The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 60

ILIPOISHIA:

Vijana wadogo tu kama mimi, wengine hata nawazidi lakini wanaendesha magari ya kifahari barabarani, kwa nini na mimi nisionje kidogo hata kama ni mbaya? Wakati akiendelea kunipa nasaha zake, Mkuu alinipa ishara kwamba nimfuate, harakaharaka nikainuka na kumuacha baba yake Rahma akiendelea kuongea.

SASA ENDELEA…

Alinishika mkono na kusogea pembeni na mimi, mawasiliano kati yetu kidogo yalikuwa magumu kwa sababu alikuwa akiongea maneno ya Kiswahili machache, tena yaliyopindapinda lakini muda mwingi alikuwa akizungumza lugha ambayo siielewi.

Katika yale machache niliyomuelewa, alionesha kufurahishwa na ujasiri wangu, na kuniambia kwamba japokuwa ndiyo kwanza nilikuwa nimejiunga, nilikuwa na kasi nzuri ya kujifunza. Kama alivyoniambia baba yake Rahma, kweli Mkuu aliniuliza ni zawadi gani akinipa nitafurahi?

Sikupepesa macho wala kumung’unya maneno, nikamwambia kwamba nataka dawa za kunifanya niwe tajiri. Alicheka sana, mapengo yake yakawa yanaonekana, ni hapo ndipo nikagundua kwamba kumbe naye huwa anacheka na kufurahi, ingawa sikuelewa nini hasa kilichomfurahisha.

 

Aliniambia kitu nilichokichagua ni kikubwa sana kuliko uwezo wangu, akaniambia atanipa dawa lakini haitakuwa ya kupata utajiri mkubwa kwa sababu utajiri una masharti magumu na nikipata pesa nikiwa bado mdogo, naweza kufa siku si zangu.

Tulirudi pale katikati alipokuwa ameweka vifaa vyake, akatoa kimkoba chake cha ngozi na kutoa kichupa kilichokuwa na dawa, akatoa na wembe kisha akaniambia nimfuate. Tulitoka pale na kupotelea vichakani kwenye giza, nikiwa namfuata nyumanyuma.

Tulitokezea kwenye eneo ambalo lina uwazi, akanielekeza kwa ishara kwamba nivue shati kisha nikae chini na kukunja miguu, kweli nilifanya hivyo, akanishika kichwani na kuanza kuzungumza maneno nisiyoyaelewa, akayaongea kwa muda mrefu kisha akachukua ule wembe na kuanza kunichanja chale kuanzia kwenye utosi kurudi mgongoni.

Aliponipaka ile dawa, nilisikia maumivu makali sana lakini nikajikaza kisabuni, alipomaliza, aliniambia nitulie hivyohivyo, akapotelea vichakani. Muda mfupi baadaye, aliibuka kutoka vichakani akiwa amembeba nyoka mkubwa, nikashtuka sana na kutaka kusimama nitimue mbio lakini akanionesha ishara kwamba nitulie.

Huku nikitetemeka kuliko kawaida, alimsogeza yule nyoka mkubwa kwenye zile chale, akawa anamlambisha damu zangu huku akiendelea kuzungumza maneno nisiyoyaelewa. Alipomaliza, aliamuachia, yule nyoka akatambaa kwa kasi na kupotelea vichakani.

Mshangao niliokuwa nao, ulikuwa hauelezeki. Akanipa ishara kwamba nisimame, nikafanya hivyo na kuvaa shati langu kisha tukarudi kule walipokuwa wenzetu, akaniambia kwamba baada ya siku saba dawa itaanza kufanya kazi lakini natakiwa kuwa naenda kutoa sadaka kwa yule nyoka mara kwa mara.

Baba alikuwa akifuatilia kila kilichokuwa kikiendelea na Mkuu alipomaliza tu kuzungumza na mimi, harakaharaka baba alinifuata. Ile furaha yote niliyokuwa nayo ndani ya moyo wangu ilitibuka kwani baba alipofika tu, alianza kunifokea kwa sauti ya chinichini na kuniambia kwamba nilichokifanya ni upumbavu wa hali ya juu na yeye hatahusika na chochote kitakachonipata nitakapokosea masharti.

“Masharti gani tena baba?” nilimuuliza kwa mshangao kwa sababu Mkuu hakuwa amenipa masharti yoyote, akaniambia kwamba siyo kwamba yeye hatamani utajiri lakini masharti yake yalivyo magumu, ndiyo maana wengi walikuwa wanaona ni bora waendelee kuishi kimaskini tu.

“Kama hajakwambia basi mimi nakwambia, kuna masharti magumu sana tena usipokuwa makini unaweza kusababisha hata sisi wazazi wako na ndugu zako wa tumbo moja wakawa kwenye hatari kubwa sana, kwa nini hukuuliza kabla?” baba aliendelea kuniwakia kwa sauti ya chini huku mara kwa mara akigeuka na kumtazama Mkuu. Nadhani alikuwa hataki asikie chochote.

Maelezo aliyonipa baba yaliniogopesha sana, japokuwa hakuwa amenifafanulia, ilivyoonesha kulikuwa na masharti magumu kwa sababu hata mimi siku nyingi nilikuwa najiuliza, kwamba kwa nini unakuta mganga anasaidia watu kupata utajiri kwa njia za kishirikina wakati yeye anaishi kwenye kijumba cha nyasi?

Nilikuwa pia najiuliza kwa nini wachawi wengi wanakuwa na maisha ya dhiki sana? Nilitamani kuyajua hayo masharti kwa sababu kama ni maji, yalishamwagika. Baba aliniambia hawezi kuniambia, kama nataka nirudi kwa Mkuu kwenda kumuuliza.

Ile furaha yote niliyokuwa nayo moyoni iliyeyuka, kurudi kwa Mkuu kumuuliza nikashindwa kwani muda nao ulikuwa umeenda sana. Nikiwa bado nimetulilia nikitafakari, yule msichana, Isrina alinifuata, hata sijui alitokea wapi, nilishtukia tu yupo pembeni yangu.

“Hongera,” alisema huku akinipa mkono, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake, nilimpa mkono lakini sikuwa nimechangamka.

“Mbona siku hizi huna taimu na mimi? Kuna jambo nimekuudhi?” aliniuliza, nikatingishwa kichwa kukataa lakini ukweli ni kwamba nilikuwa na kinyongo kikali sana dhidi yake.

“Basi nitakutafuta tuzungumze, nakuomba ukubali,” alisema huku akiinuka, nikatingisha kichwa kwa sababu nilikuwa nataka aondoke haraka.

Mpaka muda wa kutawanyika unafika, bado nilikuwa sielewi nini itakuwa hatma yangu na nifanye nini kwa wakati huo. Tulirudi nyumbani kama kawaida ambapo nilijipa muda wa kutafakari mambo yote yaliyotokea kwa siku hiyo maana kiukweli kwenye ulimwengu wa giza, dunia inakwenda kasi sana kuliko unavyoweza kudhani. Kutokana na uchovu niliokuwa nao, nilipitiwa na usingizi mzito, nikiwa na maswali mengi ndani ya kichwa changu ambayo yote hayakuwa na majibu.

Kesho yake nilichelewa sana kuamka kwa sababu ya uchovu, nilipoamka, majira kama ya saa nne hivi, nilimfuata baba yake Rahma nikitaka ufafanuzi zaidi. Tulizungumza mambo mengi lakini kubwa aliniambia utajiri wa kishirikina, huwa unahitaji makafara ya damu mara kwa mara.

Akaniambia kwamba bahati mbaya ni kwamba, sina uwezo wa kuchagua nani atolewe kafara muda wa kufanya hivyo unapofika bali nitakuwa nachaguliwa, kwa hiyo natakiwa kuwa makini sana.

Maelezo hayo yalinitisha sana, nikawa najaribu kuunganisha matukio, ni kweli watu wenye utajiri wa kishirikina, huwa wanasumbuliwa sana na kashfa ya kuwatoa kafara watoto wao, wazazi wao au watu wao wa karibu.

Nilijaribu kujitazama kwa upande wangu, nikawafikiria wazazi wangu na ndugu zangu tuliozaliwa nao tumbo moja, nikawa najiuliza kama siku nitatakiwa kumtoa yeyote kafara nitaweza kweli? Ulikuwa ni mtihani mgumu sana kwangu.

Ila aliniambia jambo ambalo kidogo lilinipa faraja, akaniambia kwamba makafara yanakuwa ni lazima pale utajiri unapokuwa mkubwa sana, lakini kwa mambo ya fedha ndogondogo hakuna ulazima wa kufanya kafara lolote.

Maelezo hayo yalinifurahisha sana ndani ya moyo wangu, nikawa nasubiri kwa hamu hizo siku saba ziishe nikapewe maelekezo ya nini cha kufanya. Nilichojiapiza ni kwamba sitataka utajiri mkubwa, fedha ndogondogo tu za kutesea mitaani zilikuwa zinanitosha sana, hasa ukizingatia kwamba sikuwa na majukumu ya moja kwa moja.

Wakati nikiendelea kusubiri hizo siku saba, niliona huo ndiyo muda muafaka wa kuanza kushughulikia suala la Rahma. Kama nilivyoeleza, kuna ukuta mkubwa ulikuwa umejengeka kati yetu, na kama nisingefanya jambo, huenda huo ndiyo ungekuwa mwisho wetu, jambo ambalo lilikuwa likituumiza sana sote wawili, hasa Rahma.

Alikuwa hanielewi kwa nini nimebadilika ghafla, nimekuwa na mambo mengi ya ajabuajabu, sioneshi kumhitaji tena kama siku za mwanzo na wala sijali hisia zake. Ukweli ni kwamba nilikuwa namlinda na ndiyo maana ilikuwa lazima nifanye hivyo na njia pekee, ilikuwa ni kumshawishi naye ajiunge nasi, kazi ambayo isingekuwa nyepesi lakini nilishajipanga kumkabili.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya>>>Simulizi za Majonzi kusoma mwendelezo..


Loading...

Toa comment