The House of Favourite Newspapers

Hakimu Afikishwa Kortini kwa Tuhuma za Kupokea Rushwa Tsh 710,000

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Ukonga jijini Dar es Salaam, Dickson Mwasenga (46), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala na kusomewa mashtaka matatu ya kupokea rushwa ya jumla ya Sh. 710,000.
Akisomewa mashtaka hayo jana na Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo, Devota Mihayo, mbele ya Hakimu Samuel Obasi, ilidaiwa mshtakiwa alipokea rushwa hiyo ili kufanya upendeleo katika kesi ya jinai namba 352 ya mwaka 2017 iliyokuwa inamkabili ofisa wa Benki ya CRDB, Ngomoi Mmbaga (42).
Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa kuwa Februari 22, 2017, mshtakiwa huyo alipokea Sh. 210,000 kutoka kwa Ngomoi Mmbaga kupitia Tigo Pesa ili kumpa upendeleo ofisa huyo wa benki katika kesi ya jinai namba 352 ya mwaka 2017. Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Aprili 14, 2017, mshtakiwa alipokea Sh. 100,000 kutoka kwa Ngomoi Mmbaga, kupitia Tigo Pesa ili kumpa upendeleo ofisa huyo wa benki katika kesi ya jinai namba 352 ya mwaka 2017.
Katika shtaka la tatu, ilidaiwa kuwa Mei Mosi, 2017, mshtakiwa alipokea Sh. 400,000 kutoka kwa Ngomoi Mmbaga kupitia Tigo Pesa ili kumpa upendeleo katika kesi ya jinai namba 352 ya mwaka 2017. Mihayo alidai mahakamani hapo kuwa, kufanya hivyo ni kinyume cha Sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 Kifungu 15(1) ya Mwaka 2017.
Mwendesha mashtaka huyo pia alisoma mashtaka matatu dhidi ya Mmbaga ya kutoa rushwa, ili kupewa upendeleo katika kesi ya jinai namba 352 ya mwaka 2017 katika mahakama hiyo ya mwanzo. Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, Februari 22, 2017, mshtakiwa Ngomoi Mmbaga alituma Sh. 210,000 kwenda kwa Dickson Mwasenga kupitia Tigo Pesa, ili kupewa upendeleo katika kesi ya jinai namba 352 ya mwaka 2017.
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Aprili 14, 2017, mshtakiwa huyo alituma Sh. 100,000 kwenda kwa Dickson Mwasenga kupitia Tigo Pesa, ili kupewa upendeleo katika kesi ya jinai namba 352 ya mwaka 2017. Katika shtaka la tatu, ilidaiwa kuwa Mei Mosi, 2017, mshtakiwa Ngomoi Mmbaga, alituma Sh. 400,000 kwenda kwa Dickson Mwasenga kupitia Tigo Pesa ili kupewa upendeleo katika kesi ya jinai namba 352 ya mwaka 2017.
Mihayo alidai mahakamani hapo kuwa, kwa kufanya hivyo ni kinyume cha Kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2017. Washtakiwa wote walikana mashtaka na kesi hiyo kupangwa kutajwa tena Februari 19, mwaka huu.

KIMENUKA: Halima Mdee ‘AVURUGA’ Bunge “Waziri Acha Upotoshaji” – VIDEO

Comments are closed.