwa wameshamaliza na sasa walikuwa wakipiga stori za hapa na pale.

“Vipi una swali lolote kwa kijana?” baba yake Rahma alimwambia baba kwa kejeli, nilishaelewa kwa nini amesema vile. Kwamba kwa sababu baba alikuwa ananiona kama nina akili za kitoto, je alikuwa na swali lingine lolote baada ya mimi kuonesha kile nilichokionesha pale mbele yao?

“Umenitoa aibu mwanangu, zawadi nitakayokupa hautakuja kuisahau maishani mwako,” aliniambia baba akionesha kuwa na furaha kubwa.

Mara sauti ya kama pembe la ng’ombe lililopulizwa kwa nguvu ilisikika, watu wote wakainuka walipokuwa wamekaa na kuanza kujipanga kwa mtindo wa duara kama ilivyokuwa mwanzo.

“Sasa hivi unaenda kukabidhiwa rasmi nguvu za giza ili uwe kama sisi, naomba ujasiri uliouonesha kwenye kula uuoneshe hapa pia, nenda pale ulipokuwa umekaa mwanzo,” baba aliniambia huku akinipigapiga begani kwa upole.

Kwa akili yangu nilijua kwamba tayari kazi imekwisha, kumbe kulikuwa na kazi nyingine, nikaanza kutetemeka tena huku nikigeuka huku na kule kuwatazama wale watu ambao wote walikuwa na nyuso za furaha. Nilipogeuka upande wa kushoto, nilimuona mtu aliyenifanya nishtuke mno, nilifikicha macho nikiwa ni kama siamini.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya Simulizi za Majonzi.

Leave A Reply