The House of Favourite Newspapers

Hadithi: Insane (Mwendawazimu -3)

Ilipoishia Sehemu ya 2

Moyo wake ulimuuma mno, muda mwingi alionekana kuwa na mawazo, hakuamini kama Mungu aliruhusu yeye kupitia katika maisha aliyotakiwa kupitia kipindi hicho. Hakuacha kuomba, hospitalini hapo, kila alipokuwa kwenye benchi, alimuomba Mungu kwa kuamini kwamba kupitia Yeye, hakukuwa na kitu ambacho kingeshindikana.

“Mungu! Najua unajua ni jaribu kubwa kiasi gani napitia. Sijui nifanye nini, ila naomba unipe nguvu ya kusonga mbele,” alisema Rachel huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.

Songa nayo

Hali ndani ya Jiji la Dar es Salaam ilikuwa imetulia, purukushani za watu zilipungua mjini kwa kuwa siku hiyo ilikuwa ni Jumapili tulivu ambayo watu wengi walikwenda ufukweni, kupumzisha akili pamoja na familia zao.
Wengine, katika siku hiyohiyo ndiyo walikuwa wakiitumia kutembelea ndugu na marafiki, wengine huku wakisubiri muda wa kwenda klabu kwa ajili ya kustarehe kutokana na purukushani za kazi nzito katika siku za wiki.

Maeneo ya Posta Mpya, hali ilikuwa ni ya ukimya, hakukuwa na watu wengi maeneo hayo, ofisi na maduka mengi yalifungwa, kwa kifupi, siku hiyo hasa kwa maeneo kama hayo, hakukuwa na idadi kubwa ya watu kabisa kwani hata daladala zilizokuwa zikifika huko, zilipungua, na zile zilizofanya hivyo, basi ziliunganisha mpaka Feri.

Wakati watu wakiwa wamepungua huko, ndiyo muda ambao mwanamke kichaa, aliyekuwa amebeba mfuko uliojaza vitu alivyokuwa ameviokota, alikuwa akitembea mitaani, kila mtu aliyakuwa akimwangalia, alimpuuzia, hakukuwa na mtu aliyekuwa na habari naye.

Kila mtu alimjua mwanamke huyo, inawezekana alikuwa maarufu kuliko mtu yeyote huko Posta, kila mtu aliyemuona, alimshangaa kwani mbali na uwendawazimu wake lakini alikuwa mzuri wa sura.

Hakukuwa na mtu aliyekuwa akimfahamu mwendawazimu huyo, kuna wengine walisema kwamba alifika katika Jiji la Dar es Salaam akitokea Kigoma lakini pia wapo wengine waliosema kwamba mwendawazimu huyo alifika Dar es Salaam miaka mingi iliyopita akitoka Morogoro.

Kazi yake kubwa kila siku ilikuwa ni kuzunguka huku na kule, mkononi mwake alikuwa na fimbo, hakuwa akiwachapa watu, fimbo hiyo aliitumia kwa ajili ya kupekulia uchafu kila alipokuwa kwenye jalala akitafuta chakula au vitu vingine.

Alichosha sana, Halmashauri ya jiji hilo lilijitahidi kumtoa katikati ya mji na kumpeleka pembeni kabisa ya mji lakini kitu cha ajabu kabisa, baada ya kipindi fulani alirudi ndani katikati ya jiji hilo na kuendelea na maisha yake.

Wengi walimpenda, mjini kukawa hakuna utamu kama tu mwendawazimu huyo hakuwepo. Hakukuwa na mtu aliyemjua jina lake halisi ila watu wengi hapo mjini walizoea kumuita kwa jina la Miriam, kutokana na uzuri wake kipindi hicho, watu wakamfananisha na mrembo, Miriam Odemba.

“Hivi huyu ni mwendawazimu kweli?” aliuliza jamaa mmoja, alikuwa akimuuliza mwenzake wakati Miriam alipokuwa akipita mbele yao.

“Ndiyo! Kwa nini umeuliza hivyo?”
“Daah! Huyu mwendawazimu ni mkali ile mbaya. Mwangalie alivyokuwa na furushi kwa nyuma! Angalia sura, daah!” alisema jamaa huyo, kwa kumtazama tu alionekana kumtamani Miriam.

Sura yake iliwapagawisha watu wengi, umbo lake lililojaajaa kwa nyuma liliwatoa udenda wanaume. Akawa stori kila kona, watu wengine kutoka sehemu mbalimbali walipoambiwa kuhusu Miriam, walikwenda mjini na kujionea kwa macho yao.

Kama walivyoambiwa ndivyo walivyomkuta, alikuwa mzuri hasa, kila mmoja alikiri kwamba Miriam alikuwa mwendawazimu aliyekamilika na hawakujua ni sababu gani zilimpelekea kuwa katika hali hiyo.

“Au alikuwa akitembea na mume wa mtu hivyo kurogwa?” aliuliza jamaa mmoja.

“Wewe unasema hivyo! Wengine wanasema alikuwa akimtaka mume wa mtu, yaani kila mtu anasema lake, ila kitu cha kujua ni kwamba Miriam ni mzuri. Mwangalie alivyo! Kweli Mungu hakupi vyote,” alisema jamaa mwingine.

Miriam alikuwa gumzo huko mjini, watu walimpenda, wengine wakamtamani lakini tatizo lilikuwa moja tu, alikuwa mwendawazimu. Hilo likawaweka watu kwenye wakati mgumu, wakati mwingine walitamani hata kumfuata na kuzungumza naye ilimradi tu walale naye lakini hilo likashindikana.

Wanawake waliokuwa wakiringa, mfano mzuri waliopewa ulikuwa wa Miriam, pamoja na urembo wake lakini alikuwa mwendawazimu. Watu walikwishamchukua sana na kumpeleka hospitalini kutibiwa lakini hakupata msaada uliotakiwa kwani alikuwa akitoroka na kurudi mitaani kama kawaida yake.

Mbali na watu wote kumpenda, kulikuwa na jamaa fulani ambaye alikuwa akimpenda zaidi. Huyu aliitwa Boniface Mrope. Alikuwa meneja wa kampuni kubwa ya Amazon Square iliyokuwa hapo Posta ambayo ilishughulika na upokeaji wa mizigo kutoka nje ya nchi.

Alikuwa mtu mwenye pesa nyingi, katika maisha yake alikwishawahi kukutana na wasichana warembo, walioumbika lakini kwa Miriam, aligonga mwamba, hakuhisi kama kulikuwa na msichana mzuri kama alivyokuwa Miriam.

Kazi yake kubwa ilikuwa ni kukaa ofisini kwake, ghorofani dirishani, alipokuwa akichungulia chini, macho yake yalikuwa yakitua kwa Miriam aliyekuwa akikaa sehemu na kuanza kula chakula alichokuwa amekiokota siku hiyo.

Moyo wa Boniface ulimuuma, kila alipomwangalia Miriam Mwendawazimu, alihisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake. Hakutaka kukubali, yeye ndiye aliyekuwa akifanya mchakato wa kumpeleka hospitali kwa kutuma watu lakini alipokuwa akimkumbuka, alikuwa akiwatuma watu haohao kwenda kumtorosha huko hospitalini.

Mapenzi aliyokuwa nayo kwa mwendawazimu huyo yalikuwa siri yake, kila siku alihuzunika moyoni mwake kumuona msichana mrembo kama Miriam akiwa kwenye hali aliyokuwa nayo.

Kumpenda sana Miriam ndipo kukamfanya kutofautiana na mpenzi wake, Jesca. Msichana huyo alimpenda, alikuwa kila kitu kwake lakini baada ya Boniface kuanza kumpapatikia Miriam, mapenzi yakapungua kwa Jesca na mwisho wa siku penzi kuyumba kwa nguvu kubwa.

“Hivi una nini Boniface?” aliuliza Jesca huku akionekana kukasirika.

“Kwani kuna nini?”
“Mbona umebadilika!”

“Nimebadilika! Nipo vipi?”
“Hivi hujioni kweli? Yaani mapenzi umepunguza, au kuna mtu?” aliuliza Jesca.

“Wala hakuna mpenzi! Wasiwasi wako tu!”

Jesca hakutaka kuridhika, alichokifanya ni kuanza kumpeleleza Boniface, alitaka kufahamu kilichokuwa kikiendelea, alitaka kumjua mwanamke aliyemfanya mpenzi wake kutokuwa na muda wa kutosha kwa ajili yake.

Upelelezi wake uliendelea kwa miezi sita, hakubaini kitu chochote kile, hata alipokuwa akishika simu ya Boniface na kuangalia, hakukuwa na meseji chafu, hakukuwa na picha za msichana yeyote na hata wakati mwingine aliichukua simu hiyo na kukaa nayo, bado hakukuwa na msichana aliyekuwa akimsumbua.

“Ila kwa nini amebadilika?” alijiuliza.

Jesca hakutaka kuridhika, alichokifanya ni kuwasiliana na marafiki zake na kuwaambia kilichokuwa kikiendelea. Marafiki hao wakaamua kumsaidia kwa kumpelelezea mpenzi wake, hivyo wakaingia kazini na kuanza kufanya kazi hiyo.

Walitumia miezi mitatu, tena wakati mwingine wakimfuatilia alipokuwa akirudi lakini hawakuambulia kitu. Iliwachanganya, walimwambia Jesca kwamba mpenzi wake, Boniface hakuwa na uhusiano na msichana yeyote lakini msichana huyo hakutaka kukubali kabisa, alichohisi ni kwamba mpenzi wake alikuwa na mtu mwingine.

“Miriam, kwa nini unaniumiza hivi? Hujui ni jinsi gani ninaumia moyoni mwangu, ninakupenda sana, kwa nini nisikuoe hata kama upo katika hali hiyo?” alijiuliza Boniface huku akiwa ofisini kwake.

Alikuwa dirishani huku akichungulia nje. Macho yake yalikuwa yakimwangalia Miriam aliyekuwa amekaa sehemu yake kama kawaida huku akila chakula alichokuwa amekiokota. Alikuwa mchafu, masizi usoni lakini kwa hali hiyohiyo alikuwa akipendwa sana.

“Ni lazima nizae na Miriam, haiwezekani hata kidogo nimuache,” alisema Boniface huku akionekana kumaanisha. Hakutaka kutoa macho yake kwa msichana huyo. Kila alipomwangalia, ndivyo alivyompenda zaidi.

KAMPUNI YA ZANTEL YANUSURIKA KUFILISIWA NA SERIKALI

Comments are closed.