The House of Favourite Newspapers

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 43

0

ILIPOISHIA:

“Hapana! Hapanaaa,” nilisema kwa sauti ya juu, ikabidi baba anizibe mdomo maana alihisi naweza kuropoka mambo mengine na kuwafanya wasiohusika wajue.

“Huna haja ya kuogopa, zipo njia za kutimiza hicho ulichoambiwa bila kuonekana kama wewe ndiyo umefanya moja kwa moja, mbona sisi huwa tunafanya sana tu,” alisema baba, macho yakanitoka.

SASA ENDELEA…

Aliondoa mkono wake mdomoni mwangu, akaniambia wameniamini ndiyo maana wameniunganisha kwenye jamii yao, akaniambia faida nitakazozipata ni nyingi na kubwa sana kwa hiyo sina sababu ya kuogopa kutimiza sharti lile dogo nililopewa.

“Sijawahi kuua mtu hata siku moja, nitaanzaje,” nilisema, baba akatabasamu na kumgeukia baba yake Rahma, wakacheka na kugongesheana mikono. Sikuelewa kwa nini wao wacheke wakati mimi nilikuwa kwenye hali mbaya kiasi hicho, hofu kubwa ikiwa imetanda kwenye moyo wangu.

“Unatakiwa ujue namna ya kudhibiti hofu yako, ukiwa mwoga hivi huwezi kufanya chochote,” alisema baba, baba yake Rahma akamuunga mkono, wakawa wananieleza kwamba mtihani niliopewa ni mdogo sana na endapo nitashindwa nitakuwa nimewaangusha sana na kila mtu atanicheka.

“Utathibitisha kwamba kauli yangu niliyoitoa juu yako ni sahihi.”

“Kauli gani?”

>>>Usikose kutembelea Simulizi za Majonzi

“Kwamba wewe bado una akili za kitoto,” baba alisema. Hakuna kitu nilichokuwa sikipendi kama kusikia kauli za namna hiyo kutoka kwa baba, nikajikuta morali fulani ukinipanda ndani kwa ndani, nikajisemea kwamba nitamuonesha kwa vitendo kama mimi siyo mtoto.

“Endelea kupumzika mpaka mwili upate nguvu, tutakuja baadaye kukuelekeza nini cha kufanya,” alisema baba, wakatoka na kuniacha nimelala palepale kitandani. Kwa nje nilisikia wakifunga mlango kwa funguo, nikabaki nashangaa kwa nini wananifungia?

Sikuwaza sana kuhusu hilo la mlango, bado nilikuwa na mawazo mengi juu ya hatma yangu na ile kazi niliyokuwa nimepewa. Sikuwahi kudhani hata siku kwamba eti na mimi naweza kuwemo kwenye orodha ya wachawi, tena wanaoua na kula nyama za watu wasio na hatia.

Ni kweli kuna kipindi nilikuwa nikitamani kuwa na nguvu kama za baba lakini nilichokuwa nikikijua ni kwamba nguvu zake zilikuwa ni za kutibu watu na kufanya yale yasiyowezekana tu, sikujua kuwa gharama zake ni kubwa kiasi hicho.

Sikupata jibu mtihani mkubwa uliokuwa mbele yangu ningeuvuka vipi, sikujua ni kwa kiasi gani moyo wangu utakuwa na hatia kwa kuyakatisha maisha ya mtu asiye na hatia. Kuna wakati nilikuwa nikitamani kama nitoroke na kuelekea kusikojulikana lakini kila nilipokuwa nikifikiria vile vitisho nilivyokuwa napewa, nilijikuta nikikosa ujanja.

Nilipokumbuka na kauli za baba za kunidharau, nilijikuta nikizidi kuchanganyikiwa, sikuelewa nini itakuwa hatma yangu. Basi niliendelea kuwaza na kuwazua pale kitandani, mwili ukaanza kupata nguvu taratibu, saa zikawa zinazidi kuyoyoma.

Mida ya jioni baba alikuja tena, akafungua mlango na kuingia akiwa na bakuli lililokuwa na supu ya kuku wa kienyeji. Akaniwekea vizuri na kuniambia niinuke mwenyewe pale kitandani. Kwa kuwa safari hii nilikuwa na nguvu, niliinuka mwenyewe na kukaa kitako.

Akanisogezea lile bakuli na kunipa. Nililipokea huku mikono ikitetemeka, nikaanza kuinywa supu ile kwa pupa. Muda mfupi tu baadaye, bakuli lilikuwa tupu. Ile njaa niliyokuwa nayo sasa ilikuwa imepungua na nilijihisi kuwa na nguvu kama zamani.

“Hebu jaribu kusimama mwenyewe,” baba aliniambia wakati akikusanya mifupa na kuiweka kwenye lile bakuli, nikajishikilia kwenye kingo za kitanda na kusimama. Bado miguu haikuwa na nguvu vizuri lakini niliweza kusimama, akaniambia nizunguke mle ndani, kweli nikaweza.

“Safi sana, sasa umekuwa mwanaume kamili,” aliniambia huku akinielekeza kuendelea kupumzika mpaka usiku. Nilirudi kitandani na kujilaza, kidogo nikawa najisikia vizuri, baba akatoka na kufunga tena mlango kwa ndani.

Kiukweli nilikuwa nimemkumbuka sana Rahma, sikujua anawaza nini juu yangu maana siyo kawaida tukae wote nyumba moja halafu tusionane siku nzima. Nilitamani japo nipate muda mfupi wa kuonana naye, nimweleze kinachonitokea maishani mwangu maana angeweza kuhisi kama labda simpendi tena na ndiyo maana nimebadilika.

Muda ulizidi kuyoyoma na hatimaye giza likaingia, mara nikasikia mlango ukifunguliwa. Walikua ni baba na baba yake Rahma, waliingia na kuwasha taa, wakanisogelea mpaka pale kitandani.

“Vipi unaendeleaje?”

“Naendelea vizuri.”

“Safi, sasa inatakiwa tuondoke kuna mahali tunaenda kukuonesha sehemu tunapochimba dawa zetu za kufanyia kazi,” baba aliniambia, nikainuka na kukaa vizuri.

“Kwa mfano hiyo kazi uliyopewa, huwezi kuifanikisha kwa urahisi mpaka uwe na dawa na inabidi dawa hizo ukachimbe wewe mwenyewe, kwa hiyo sisi tunachokifanya ni kukuelekeza tu, mambo mengine utafanya mwenyewe ikiwa ni pamoja na kujifunza kwa vitendo,” alisema baba.

Sikuwa na cha kujibu zaidi ya kuinuka, nikataka kwenda kuoga lakini baba alinikataza, akasema sitakiwi kuoga kwa muda wa siku saba, nikashangaa sana. Aliniambia nivae nguo zangu tuondoke haraka maana tulikokuwa tukienda ni mbali.

Ilibidi nifanye kama walivyoniambia, nilivaa nguo zangu vizuri, baba akafungua mlango na kutangulia, kabla hajatoka aliniambia kwamba kila tunakoenda, sitakiwi kutangulia mbele wala kubaki nyuma, muda wote niwe katikati yao.

Sikuelewa maana ya maelekezo yake hayo ila nilitii, akatangulia, nikafuata halafu baba Rahma akafuatia nyuma. Nikiri kwamba baada ya yale yote yaliyotokea, nilikuwa nikiwatazama baba na baba yake Rahma kwa jicho tofauti kabisa. Hata sijui nieleze vipi lakini kwa kifupi nilikuwa nikiwatazama kwa jicho la tofauti.

Tulitoka moja kwa moja mpaka nje na nadhani hakuna mtu yeyote aliyetuona, tulitoka mpaka pale nje kabisa palipokuwa na maegesho ya Bajaj na bodaboda.

“Yule jamaa aliyekamatwa kwa mauaji ameachiwa? Sijui kama tutapona mtaa huu,” nilimsikia dereva bodaboda mmoja akiwaambia wenzake, akimaanisha mimi. Nilijua kwamba ananizungumzia mimi maana hata siku ile nilipokuja kuchukuliwa na polisi pale nyumbani, yeye ndiyo alikuwa kiherehere wa kuwasimulia wenzake kwamba eti mimi nimemuua mtu gesti.

Nilijikuta nimepandwa na jazba, nikatamani kama nimrukie na kumtandika makofi kwa hasira. Hakuna kitu ambacho huwa sikipendi kama dharau. Kumbe wakati nikifikiria nini cha kufanya, baba na baba yake Rahma walishajua ninachowaza.

“Hutakiwi kuwa na hasira zisizo na msingi, muache afurahishe mdomo wake,” alisema baba yake Rahma huku akinipigapiga begani. Nilishusha pumzi ndefu, baba akazungumza na dereva mmoja wa Bajaj, tukaingia na mimi nikakaa katikati.

>>>Usikose kutembelea Simulizi za Majonzi

“Tupeleke Ubungo,” alisema baba, safari ikaanza. Ubungo hapakuwa pageni kwangu kwani ndiyo sehemu ya kwanza kukanyaga tuliposhuka kwenye basi tukitokea Chunya. Basi tulienda mpaka Ubungo, tulipofika baba alimlipa dereva, tukavuka kwenye mataa ya kuongozea magari na kwenda upande wa pili mpaka kwenye stendi ya daladala.

Tulipanda kwenye gari moja, hata sijui linaelekea wapi, tukaenda kukaa siti ya nyuma kabisa, mimi nikiwa katikati.

“Kwani tunaenda wapi?”

“Tunaenda Kibaha,” alisema baba, nikashindwa kumhoji chochote maana hata huko kibaha kwenyewe sikuwa nakujua.

Baadaye gari liliondoka, ikiwa ni majira ya kama saa tatu za usiku, tukaenda mpaka tulipofika Kibaha, tukashuka na kuanza kutembea kwa miguu. Tulivuka barabara, nikaona kuna kibao kimeandikwa Tumbi Hospital, nimewahi sana kuisikia hii hospitali kwani mara nyingi ajali nyingi zinazotokea mkoa wa Pwani majeruhi au maiti huwa zinapelekwa Tumbi.

Basi tulianza kutembea kuifuata barabara hiyo, giza nalo likawa linazidi kuwa nene, tukatembea umbali mrefu, tulipofika kule juu kabisa, tuliiacha barabara ya lami na kuingia vichakani, nako tukatembea umbali mrefu sana, hatimaye tukatokezea kwenye eneo lililokuwa na vichana vifupivifupi.

Kwa kutumia tochi aliyokuwa nayo, baba alianza kumulika kwenye vile vichaka kama anayetafuta kitu, mimi na baba yake Rahma tukawa tunamfuata kwa nyumanyuma maana kama nilivyosema, mimi sikutakiwa kutangulia mbele wala kubaki nyuma kwa hiyo ilikuwa ni lazima tutembee watatuwatatu.

“Unauona huu mti, unaitwa mtunguja, huu ndiyo hutumika sana kutengeneza ajali za kichawi na unapatikana kwa wingi eneo hili na ndiyo maana huku kila siku unasikia ajali mbayambaya zinatokea maana wanafunzi kama wewe, huku ndiyo eneo la kujifunza kwa vitendo,” alisema baba huku akianza kufukua kwenye shina la mti huo mdogo.

“Sifa yake moja, huu mtu huwa unatoa damu,” alisema baba, akatoa kisu na kubandua sehemu ndogo ya ganda lake, nikashangaa kweli mti ukitoa vitu vilivyokuwa vikifanana kabisa na damu.

“Niangalie vizuri namna ya kuchimba maana tukitoka hapa inabidi na wewe ukafanye majaribio kama wenzako,” alisema baba. Muda huo ulikuwa ni kama saa sita hivi za usiku, giza nene likiwa limetanda kila sehemu.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya Simulizi za Majonzi.

Leave A Reply