‘Hackers’ wazuia mashambulizi ya ISIS nchini Italia

ISIS-militantsMagaidi wa ISIS

Rome, Italia
Kundi la wadukuzi wa mtandaoni (Online Hackers) linalojiita Anonymous, limefanikiwa kuzima shambulizi la kigaidi la kundi la ISIS baada ya kuvamia akaunti zao za mitandao ya kijamii kisha kuwataarifu polisi na wahusika wa eneo shambulio hilo lilipokuwa limepangwa kufanyika.
Kwa mujibu wa Anonymous, shambulio hilo lilipangwa kufanyika Jumatatu, Desemba 28, mwaka huu lakini wakafanikiwa kunasa taarifa za magaidi hao wakati wakipanga mipango yao kisha kuivuruga.
“Tumefanikiwa kuzima shambulio moja la kigaidi nchini Italia leo, tunaamini tutazuia mengine,” Anonymous waliliambia Gazeti la The Independent.
Anonymous walitangaza kuingia kwenye vita ya kimtandao na Kundi la ISIS baada ya mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea jijini Paris, Ufaransa na kusababisha vifo vya watu 130, mwezi Novemba.
Kundi hilo liliachia video yake mtandaoni likieleza kuwa litatumia teknolojia ya mawasiliano ya intaneti, kuwasaka wahusika wa shambulio hilo, kuvamia mawasiliano yao, kuzifunga akaunti za magaidi mtandaoni na kuwakamatisha kwa polisi kwa lengo la kuwavuruga ili waache kuua watu wasio na hatia.
Siku chache baadaye, Anonymous waliposti mitandaoni taarifa kwamba wamenasa mawasiliano ya siri ya ISIS wakipanga kufanya mashambulizi Marekani, Indonesia, Italia na Lebanon na wakafanikisha kuzima mashambulizi hayo.
“Lengo letu ni kuifanya dunia, au kundi fulani la watu kujua kwamba eneo fulani limewekwa kwenye ‘target’ ya kushambuliwa ili hata kama mtu anaamua kwenda, awe anajua mapema,” ulisomeka ujumbe kwenye akaunti ya Anonymous na kuongeza kuwa changamoto kubwa wanayoipata, ni watu kupuuza taarifa wanazozitoa.
“Hatuhitaji kuaminiwa, cha msingi ni kuhakikisha hakuna mtu mwingine anayeuawa na magaidi,” liliposti kundi hilo kwenye akaunti yao ya mtandao wa Twitter.

Loading...

Toa comment