The House of Favourite Newspapers

Hafsa Kazinja: Waganga Wamenifilisi Nyumba, Magari

0

KARIBU mpenzi msomaji wa kolamu hii ya Yupo Wapi ambayo huwa inakuletea wasanii waliowahi kuwika kisha kuwa kimya ghafla.

Leo tunaye mwanadada Hafsa Kazinja ambaye ngoma yake ya Presha aliyoshirikiana na Banana Zorro ilimpa umaarufu mkubwa.

 

Hafsa mwenyewe anasema ngoma hiyo ilimfanya apate shoo ndani na nje ya Bongo mpaka Uingereza. Msanii huyu anafichua siri kwamba alipotea kwenye ulimwengu wa sanaa kutokana na matatizo ambayo yalimsababisha kuuza nyumba na magari mawili kwa ajili ya waganga wa kienyeji.

 

Unajua ni kwa nini waganga wa kienyeji na ilikuwaje? Ungana na Hafsa hapa chini katika mahojiano aliyofanya na Risasi Mchanganyiko:

Risasi: Hafsa umekuwa kimya sana, mashabiki wako wanapenda kujua uko wapi na unafanya nini kwa sasa?

 

Hafsa: Nipo hapahapa Dar.

Risasi: Unafanya shughuli gani ya kukuingizia kipato?

Hafsa: Nina shughuli nyingi hasa za biashara ingawa sipendi kuziweka wazi, ninachopenda kuweka wazi ni kazi yangu ya uimbaji nyimbo za Injili.

 

Risasi: Sasa hivi umeachana kabisa na muziki wa kidunia na huimbi tena Presha?

Hafsa: Tangu nibadili dini na kuokoka nimekuwa nikishinda kanisani na sitaki hata kuzisikia hizo nyimbo za kidunia.

Risasi: Unaabudu kanisa gani?

 

Hafsa: Naabudu pale KKKT Kimara Korogwe na ndipo nilipopatia wokovu.

Risasi: Nini kilikufanya uokoke?

Hafsa: Ni mapito tu ya kidunia, niliteseka kwa miaka saba nikauza nyumba yangu na magari mawili kwa ajili ya kupata pesa niwape waganga wa kienyeji waweze kumaliza matatizo na maradhi yaliyokuwa yakiniandama.

 

Risasi: Vipi baada ya kuuza hizo mali zako hao waganga waliweza kukutatulia hizo shida zako?

Hafsa: Hakuna kitu kama hicho, hizo pesa walizikomba zote na matatizo ndiyo kwanza yakaongezeka.

Risasi: Ulitafuta suluhisho gani badala yake?

Hafsa: Nilipoamua kuokoka na kuutupa mzigo wa dhambi hilo ndilo likawa suluhisho la matatizo yote yaliyokuwa yakinikabili.

 

Risasi: Maisha yako ya sasa na kipindi ukitamba na Ngoma ya Presha ukisafiri pande mbalimbali unayalinganishaje kiubora?

Hafsa: Maisha ya ndani ya Yesu ni bora zaidi hayana mfano.

Risasi: Mashabiki zako wangependa kujua una nyimbo ngapi za Injili au albamu?

 

Hafsa: Nina albamu moja inaitwa Kwa Yesu Hakuna Presha na kuna albamu nyingine natarajia kuizindua tena hivi karibuni.

Risasi: Vipi kuhusu familia?

 

Hafsa: Hilo huwa sipendi kuliweka bayana sana ila tambua kuwa nina watoto wangu walewale wawili niliowapata nikiwa katika muziki wa kidunia.

Risasi: Sawa Hafsa nakutakia kazi njema.

Hafsa: Asante.

 

“NILIMFANYIA DIAMOND WIMBO BURE, KUHUSU YOUNG D MMH!” – LAMAR

Leave A Reply