Hadithi ya Eric Shigongo: Dimbwi la Damu-04
ERIC SHIGONGO: DIMBWI LA DAMU-04
GLOBAL PUBLISHERS
Wodini: “Mama maputo yangu! Nipeni maputo yangu twende nyumbani kwenye pati yetu Nicky na watoto wengine wanatusubiri!” Hayo ndiyo maneno aliyoanza kusema Vick aliporudiwa na fahamu zake baada ya siku tano za kuzirai! Ilikuwa ni siku tatu baada ya baba na mama yake kuzikwa.
Pembeni mwa kitanda chake alikuwepo Leah na Nicholaus ambao walielewa ni kitu gani alichokuwa akikisema Vicky! Walilia machozi ya uchungu, kwa sababu Vicky alifungwa bendeji machoni hakuweza kugundua kuwa Nicholaus na Leah walikuwa pembeni mwa kitanda chake, aliendea kuwaita baba na mama yake!
“Mama! Baba! Njooni twende!” Aliendelea kusema Vicky kama mtu aliyekuwa usingizini, maneno hayo yalizidisha uchungu mioyoni mwa Nicholus na Leah na kuwafanya walie zaidi, walipiga magoti na kuanza kusali sala ya baba yetu ulie mbinguni wakimwombea Vicky! Waliona hawakuwa na kimbilio jingine zaidi ya kumuomba Mungu! Hawakutaka kupoteza kila kitu, walitaka angalau Vicky abaki hai na waendelee kuwa naye.
Wakiwa bado wamepiga magoti mlango ulifunguliwa na watu waliingia hadi ndani ya chumba hicho! Hawakuongea kitu mpaka Leah na mtoto Nicholaus waliponyanyuka na kuketi.
“Mnasali dhehebu gani?”
“Sisi?”
“Tunasali Lutherani”
“Ok! Hata mimi ni mlutheri pia”
“Sawa daktari!” Alijibu Leah huku akimpisha daktari amwangalie Vicky ambaye bado aliendelea kuongea maneno mengi.
“Kaanza saa ngapi kuongea hivyo mgonjwa!”
“Hana hata dakika kumi na hata sisi bado hatujaongea nae, tuliposikia anaongea ndipo tulipopiga magoti kumshukuru Mungu!”
“Kweli Mungu ni mwema, Vicky kapona!” Aliongea daktari kwa mshangao hata yeye kumbe hakuwa na matumaini.
“Kweli ataoiba?”
“Atapona ila kitu kimoja tu ………..”
“Macho yakeyameharikika kabisa! Hayafai kutumia tena inavyoonekana kuna vipande vidogo vidogo vya vioo vilimwingia katika macho yake siku ya ajali na kuyapasua kabisa! Hakuna uwezekanao mwingine kumsaidia zaidi ya kuyang’oa macho yake inasikitisha lakini inabdi iwe hivyo!”
“Mungu wangu! Kuyang’oa ina maana Vicky atakuwa kipofu?”
“Hivyo ndivyo itakavyokuwa lakini bi bora awe hai!” Daktari aliongea kwa huzuni.
“Daktari hakuna njia nyingine ya kumsaidia kweli?”
“Nasikitika hakuna !”
“Dada Leah!”
Naam!”
“Kumbe upo? Nicholaus yuko wapi? Baba na mama wako wapi?” aliuliza Vicky.
“Baba na mama waliku…………..!” alitaka kujibu Nicholaus lakini kabla hajamaliza sentensi yake Leah alimziba mdomo wake!
“Wapo nyumbani watakuja baadaye!” Leah alimficha.
******
“Nani kafunga?” Leah aliuliza baada ya kukuta kuna kufuli jipya kwenye mlango wa nyumba yao walipotoka hospitali. Kabla hajapata jibu mtu mmoja alitokea nyuma yake na kuuliza wao ni akina nani.
“Sisi?”
“Ndio!”
“Kwanini unatuuliza?”
“Mimi ni mlinzi mpya nimeletwa hapa na shangazi yenu Christina hamtakiwi kuingia katikanyumba hii!”
“Kwanini?”�”Nyumba hii imechukuliwa na yeye mnatakiwa mtafute mahali pengine pa kuishi!”
Leah alijifanya hakusikia maneno hayo na kuuparamia mlango na kuanza kulivuta kufuli lao, mlinzi alimkamata na kuanza kumzaba vibao vingi usoni.
“Unajifanya kiburi siyo?”
Roho ya Nicholaus iliumia kuona Leah akipigwa bila sababu, alirudi nyuma na kuokota kipande cha jiwe na kulirusha kwa nguvu zake zote likatua usoni kwa mlinzi huyo! Damu iliruka kama bomba kutoka sehemu lilipotua jiwe, mlinzi huyo alianguka chini na kutulia tuli!
Leah na Nicholaus hawakuwa na mahali pa kulala ilibidi wakae nje wakinyweshewa na mvua hadi usiku wa manane! Kifo cha Martin na Hoyce kilionekana kuwa mwisho wa kila kitu.
Mpaka majira ya saa nane �hivi usiku Leah na �Nicholaus walikuwa bado wako nje wakinyeshewa mvua na kupigwa na baridi! Mlinzi alikuwa bado amelala chini lakini ghafla walimwona akinyanyuka na kukaa kitako, kwa mkono wake wa kulia alijishika usoni na kupambana na kidonda pamoja na damu iliyoganda! Leah alishtuka akijua kama mlinzi angewaona ni lazima angewadhuru.
“Twende tukajifiche nyuma ya nyumba Nicky!” Leah alisema na kuanza kumvuta Nicholaus wote wawili wakazunguka nyuma ya nyumba na kuingia ndani ya shimo refu la takataka na kujificha! Wakiwa ndani ya shimo hilo walisikia vishindo vya mtu akitembea kuelekea mahali lilipokuwa shimo hilo, walijua lazima alikuwa amewaona na alikuwa akiwafuata lakini ghafla walisikia vishindo hivyo vikigeuza na kuelekea tena mbele ya nyumba.
“Nikiwakamata ni lazima niue mwenye kwa mkono wangu kabla hata huyo shangazi yao hajaja!” Alisikika akisema mlinzi huyo Leah alizidi kumkumbatia Nicholaus wakiwa ndani ya shimo la takataka lililoendelea kujaa maji ya mvua.
Hali ikawa shwari hawakusikia tena vishindo vya mlinzi lakini mvua ilizidi kunyesha na maji yalizidi kutiririka kuingia ndani ya shimo wasiwasi wa maji kujaa na kuwafunika ulizidi kumwingiea Leah! Nicholaus alitetemeka kwa baridi kiasi cha meno yake kugongana lakini kwa hali iliyokuwepo hakuthubutu kulia kwani hata yeye tayari alishaigundua hali ya hatari iliyokuwepo.
Maisha yao yalikuwa yameharibika ghafla hawakuwahi hata siku moja kufikiri wangekuja kupatwa na shida walizokuwa nazo usiku huo tena wakiwa nje ya nyumba iliyojengwa na baba yao!
Muda mfupi baadaye majira ya kama saa kumi hivi za usiku Leah alisikia lango likifunguliwa na baadaye sauti za watu wakiongea zilifuata, aliposikiliza vizuri aliitambua moja ya sauti hizo! Ilikuwa ni sauti ya shangazi yao ikimuuliza mlinzi ni wapi walikokuwa watoto.
“Walikuja nikawazuia wasiingie ndani ya nyumba lakini yule msichana akataka kuingia kwa nguvu ndipo nikalazimika kumpiga! Lakini kile kitoto kidogo kikanipiga na jiwe hapa puani sijui kilinipiga vipi hata mimi sielewi nikajikuta nimeanguka chini na kupoteza fahamu zangu kabisa! Nilipozinduka nilijaribu kuwatafuta humu ndani lakini sikuwaona!”
“Geti lilikuwa wazi ulipozinduka?”
“Hapana lilikuwa limefungwa kama mlivyolikuta!”
“Sasa wametoka vipi?Nina hakika bado wapo humuhumu ndani hebu watafute mimi nimekuja na hao vijana kuwamaliza kabisa ili hizi mali ziwe zangu moja kwa moja!” Alisema shangazi yao na Leah pamoja na Nicholaus waliyasikia maneno hayo na kuzidi kuogopa.
“Dada Leah,kwanini shangazi anataka kutuua?”
“Inavyoonekana anataka hizi mali zenu!”
Mlinzi alianza kuzunguka nyumba tena akiwatafuta shangazi akiwa nyuma yake mara kwa mara walilikaribia shimo walilojificha Leah na Nicholaus lakini hawakupata wazo na kuangalia ndani yake kwa jinsi mvua ilivyonyesha walikuwa na uhakika kulikuwa na maji hivyo walikata tamaa ya kuwatafuta.
Walikaa ndani ya shimo hilo maji yakiwa yamemfikia Leah kiunoni na Nicholaus shingoni hadi asubuhi bila kugundulika! Walikuwa wakitetemeka sana miili yao, Leah alijua ni lazima Nicholaus angeugua kichomi.
Majira ya kama saa moja hivi walisikia lango likifunguliwa na shangazi pamoja na vijana wanne aliongozana nao waliondoka na kumwacha mlinzi peke yake, Leah na Nicholaus waliendelea kukaa ndani ya shimo hilo hadi saa sita za mchana! walisikia geti likifunguliwa tena na kufungwa wakajua mlinzi alikuwa anatoka kwenda nje, Leah aliamua kuitumia nafasi hiyo kuokoa maisha yao.
“Nicholaus njoo twende!” Alisema Leah na kumpakata Nicholaus wakatoka shimoni na kuanza kutembea kuelekea getini ambako walitoka hadi nje kabla hawajafika mbali walimwona mlinzi akija mbio kuwafuata!
“Nyie mlikuwa wapi?”
“Tulikuwa ndani!”
“Haya twendeni nikawafungulie mlango muingie!” Mlinzi alidanganya lengo lake likiwa kuwarudisha ndani halafu ampigie simu shangazi ili aje na vijana wake kukamilisha mpango wao wa mauaji, kwa sababu walishasikia kila kitu usiku walikataa kurudi.
“Hapana tuna haraka tunakwenda hospitali kumwona mgonjwa!”
“Mtakuja tena jioni? Nimeambiwa na shangazi niwafungulie!”
“Sawa! Tutakuja!” Aliitikia Leah lakini ukweli hakuna mtu ambaye angerudi tena katika nyumba ile hadi mwisho wa maisha yake!
********
Martin na Hoyce waliishi na Leah kwa miaka mitano kabla ya kifo chao walimchukua binti huyo kutoka kwenye kituo cha kulelea watoto cha Msamaria mwema kilichopo katikati ya mji wa Arusha na kuamua kuishi naye baada ya kufikish umri wa miaka kumi na tatu uliokuwa mwisho kwa kituo hicho kulea mtoto Yatima.
Leah hakumjua baba wala mama yake alitupwa mtaani na mama yake baada tu ya kuzaliwa na mama huyo akaondoka kwenda kusikojulikana! Hivyo kwake Martin na Hoyce walikuwa ni kama baba na mama na aliwachukulia Nicky na Vicky kama wadogo zake na aliahidi kuwa na watoto hao hadi hatua ya mwisho!
Walinyoosha hadi hospitali na kwenda katika wodi aliyolazwa Vicky lakini hawakumkuta kwenye kitanda alicholazwa! Leah alishtuka lakini kabla hajafanya lolote au kumuuliza mtu ghafla alishtukia sauti ikimwita kutoka ofisini kwa wauguzi alipogeuka alikutana na sura muuguzi akimwita.
“Naam mama!”
“Hebu njoo hapa kidogo!”
Leah akiwa amemshika Nicky mkono walitembea hadi ofisini kwa wauguzi na kuwasalimia watu wote aliowakuta wodini.
“Wewe ni ndugu yake Victoria?”
“Ndiyo yupo wapi?”
“Walikusubiri sana asubuhi ili utie saini karatasi kabla hajapelekwa chumba cha upasuaji, hivi nyumbani kwenu hakuna watu wazima?”
“Watu wazima?”
“Ndiyo!”
“Wote wamefariki!”
“Wamefariki?”
“Ndiyo kwani wewe hukusikia dada watu waliogongwa na treni juzi?”
“Mh! Nyie ni watoto wa Martin?”
“Ndiyo!”
“Masikini poleeeni!”
“Ahsante!”
Nesi alimueleza Leah sababu ya Vicky kupelekwa chumba cha upasuaji, Leah alilia machozi.
“Vipi mbona unalia?”
“Nashindwa kuelewa nitaishije na hawa watoto!”
“Kwani vipi?”
“Sasa wakiyang’oa macho ya Vicky mimi nitamtunzaje?” Alisema huku akilia kwa sauti kubwa zaidi.
“Dada kwa hiyo Vicky hataona tena?” Nicholaus aliuliza.
“Hapana atakuwa anaona kwa kutumia mashine!”Leah alimdanganya Nicholaus kwa kuogopa kumkatisha tamaa.
*******
Alipotolewa chumba cha upasuaji masaa manne baadaye uso wake wote ulifunikwa na bendeji, lakini alikuwa na fahamu kama kawaida! Leah alishangaa kwani matarajio yake yalikuwa tofauti yeye alitegemea Vicky angerudi akiwa katika mzito wa nusu kaputi.
“Hapana katika operesheni za aina hii huwa hatutoi nusu kaputi bali huwachoma wagonjwa sindano za ganzi katika macho yao!”
Masaa mawili baadaye Vicky alianza kulalamika maumivu katika macho yake ikabidi apewe dawa za kutuliza maumivu pamoja na usingizi.
“Mpeni sindano ya Pethedine 25mg itamsaidia!” alisema daktari na kweli Vicky alipochomwa sindano hiyo alilala usingizi kabisa na kuzinduka saa mbili ya usiku.
“Dada poleeee!” Nicholaus alisema.
“Ahsante!”
Victoria alikaa hospitali pamoja na Leah na kwa muda wa siku saba bila baba yao mdogo wala shangazi yao kufika kuwaona, waliishi maisha ya shida wakila chakula cha hospitali kama wagonjwa wengine, kilikuwa chakula kibaya kikilinganishwa na chakula walichozoea kula nyumbani wakati wa uhai wa wazazi wao mara nyingi Nicholaus alikataa kula na kujikuta akikonda.
Siku ya kumi na mbili waliruhusiwa kutoka wodini, Leah alishindwa kuelewa baada ya kutoka hospitalini angekwenda wapi na watoto hao kwani asingeweza kurudi tena kulikokuwa nyumbani kwao ambako alikuwa na uhakika Nicholaus na Victoria wangeuawa!
Kwa siku tatu mfululizo alilala mitaani mbele ya maduka ya wahindi pamoja na ombaomba wenye Ukoma, usiku mzima yeye na watoto waliwalia wazazi wao, aliwaonea huruma Nicky na Vicky kuliko alivyojionea huruma mwenyewe! Hakuwa na njia nyingine ya kupambana na maisha zaidi ya kuombaomba! Hiyo ndiyo ikawa njia pekee ya kumwezesha yeye na watoto kuishi mjini.
Aliwaeleza watoto ukweli juu ya yaliyotokea na kuwaomba wawe wavumilivu, walichofanya kila siku kikawa ni kupita mitaani katika maduka ya wahindi hasa siku ya ijumaa na kuomba, Victoria akiwa mbele na kopo!
“Hili ni fundisho ni lazima tuwe tunawaandalia watoto wetu mazingira mazuri!”
“Kwanini?”
“Wale watoto niliowapa pesa pale ni watoto wa Martin!”
“Mh! Kweli?”
“Ndiyo! Baada ya kufariki Martin baba yao mdogo na shangazi wamechukua mali zote hivi sasa watoto wanateseka mitaani wao wanatesa na mashati ya marehemu!”
“Masikiniii!” Mke wa bwana huyo alisema kwa huzuni, machozi yalimtoka kwa sababu alimfahamu Martin na utajiri aliokuwa nao ilibidi arudi mbio hadi waliposimama watoto na kuwaogezea noti nyingine ya shilingi elfu kumi!
“Poleni sana watoto Mungu atawasaidia!”
“Ahsante!” Aliitikia Vicky ingawa hakumwona mtu aliyewapa pesa.
Muda mfupi baadaye gari aina ya BMW open roof aliyoitumia Martin kuwapeleka watoto ufukweni kabla ya kifo chake ilipita na Nicholaus akaiona.
“Dada Leah gari ya baba hiyooo!” Nicholaus alisema.
“Sio yenyewe!” Leah alikataa ingawa alimwona hata aliyekuwa akiendesha, alikuwa baba yao mdogo! Hakutaka kuwaumiza watoto.
********
Kwa pesa walizopata katika omba omba kila siku Leah alipanga chumba kimoja maeneo ya Njiro kilikuwa ni chumba kidogo lakini kilitosha na alinunua pia vyombo vya kupikia, jiko na mikeka ya kulalia! Baada ya kupanga chumba alianza kazi ya kulea watoto nyumbani kwa mhindi mmoja mjini Arusha!
Alifanya kazi yake tangu asubuhi hadi saa mbili ya usiku aliporudi nyumbani na kuwapikia watoto chakula cha usiku huo na siku iliyofuata! Maisha yalikuwa magumu lakini alivumilia.
Miaka mitano baadaye:
Pamoja na kupenda shule Vicky na Nicky hawakupelekwa shule na baba mdogo na shangazi walizidi kuponda mali bila kujali kuwa watoto wa ndugu yao walikuwa wakiteseka, watoto wao wakisoma shule za kimataifa nchini Kenya na Uganda! Kila mara Nicholaus alilia shule lakini Leah hakuwa na uwezo wa kumsomesha.
Baadaye Nicholaus akiwa na umri wa miaka kumi na mbili aliandikishwa darasa la kwanza, lakini kwa sababu ya kuanza shule akiwa na umri mkubwa alishindwa kumaliza darasa la saba na kukomea darasa la sita akaanza biashara za kuuza mafuta ya taa mitaani ili kusaidiana na Leah katika maisha yao ya kila siku.
Lakini biashara hiyo haikudumu sana mtaji aliopewa na Leah ulikwisha Nicholaus akajikuta akiwa kijiweni ni huko ndipo alikojifunza tabia chafu! Ni huko ndiko alikoharibika, mazingira yalimlazimisha kuharibika. Alikuwa na shida nyingi na hakuwa na mtu wa kumsaidia au kumsikiliza zaidi ya Leah.
Mara tatu mfululizo alishakwenda nyumbani kwa baba yake mdogo kuomba msaada lakini alifukuzwa kama mbwa! Roho ilimuuma sana ukizingatia mali waliyotumia ilikuwa ya baba yake, aliondoka akilia na kuahidi kutorudi tena.
“Ni bora niondoke hapa nchini vinginevyo nitamuua baba mdogo tena kwa mkono wangu mwenyewe!” Nicholaus alimwambia Leah.
Nicholaus alishajifunza habari za ulaya na Marekani kutoka kijiweni
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumanne hapahapa
Comments are closed.