The House of Favourite Newspapers

Hadithi: Insane (Mwendawazimu -01)

Mtunzi: Nyemo Chilongani

“Kwanza anza kuutoa huo mlango, mafuta yameanza kumwagika, gari linaweza kulipuka nakwambia,” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja.

“Ndiyo najitahidi, mlango mgumu sana kung’oka…”

“Basi kama vipi vunja kioo. Tufanye haraka, hii petroli bwana, isije kulipuka,” alisikika jamaa huyo.

“Sawa! Ila wengine nendeni upande mwingine basi tuyaokoe maisha ya hawa watu,” alisema jamaa mwingine.

Gari zuri, la kifahari, Range SUV lililokuwa na gharama ya zaidi ya shilingi milioni mia moja lilikuwa limepata ajali katika Barabara ya Ali Hassani Mwinyi maeneo ya Kinondoni, matairi yaliangalia juu, gari lilibondeka, vioo vilivunjika na kupinduka, chini ikawa juu na juu kuwa chini.

Kila mtu aliyeiona ajali hiyo, hakuamini, ilikuwa ajali mbaya, hakukuwa na mtu aliyeamini kama wangekuta mtu ndani ya gari hilo akiwa salama kabisa, ajali hiyo ilitisha, kila mtu aliyeiangalia, alishikwa kichwa chake.

Watu walizidi kusogea eneo la tukio, baada ya kusikia kwamba mafuta yalikuwa yakitoka katika tenki lake, wakaanza kupiga hatua nyuma, kila mmoja aliyapenda maisha yake, hakukuwa na mtu aliyekuwa tayari kufa.

Wanaume wanne walikuwa wakihangaika kuwatoa watu waliokuwa ndani ya gari hilo. Hakukuwa na mtu aliyejua hao walikuwa wakina nani, walitaka kuwasaidia kama Watanzania wenzao, wenye upendo ambao nao wangeweza kusaidiwa kama tu wangekuwa katika hali hiyo.

Ndani ya gari hilo kulikuwa na watu wawili, mwanaume mmoja, aliyeonekana kuwa kijana wa miaka thelathini na msichana mmoja mrembo. Wote walikuwa kimya, hakukuwa na aliyekuwa akitingishika, kama walivyokuwa wakati gari likipata ajali ya kugongwa na lori, wakabaki vilevile huku wakiwa wamejifunga mikanda.

“Jamani mbona wengine mmesimama tu! Tusaidieni,” alisema jamaa mmoja huku akiwaangalia wanaume wengine waliokuwa wamesimama tu huku wakiwa wamevishika viuno vyao.

Huo haukuwa muda wa kutazamana, walichokifanya ni kuanza kufanya harakati za kuwatoa watu hao waliokuwa garini. Haikuwa kazi nyepesi hata kidogo, ilikuwa kazi ngumu na nzito ambayo iliwachukua dakika kumi mpaka kufanikiwa kuwatoa wote.

Miili yao ilitapakaa damu kutokana na vioo vilivyopasuka kuwachanachana. Nyuso zao hazikuonekana vizuri lakini mwanaume alikuwa amevalia miwani iliyokuwa imepasuka upande mmoja.

Hawakutaka kuwachunguza sana, walichokifanya ni kuwabeba katika gari jingine na kuondoka nao kuelekea hospitalini. Kwa muonekano, walionekana kama tayari walifariki dunia lakini kilichowatia moyo watu kuhisi kwamba watu hao walikuwa wazima ni namba mioyo yao ilivyokuwa ikidunda japo kwa mbali.

“Ni wazima hawa…cha msingi ni kuwahi hospitalini,” alisema jamaa mmoja.

Hawakuchukua muda mrefu wakawa wamekwishafika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapom machela ikaletwa na watu hao kupakizwa na kuanza kusukumwa kuelekea katika chumba cha upasuaji.

Hakukuwa na mtu aliyewatambua watu hao, nyuso zao zililowanishwa na damu zilizosababishwa na vioo vilivyowakatakata nyuso zao, hawakuwa na fahamu, maneso waliendelea kuzisukuma machela zile mpaka katika chumba hicho kilichoandikwa ‘Theatre’ kwa juu.

Huko, kazi kubwa ilikuwa ni kuwafanyia upasuaji mdogo kwa kuwaosha sura zao na hata kuwatibu vile vidonda walivyokuwa navyo, kuwawekea mashine za oksijeni na kuwatundikia dripu.

Kazi hizo zote zilifanyika kwa pamoja. Baada ya kila kitu kufanyika na miili yao kuoshwa, hakukuwa na mtu aliyeamini kwamba mwanaume aliyekuwa amepata ajali hiyo alikuwa Edson Makumila, bilionea kijana mwenye umri wa miaka thelathini na mbili ambaye alikuwa akitisha kwa utajiri kipindi hicho.

“Edson…” alijikuta akiita dokta huku akishangaa.

“Kumbe ni bilionea! Mungu wangu!” alidakika nesi mmoja. Walimfahamu mwanaume huyo, alijulikana kila kona kutokana na utajiri wake mkubwa uliomfanya kuwa kijana mwenye utajiri mkubwa kuliko wote barani Afrika.

“Jamani! Na yule mwanamke ni mkewe?”

“Hapana! Yule ni muigizaji, Stela John, yule wa Bongo Muvi.”
“Unasemaje?”
“Ni Stela wa Bongo Muvi!”
“Haiwezekani kabisa. Si nilimsikia kwa masikio yangu Edson akikana kuwa na mahusiano ya kimapenzi na huyu msichana, sasa ilikuwaje awe naye ndani ya gari?” aliuliza daktari mmoja.

“Hata mimi mwenyewe nashangaa…hebu tumpigie simu mke wake kwanza,” alishauri daktari mwingine.

Hicho ndicho walichokifanya, harakaharaka simu ikapigwa kwa mkewe ambaye baada ya dakika kadhaa, akawa hospitalini hapo. Moyo wake uliumia, alikuwa akilia kama mtoto, hakuamini alipoambiwa kwamba mume wake alipata ajali akiwa na mwanamke mwingine.

Alimfahamu sana mwanamke huyo, ndiye aliyeleta ugomvi baina yake na mumewe, ndiye aliyemliza kila siku, alimwambia mumewe kuachana na mwanamke huyo lakini hakusikia, ndiyo kwanza alimwambia kwamba hizo zilikuwa skendo za magazeti hivyo hakutakiwa kuziamini.

Mkewe hakutulia, moyo wake uliungua, alihisi ukichomwa na kitu chenye ncha kali, alimpenda sana mume wake, alifunga na kuomba, alimwambia Mungu wazi kwamba alitaka kujua ukweli wa kilichokuwa kikiendelea.

Chozi lake la thamani likadondoka kwa ajili ya mumewe na msichana huyo. Kila alipokuwa akiikutanisha mikono yake na kuanza kuomba, alilitaja jina la mumewe na jina la Stela huku akimwambia Mungu kwamba ukweli ujulikane.

Baada ya maombi hayo ya miezi miwili, ndipo akaja kujua ukweli juu ya kilichokuwa kimetokea, japokuwa mumewe alikataa kila siku lakini mwisho wa siku akapata ajali akiwa na mwanamke huyo ndani ya gari.

Hospitalini hapo alikuwa akilia mfululizo, hakuumia kwa sababu mumewe alikuwa hoi kitandani, aliumia kwa sababu aligundua kwamba mumewe alimdanganya kitu kilichouumiza mno moyo wake.

“Mungu…” alijikuta akiita hivyo, hakuzungumza kitu, akanyamaza na kuendelea kulia kilio kilichojaa kwikwi.

Hakuondoka hospitalini hapo, bado aliendelea kuwa hapo, alimuomba Mungu amponye mume wake, arudiwe na fahamu na kuzungumza tena. Kila madaktari walipokuwa wakitoka ndani ya chumba kile, aliwafuata na kuwauliza juu ya hali aliyokuwa nayo mume wake.

“Anaendeleaje?” alimuuliza daktari.

“Hali yake ni nzuri kidogo japokuwa bado hajarudiwa na fahamu ila tunaendelea kupambana…” alijibu daktari.

“Na vipi kuhusu huyo mwanamke wake?”

“Hali yake ni mbaya sana! Anahitaji maombi zaidi kwani…” alijibu daktari, hakumalizia sentensi yake, akanyamaza.

“Naweza nikaomba kwa ajili yake pamoja nawe ili Mungu akutie nguvu wakati unafanya upasuaji kwa ajili yake?” aliuliza mwanamke huyo
“Hakuna tatizo!”

Alichokifanya ni kuishika mikono ya daktari na kuanza kumuombea Stela ambaye hakuwa akijitambua kitandani. Aliumia sana lakini bado alisikia sauti ikimwambia moyoni mwake kwamba hakutakiwa kuonyesha chuki kwa mtu aliyehisi kuwa adui yake bali alitakiwa kumuombea baraka.

Aliomba kwa uchungu, kila alipolitaja jina la Stela alisikia kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake lakini hakutaka kuacha. Huo ndiyo ulikuwa muda wa kumuombea adui yake kwa mapenzi ya dhati. Maombezi yalichukua dakika moja, akanyamaza na kisha kutulia kwenye benchi.

Kila mtu alibaki akimwangalia, alimuonea huruma kwani kwa jinsi alivyokuwa akilia, alionekana kuwa mtu mwenye maumivu makali moyoni mwake. Alikaa hapo kwenye benchi kwa saa nne ndipo madaktari wakamtoa mumewe katika chumba kile na kumpeleka katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa ajili ya mapumziko.

“Mungu! Naomba umpiganie mume wangu! Naomba umpe uzima, najua madaktari wanahangaika kwa ajili yake. Wao si chochote kile, wewe ndiye daktari wa mwisho mwenye nguvu ya kumponya mume wangu! Naomba ufanye muujiza, naomba umuinue tena kitandani pale alipolala,” alisema mwanamke huyo huku machozi yakiendelea kutiririka mashavuni mwake.

Kila alichokiomba, aliomba akiwa na maumivu makali mno moyoni mwake.

****

Irene Uwoya Afanya Kufuru Birthday Yake, Amkumbuka Samwel Sitta Aliyezaliwa Naye Des. 29

Comments are closed.