The House of Favourite Newspapers

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 61

ILIPOISHIA:

Alikuwa hanielewi kwa nini nimebadilika ghafla, nimekuwa na mambo mengi ya ajabuajabu, sioneshi kumhitaji tena kama siku za mwanzo na wala sijali hisia zake. Ukweli ni kwamba nilikuwa namlinda na ndiyo maana ilikuwa lazima nifanye hivyo na njia pekee, ilikuwa ni kumshawishi naye ajiunge nasi, kazi ambayo isingekuwa nyepesi lakini nilishajipanga kumkabili.

 SASA ENDELEA…

“Rahma!” nilimuita msichana huyo baada ya kukutana naye koridoni, mimi nikitoka bafuni kuoga na yeye akitoka chumbani kwake. Tofauti na siku zote ambazo alikuwa akinichangamkia sana anaponiona, wakati mwingine hata akinifuata chumbani kwangu, siku hiyo Rahma alikuwa tofauti kabisa, alipooza na alionesha kutotaka kuzungumza chochote na mimi.

“Rahma si nakuita jamani,” nilisema baada ya kumuona amenipa mgongo, akitembea haraka kuelekea sebuleni. Licha ya kutamka maneno hayo, bado hakutaka kusimama, ikabidi nitumia nguvu kumshika mkono na kumgeuza.

“Samahani nina mazungumzo na wewe, naomba unisikilize tafadhali,” nilimwambia kwa upole, akanitazama usoni, macho yake na yangu yakagongana, nikashtuka kumuona akilia.

“Unalia nini Rahma?” nilimuuliza lakini hakunijibu kitu zaidi ya kuendelea kunitazama kwa huzuni. Ilibidi nianze kumbembeleza lakini kwa kuwa tulikuwa tumesimama koridoni, niliona haiwezi kuwa picha nzuri kwani mtu yeyote angetuona tukibembelezana hapo angeweza kutufikiria vibaya.

“Naomba tutoke tukanywe japo soda pale dukani, nina mazungumzo ya muhimu sana na wewe,” nilimwambia Rahma, akatingisha kichwa bila kunijibu chochote kisha akarudi chumbani kwake.

Ilibidi na mimi nirudi chumbani kwangu, nikachukua nauli iliyokuwa imebaki siku nilipoenda Mlandizi na kuitia mfukoni, nikajiweka vizuri na kutoka nje. Nilizugazuga pale nje, nilipoona hakuna anayenifuatilia, nilifungua geti kubwa na kutoka nje. Ile kutoka tu, madereva Bajaj na bodaboda waliokuwa wanapaki pale nje, waliacha kila walichokuwa wanakifanya na kuanza kunitazama.

Kibaya ni kwamba upande ule waliokuwa wakipaki, kwa mbele kidogo ndiyo kulikuwa na duka ambalo nilipanga tukae pale na Rahma kwa sababu kulikuwa na viti upande wa nyuma, kwa hiyo ilikuwa ni lazima niwapite palepale walipopaki.

Nimewahi kusikia matukio kadhaa ya madereva hao wa Bajaj na bodaboda kushirikiana kufanya uhalifu, hasa pale inapoonekana mmoja wao ameonewa, nikajua lazima watakuwa wamenipania kwa jinsi nilivyomsulubu mwenzao. Hata hivyo, kwa sababu nilikuwa na nguvu za giza, tena za kutosha kabisa, sikuogopa chochote, ndiyo kwanza nikawa napiga mluzi huku nikielekea kule walikokuwa.

Cha ajabu, nilishangaa kuona kila mmoja akikimbilia kwenye chombo chake na kukiwasha, wakaanza kuondoka mmoja baada ya mwingine wakikimbia kwa kasi, sekunde chache baadaye eneo lote likawa tupu.

Hakukuwa na mashaka kwamba walikuwa wakinikimbia mimi, kwa sababu hata kama wanawahi abiria, wasingeweza kuondoka wote kwa mkupuo, tena kwa kasi kubwa wengine wakinusurika kugongana wao kwa wao.

Sikuelewa nini kimetokea mpaka wawe wananiogopa kiasi hicho lakini sikuwajali maana na mimi nilikuwa na majanga yangu mengi kichwani. Nilienda mpaka pale dukani, nikamsalimia muuza duka ambaye aliponiona tu, alishtuka sana, akaitikia kwa woga.

“Naomba Fanta,” nilisema huku nikimeza mate kwani mara ya mwisho kunywa soda, ilikuwa ni siku ile tuliposafiri kuja jijini Dar es Salaam.”

“Hatuuzi soda hapa!” alisema yule muuzaji, kauli ambayo nilishindwa kuielewa ina maana gani. Juu ya meza kulikuwa na chupa tupu za soda kuonesha kwambamuda si mrefu kuna watu walikuwa wakinywa soda, na mara kadhaa nilipita pale na kuona watu wakipata vinywaji, kwa nini aniambie kwamba hawauzi soda?

Nikiwa bado nimeduwaa, nikishindwa nimuulizeje, mara Rahma aliwasili, kumbe hatukuwa tumeachana umbali mrefu, akamsalimia yule muuzaji. Alimuita kwa jina lake na ilionesha wanafahamiana.

“Kumbe anaitwa Vero,” nilijisemea moyoni, alikuwa mwanamke ambaye kwa kumkadiria alionesha kuwa bado mdogo lakini mwenye uso uliokomaa na kupoteza nuru kama walivyo wanawake wengi wa vijijini kama kule kwetu Chunya.

“Huyu ni kaka yangu, unamjua? Anaitwa Togo,” Rahma alisema huku akinishika begani, nikamuona yule mwanamke akijaribu kuvaa tabasamu la uongo usoni.

“Tuletee soda, Togo unakunywa nini?” alisema Rahma, yule mwanamke akawa anababaika, kama anayeshindwa ajibu nini maana mimi aliniambia hawauzi soda. Rahma alinishika mkono huku akionesha kabisa kwamba anailazimisha furaha, tukaenda mpaka kwenye viti na kukaa, tukawa tunatazamana huku tukisubiri yule mwanamke aje atuhutubie.

“Unataka kuniambia nini?” alisema Rahma huku akikwepesha macho yake pembeni.

“Rahma! Najua unanifikiria vibaya sana kwa sasa, najua unaona kama nakufanyia makusudi kwa sababu sikupendi lakini ukweli ni kwamba ni matatizo makubwa sana na badala ya kunichukia, unatakiwa unionee huruma mwenzio,” nilianza kumbembeleza Rahma.

Kama nilivyosema awali, sikuw anajua mambo ya mapenzi kwa hiyo hata kubembeleza kwangu, nilikuwa naungaunga tu ilimradi Rahma anielewe. Niliendelea kushuka mistari kwa kuzunguka, nikamwambia kuna jambo zito ambalo halijui nataka kumweleza.

Maneno yangu yalimbadilisha kabisa Rahma, akawa ananitazama kwa shauku huku ile huzuni aliyokuwa nayo, ikiyeyuka ghafla. Ili kumuweka sawa, ilibidi nibadilishe mada kwanza, nikamuuliza vipi yule muuzaji mbona haleti hizo soda?

“Una kiu? Ngoja nimfuate,” alisema huku akiinuka lakini alipofika pale dukani, yule mhudumu alikataa katakata kutoka, akampa Rahma funguo ya friji na kutaka ajihudumie mwenyewe. Rahma aliichukua, akaniuliza nakunywa soda gani, akatoambili pamoja na yake, akaja mpaka pale tulipokuwa tumekaa, akazifungua zote na kurudisha funguo kwa mwenyewe.

“Kwa nini amekataa kuja kutuhudumia mwenyewe?”

“Hata mimi nashangaa! Achana naye tuendelee na yetu,” alisema Rahma, nikapiga funda moja kisha nikaendelea kuzungumza. Lengo langu lilikuwa ni kumpasulia ukweli kwamba baba yake alikuwa mwanachama wa jamii ya siri, vilevile baba yangu na mimi pia wameniingiza bila ridhaa yangu.

Niliona hiyo ndiyo gia nzuri ya kumuingia kwa sababu kama ningesema mimi mwenyewe ndiye niliyetaka kujiunga, angenishangaa sana na pengine nisingeweza kumshawishi. Nilianza kwa kumdadisi kwa kina kuhusu baba yake, nikitafuta sehemu ya kuanzia.

“Mbona unaniuliza kama una kitu unataka kuniambia? Tatizo langu wala halimhusu baba, ni mimi na wewe.”

“Ni stori ndefu Rahma ila naomba unielewe nitakachokwambia,” nilisema, nikashusha pumzi ndefu na kuamua liwalo na liwe. Nilitaka kwenda moja kwa moja, kwamba baba yake na baba yangu walikuwa wachawi. Cha ajabu, kila nilipotaka kusema hivyo, mdomo ulikuwa mzito, nikawa naumauma maneno, hali iliyosababisha anikazie macho.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue au bofya>>>Simulizi za Majonzi kusoma mwendelezo.

Comments are closed.