The House of Favourite Newspapers

Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 5

0

ILIPOISHIA:

MWANAUME mzee mwenye macho mekundu sana na midomo myeusi, akiwa amejifunga shuka refu lenye rangi nyekundu na nyeusi, kichwani akiwa amejifunga kitambaa cheusi, shingoni akiwa na hirizi kadhaa na shanga, alisimama na kunyoosha juu mkia wa mnyama ambaye sikuwa namjua, watu wote wakashangilia kwa nguvu.

SASA ENDELEA…

“Sina mengi ya kuzungumza, naomba ushirikiano wenu tuwakomeshe wachawi wa kijiji hiki,” alisema mwanaume huyo kwa Kiswahili kibovu, watu wakashangilia tena kwa nguvu kisha Mwene akaendelea na maelezo, akisisitiza kwamba kazi lazima ianze siku hiyohiyo usiku.

Baada ya maelezo marefu yaliyojaa vitisho kwa watu waliokuwa wakitajwa kuhusika na uchawi, mkutano uliahirishwa, watu wakatawanyika huku kiongozi huyo wa kijiji akiwataka watu wote kutoa ushirikiano kwa mganga Mabwanji atakapoenda kuwatembelea kwenye nyumba zao.

Hofu niliyokuwa nayo ilikuwa kubwa mno, kwa jinsi watu walivyokuwa wanatuchukia pale kijijini nilijua lazima moto utawaka. Baadhi ya wazee waliokuwa wanaheshimika pale kijijini, walianza maandalizi ya kumsaidia mganga huyo kwa kila alichokuwa anakihitaji, dawa zikaandaliwa na hatimaye muda uliokuwa ukisubiriwa na wengi ukawadia.

Saa tatu juu ya alama usiku, kazi ya kuzunguka kwenye nyumba za watu waliokuwa wakishukiwa kuwa wachawi ilianza, kutokana na jinsi nilivyokuwa na shauku kubwa ya kutaka kuona kazi hiyo inavyofanyika, nilichomoka nyumbani kimyakimya na kwenda kushuhudia licha ya kwamba baba alitutaka wote tukae ndani kwa sababu siku hiyo ilikuwa mbaya kwa familia yetu.

Mtu wa kwanza kufuatwa alikuwa ni mwanamke mjane ambaye tulizoea kumuita mama Chinga, Mmakonde kutoka Kusini ambaye alikuwa akifanya kazi ya kupika pombe za kienyeji.

Kwa kipindi kirefu nilikuwa nikisikiasikia kwamba eti mwanamke huyo alikuwa akitumia viungo vya binadamu kupikia pombe zake ndiyo maana alikuwa na wateja wengi sana hapo kijijini. Tangu nikiwa mdogo niliaminishwa kwamba eti ule ambao huwa tunaona kama ni mwiko mkubwa anaoutumia kukorogea mapipa yake ya pombe, ulikuwa ni mkono wa binadamu.

Watu hao walipofika, huku ngoma ikipigwa na pembe za wanyama zikipulizwa, kila mtu akiwa ameshika tochi za kienyeji ambazo hutengenezwa kwa kuviringisha matambara mbele ya kipande cha mti kisha kuchovya kwenye mafuta ya taa, nyumba yake ilizungukwa kisha mganga akaanza kazi yake.

Akawa anafanya uchawi wake pale, mara afukue kwenye kona ya nyumba na kutoa hirizi kubwa, mara afukue pembeni ya mlango na kutoa fuvu la mnyama wa ajabu, yaani ilikuwa ni patashika nguo kuchanika.

Mwanamke huyo na yeye akatolewa na kukalishwa chini, mbele ya nyumba yake, akapakwa unga mweupe kichwani na kuanza kunyolewa nywele huku ngoma zikiendelea kupigwa, mganga akawa anaimba nyimbo za ajabu na kumtolea vitisho vingi mwanamke huyo kwamba akirudia tena kujihusisha na uchawi lazima atakufa.

Baada ya zoezi hilo lililochukua karibu saa zima, watu wote waliondoka na kumuacha mwanamke huyo akilia kwa uchungu, huku akiendelea kusisitiza kwamba yeye siyo mchawi wala haujui uchawi. Safari ya kuelekea kwenye nyumba nyingine ikaanza, na mimi nikawa nawafuata kwa nyuma.

Cha ajabu, niliwaona wakielekea nyumbani kwetu, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio kuliko kawaida, sikujua mwisho wake utakuwaje. Walipofika, walifanya kama walivyofanya kwa yule mwanamke, wakaizunguka nyumba yetu huku wakiimulika na tochi za kienyeji, ngoma ikawa inapigwa huku mganga akiimba nyimbo ambazo hakuna aliyekuwa anazielewa.

Akawa anazunguka huku na kule kama anayetafuta kitu fulani pale nje kwetu, ghafla nikaona mlango ukifunguliwa, baba akatoka kwa kasi na kuwapita watu wote, akasogea mpaka pale yule mganga alipokuwa amesimama, wakawa wanatazamana.

“Ni nani aliyekupa mamlaka ya kuingia kwenye miji ya watu na kutapeli ukijifanya unawatoa watu uchawi?”

“Wewe ni nani wa kunihoji maswali hayo? Wewe ni mchawi na wanakijiji wenzako wamekuchoka hapa kijijini. Hii safari ya ujio wangu ni kwa ajili yako, lazima nikunyooshe.”

“Wewe bado ni mwepesi sana kwangu, huna ubavu wa kushindana na mimi. Isitoshe mimi siyo mlozi kama wewe, mimi ni mtaalamu, tena gwiji,” alisema baba kwa sauti ambayo niliisikia vizuri kisha baada ya hapo akageuka na kurudi ndani, nikamuona yule mganga akivuta na kutoa pumzi ndefundefu kama anayejiandaa kufanya tukio moja kubwa sana.

Alipoingia ndani na kufunga mlango, huku nje yule mganga aliendelea kuzunguka huku na kule, wasaidizi wake wakawa wanampigia manyanga na kumuimbia nyimbo ambazo walizielewa wenyewe.

“Inatakiwa tumkamate kwa nguvu na kumtoa nje, anaonyesha ni jeuri sana,” alisema mganga huyo kwa Kiswahili kibovu, watu wote wakawa wanatingisha vichwa kuonyesha kukubaliana na alichokuwa anakisema.

Nilijikuta nikitetemeka sana pale nilipokuwa nimejibanza, nikajua arobaini za baba zilikuwa zimewadia. Japokuwa bado sikuwa na majibu kamili kichwani mwangu kama baba ni mganga au mchawi, bado sikukubaliana na kitendo alichokuwa anataka kufanyiwa kwa sababu ulikuwa ni udhalilishaji wa hali ya juu.

Wakati kundi la wanaume wakijiandaa kuingia ndani kwa nguvu na kuvunja mlango, nilimuona baba akitoka kwa kujiamini, kifua akiwa amekitanguliza mbele na kusimama tena mbele ya mganga, wale watu wote wakamzunguka kisharishari.

“Mnataka kutumia nguvu kunikamata? Hivi mna akili timamu nyie? Haya mwenye ubavu anyooshe mkono wake na kunigusa,” alisema baba kwa hasira. Nilibaki namshangaa baba kwani sikujua amepata wapi ujasiri wa kiasi kile. Kauli hiyo iliwashtua hata wale watu waliokuwa wanataka kumkamata, nikaona wote wakirudi nyuma lakini mganga aliendelea kusisitiza kwamba ni lazima wamkamate kwa nguvu.

Watu wote walipojaribu kufanya hivyo, tulishtuka kuona kimbunga kikubwa ambacho hata sikujua kimetokea wapi, kikianza kuvuma kwa nguvu pale baba alipokuwa amesimama, vumbi jingi na takataka za kila aina zikawa zinarushwa huku na kule, kufumba na kufumbua, baba hakuwepo tena eneo hilo.

Wale watu wote, akiwemo na mganga mwenyewe, walibaki wamepigwa na butwaa, kila mmoja akawa anajifuta vumbi. Sikuwahi kushuhudia kimbunga kikubwa kikitokea, tena usiku kama ule, nikabaki na maswali mengi yaliyokosa majibu.

“Ametukimbia! Ametukimbia!” alisema yule mganga kwa sauti ya juu, huku na yeye akionyesha dhahiri kuwa na taharuki kubwa ndani ya moyo wake.

“Siwezi kuwakimbia kwa sababu hakuna wa kunitisha hata mmoja kati yenu,” ilisikika sauti ya baba kisha nikashangaa kumuona akitokea gizani na kurudi tena pale alipokuwa amesimama awali, nikaona watu wote wakianza kurudi nyuma kwa hofu kubwa kwa sababu walishajua baba anaweza kufanya chochote muda wowote.

“Nataka hili liwe funzo kwako na kwa watu wengine wenye akili kama zako,” alisema baba kwa kujiamini huku akiendelea kumsogelea yule mganga, akafanya ishara kama ananyonga kitu kwa nguvu, kufumba na kufumbua mganga yule alidondoka chini na kuanza kutapatapa kama anataka kukata roho.

Kuona hivyo, watu wote waliokuwa wameandamana na mganga huyo, walitimua mbio, kila mmoja kuelekea njia yake na muda mfupi baadaye, wote walikuwa wametokomea gizani, ikabidi nitoke pale nilipokuwa nimejibanza huku na mimi nikiwa na hofu kubwa ndani ya moyo wangu.

“Hebu beba huko miguuni tuutoe huu mzoga hapa,” alisema baba, akimaanisha tumtoe yule mganga.

Huku nikitetemeka nilisogea mpaka pale yule mganga alipokuwa amelala, akiendelea kukoroma kwa nguvu, mimi nikamshika miguuni na baba akamshika kichwani, tukaanza kumkokota kumtoa nje ya eneo letu, tukaenda kumbwaga pembeni kabisa kwenye vichaka kisha tukarudi ndani. Ile tunaingia ndani tu, tukasikia mlango ukigongwa kwa nguvu.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya hapa Simulizi za Majonzi.

 

INSTALL GLOBAL PUBLISHERS APP sasa usipitwe na matukio
PAKUA HAPA==>GLOBAL PUBLISHERS APP

FULL VIDEO; Mapambano Ngumi za Global TV – Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Tanzania Bingwa

Leave A Reply