BAADA ya ushindi wa michezo mitano mfululizo ya Ligi Kuu Bara, wadhamini wa Yanga ambao Kampuni ya GSM jana jioni walitarajiwa kuvamia kambi ya timu hiyo kwa ajili ya kuwapa bonasi ya Sh 50Mil.GSM, kwenye msimu uliopita ilikuwa ikitoa Sh 10Mil katika kila mchezo wa ligi.
Waliokuwa wakishinda kabla ya msimu huu kuja kivingine katika utoaji wa bonasi kwa wachezaji wake.Yanga hadi hivi sasa imecheza michezo sita kati ya hiyo mmoja wametoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Prisons huku mingine wakishinda walipocheza na Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Mbeya City, Polisi Tanzania na Coastal Union.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, wachezaji hao walitarajiwa kupewa bonasi ya ushindi wa michezo mitano jana jioni mara baada ya mazoezi yanayoendelea kwenye kambi ya timu hiyo iliyoweka kwenye eneo la Avic Town, Kigamboni.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, bonasi hiyo ni sehemu ya muendelezo wa ahadi ya wadhamini Yanga ambao ni GSM kwa wachezaji kuwapa bonasi kama motisha ya kuongeza pointi tatu tatu katika kila mchezo.
“Wachezaji wa Yanga wameandaliwa sapraizi ya kutosha na wadhamini wetu GSM ambao leo (jana) jioni wanatarajiwa kupewa bonasi ya Sh 50Mil wachezaji baada ya ushindi wa michezo mitano mfululizo ya ligi.
“Hiyo yote katika kuhakikisha wanarejesha morali ya wachezaji kujituma na kuendelea kupambana ili kuhakikisha wanaendelea kushinda michezo ijayo ya ligi,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumza hilo Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said, alisema: “Msimu huu tumekuja na utaratibu mzuri wa utoaji wa bonasi kwa wachezaji wetu na kikubwa tumepanga kuwapa bonasi kwa ushindi wa mfululizo na siyo mmoja mmoja kama ilivyokuwa msimu uliopita.
“Hivyo tumewapanga kuwapatia bonasi hiyo wachezaji wetu baada ya ushindi wa michezo mitano mfululizo ambayo ni siri kati ya wadhamini na wachezaji.”
Wilbert Molandi,Dar es Salaam