The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 59

ILIPOISHIA:
Kilichotokea baada ya kufanya hivyo kwa mara ya tatu, kilinifanya nihisi kama mwili wangu unakufa ganzi kwa hofu, sijawahi kushikwa na hofu kama niliyoipata siku hiyo na kama baba asingeniwahi, huenda ningedondoka kama mzigo chini maana mwili wote uliisha nguvu.
Japokuwa ilikuwa ni usiku, tena nikiwa sina nguo na kulikuwa na baridi kali, nilihisi kijasho chembamba kikinitoka, ama kweli duniani kuna mambo na ukishangaa ya Musa, utayaona ya Firauni.
SASA ENDELEA…
Kitendo cha kufuata maelekezo yale tu, mara kaburi lilifunuka lote, yaani ule udongo wote uliokuwa umetumika kulifukia, ukapotea kiasi kwamba kila kitu kilichokuwa ndani ya kaburi kilikuwa kikionekana.
“Ingia tukasaidiane kumtoa kwenye jeneza,” alisema baba, nikajikuta nguvu za kuendelea kusimama zimeniisha maana miguu ilikuwa ikitetemeka kuliko kawaida, nikakaa kwenye kaburi lililokuwa pembeni, uso wote ukiwa umelowa kwa machozi.
Ni hapo ndipo nilipoelewa kwa nini baba alikuwa akiniambia kwamba bado sijakomaa kiakili na sitakiwi kuingizwa kwenye hayo mambo.
“Inuka acha kuleta mambo ya kijinga hapa, upumbavu wako ndiyo uliotufikisha hapa,” alisema baba kwa ukali, nikajikakamua na kusimama huku nikiwa bado natetemeka. Alichokifanya baba baada ya kuona kama nasuasua, alinisukumia ndani ya lile kaburi, nikaporomoka na kwenda kujibamiza kwenye jeneza.
Nilijikuta nikipiga kelele kwa sauti kubwa huku nikitafuta sehemu ya kutokea, kwa kuwa ilikuwa ni ndani ya shimo kelele zangu hata hazikufika mbali, zikawa zinajirudia na kusababishwa mwangwi. Tayari baba naye alishaingia mle kaburini, akaninyamazisha kwa ukali kama kawaida yake.
“Wewe ndiyo unatakiwa uifanye hii kazi, mimi nakusaidia tu,” alisema huku akihangaika kulifungua jeneza lililokuwa na ule mwili.
Nisingependa sana kueleza kuhusu kipengele hiki kwa sababu hata mwenyewe nikikumbuka huwa naogopa sana, lakini kwa kifupi, nilisaidiana na baba kuutoa ule mwili kwenye jeneza, sanda yote ikiwa imelowa damu hasa maeneo ya kichwani inakoonesha marehemu aliumia sana kwenye ile ajali.
Tukautoa na kuulaza pembeni ya kaburi huku lile jeneza baba akilirudishia kama lilivyokuwa mwanzo. Huku nikitetemeka kuliko kawaida, baba aliniamuru tena kufanya kama nilivyofanya mwanzo, nikafanya mara ya kwanza, ya pili, kisha nikafanya mara ya tatu.
Cha ajabu kaburi lilijifukia vilevile na kurudi kama lilivyokuwa mwanzo, tofauti yake ni kwamba kidogo lilikuwa limetitia. Ni hapo ndipo nilipoamini kauli niliyokuwa nikiisikia kwa muda mrefu, kwamba ukiona kaburi jipya limetitia sana, kuna uwezekano mkubwa kwamba kilichozikwa ndani siyo mtu au kama ni maiti, basi imechukuliwa na wachawi.
Baada ya zoezi hilo kukamilika, baba aliniamuru niibebe ile maiti huku baba yake Rahma akinitoa hofu kwamba mtu akishakufa hana madhara yoyote, hawezi kunidhuru kwa namna yoyote, nikajikakamua na kuiweka begani, tukaanza kuondoka makaburini hapo huku ikichuruzika vitu ambavyo hata bila kutazama nilijua ni damu.
Unajua baadaye nilikuja kujifunza kitu kingine, kwamba watu wanaofariki katika mazingira ya kishirikina, unaweza kutambua maiti zao kwa haraka kama na wewe una uelewa kuhusu mambo hayo, kwa sababu kwanza imezoeleka kwamba mtu akifa mwili wake hupoa na kuwa wa baridi sana lakini kama amekufa kwa mipango ya watu, mwili huendelea kuwa na joto kwa muda mrefu.
Pia maiti za namna hii zinakuwa na kawaida ya kutoka damu. Inafahamika kwamba mtu akifa, moyo unakuwa umeacha kusukuma damu kwa hiyo hata mzunguko mzima wa damu nao unasimama lakini kwa watu waliochukuliwa kabla ya muda wao, japo kwa nje anaonekana amekufa, bado mzunguko wa damu unakuwa unaendelea japo kwa kasi ndogo sana na ndiyo maana, utakuta maiti inatoka damu puani, mdomoni, masikioni au kama ni ya ajali kama hiyo, majeraha yanakuwa yanaendelea kuchuruzika damu.
Tulitoka huku nikijikaza kiume na ule mwili begani kwa sababu ulikuwa mzito sana lakini kwa kuwa na mimi kidogo nilikuwa na ubavu, niliweza kuhimili uzito huo mpaka kwenye mti mkubwa uliokuwa pembeni ya makaburi hayo, kama kawaida, maandalizi ya safari yakaanza kufanyika ambapo baba aliniambia niulaze ule mwili chini.
Mchakato ulifanyika na kama kawaida, muda mfupi baadaye, akili ilinitoka, nilipokuja kuzinduka, tulikuwa tayari kwenye lile eneo letu tunalokutania, watu wengi wakiwa wamezunguka na kutengeneza duara kama kawaida huku nyimbo za ajabuajabu zikiendelea kuimbwa na kuifanya hali iwe ya kutisha sana.
“Mkuu akikusogelea, inabidi uinamishe kichwa chako chini na kuweka mikono hivi maana umefanya makosa,” baba aliniambia kwa sauti ya chini, akinielekeza nini cha kufanya. Kwa mbali nikawa namuona Mkuu akija huku kama kawaida yake, vishindo vyake vikisikika eneo lote hilo.
Baba na baba Rahma walimsogelea na kuinamisha vichwa vyao kwa utii, akawa anawagusa na mkia wa mnyama ambaye simjui, aliokuwa ameushika, harakaharaka wakaondoka na kwenda kukaa kule walikokuwa wamekaa wale watu wengine.
Mkuu akanisogelea mpaka pale nilipokuwa nimepiga magoti huku uso wake akiwa ameukunja, nilipomtazama mara moja sikurudia tena kumtazama kwa sababu alikuwa anatisha sana. Nilizoea kumtazama akiwa hajakasirika lakini siku hiyo alikuwa kama mnyama mkali wa porini kwa jinsi alivyokuwa anatisha, midomo ikimchezacheza kwa hasira.
Ilibidi niinamishe kichwa kama baba alivyonifundisha, mikono nikaiweka kifuani kwa unyenyekevu, aliendelea kunitazama bila kusema chochote kwa sekunde kadhaa kisha nikasikia akinipigapiga na ule mkia.
“Sirudie masiku mengine,” alisema Mkuu kwa Kiswahili kibovu huku akiendelea kunipigapiga, kidogo kamoyo kalitulia ila nilichojifunza ni kwamba kumbe nilikuwa nimefanya kosa kubwa sana na pengine bila kufanya kile tulichokifanya kwa msaada wa baba na baba yake Rahma, huenda huo ndiyo ungekuwa mwisho wangu.
Kumbe ndiyo maana ni rahisi sana kusikia wachawi wamekufa ghafla vifo vya kutatanisha, wakati mwingine inakuwa ni kukosea masharti kama kilichotaka kunitokea mimi na adhabu inayomfaa mtu anayekiuka masharti, ni kuuawa na kuliwa nyama, kama siyo yeye basi mtu wake wa karibu.
Baada ya kupitisha msamaha kwangu, niliinua uso wangu, mkuu akaugeukia ule mzigo niliokuwa nao ambapo kwa kutumia kisu kikali alikata ile sanda kisha akanigeukia na kutingisha kichwa, akainua ule mkia wake juu na watu wote wakapaza sauti zao kutamka maneno ambayo hata sikuwa nayaelewa.
Basi kilichoendelea hapo ni utaratibu wa kawaida, watu wakala na kucheza ngoma huku mara kwa mara Mkuu akinikata jicho kama anayenichunga kuhakikisha siharibu kitu kingine.
“Amefurahishwa na kazi uliyoifanya, amesema anataka kukuongeza nguvu maana japikuwa umefanya makosa, lakini kupitia makosa hayo umeweza kuonesha ushujaa ambao wengine huwa wanashindwa, mshukuru sana baba yako,” baba Rahma aliniambia kwa sauti ya chini, nikageuka kumtazama Mkuu, macho yake na yangu yakagongana, nikamuona akiachia tabasamu hafifu.
“Akikupa nafasi ya kuchagua akuongezee uwezo gani utachagua nini?”
“Nataka niwe na uwezo wa kupata hela kirahisi, nataka kuwa tajiri.”
“Tajiri? Utajiri wa kichawi ni mbaya sana, jaribu uone mwenyewe, bora hata uombe kitu kingine chochote,” alisema baba yake Rahma lakini maneno yake wala hayakuwa yakiniingia akilini. Kiukweli na mimi nilikuwa natamani kuwa tajiri kwa sababu tangu nizaliwe, maisha yetu yalikuwa ya kimaskini kule kijijini na umuhimu hasa wa kuwa tajiri, niliuona baada ya kufika mjini.
Vijana wadogo tu kama mimi, wengine hata nawazidi lakini wanaendesha magari ya kifahari barabarani, kwa nini na mimi nisionje kidogo hata kama ni mbaya? Wakati akiendelea kunipa nasaha zake, Mkuu alinipa ishara kwamba nimfuate, harakaharaka nikainuka na kumuacha baba yake Rahma akiendelea kuongea.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya>>>Simulizi za Majonzi kusoma mwendelezo.

Loading...

Toa comment