HAKUNA MABADILIKO PASIPO MAUMIVU!

Rais John Pombe Magufuli.

ACHA leo nianze kwa kujinukuu mwenyewe; Maishani tutafanya makosa, Lakini kama tukiendelea kujifunza kutokana na makosa yetu na kubaki kwenye njia yetu, Lazima tutafikia hatma za maisha yetu -Eric Shigongo James,
Mwandishi wa Vitabu.

 

Hiki ndicho kiini cha maandishi yangu ya leo, Novemba 21, 2017, kilichonisukuma kuandika maneno haya leo hii ni kile kinachoendelea nchini mwangu na kelele nyingi ninazozisikia kila kona! Watu wanalia hali ngumu ya maisha, si wao tu, hata mimi! Wanasiasa, wananchi, wachambuzi wananyoosha vidole vyao kwa watawala, kwamba ndiyo wanaohusika na hali inayoendelea nchini kwa sasa.

 

Watu wanataka matokeo ya haraka kwa mabadiliko yanayofanywa nchini Tanzania ambayo kwa muda mrefu imehangaika na saratani ya uadilifu, ufisadi na matumizi mabaya ya mali za umma, zikiwanufaisha wachache huku wengi wakiteseka, inatakiwa ibadilike na kuwa paradiso ndani ya miaka miwili ya mabadiliko yaliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.

 

Wakati wa kampeni za urais, waliambiwa wanakwenda katika nchi ya ahadi, wanataka kufika katika nchi hiyo ndani ya muda mfupi, bila watu kupita nyikani kwenye mateso na kulipia gharama! Malalamiko kila kona, wengine wanatamani kurejea tulikotoka kwa sababu mateso yamezidi sana hapa nyikani, bila kufahamu kwamba tumekaribia kuingia katika nchi ya ahadi, lakini ni lazima tuwe tayari kulipa gharama.

 

Kamwe sitabeza viongozi wa awamu zilizopita, kila zama na watawala wake, rais wa kwanza wa taifa letu, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliitoa nchi yetu katika ukoloni na akajenga misingi ya kuongoza taifa hili kwa usawa, haikuwa rahisi kusimama mbele ya mkoloni wa Kingereza na kumwambia; ‘rudi kwenu, utuachie nchi yetu’ mzee huyu na wenzake walilipa gharama wakatuletea uhuru na kufikisha taifa leo. Bahati nzuri mhenga mimi wakati wa Nyerere nilikuwa “nipo”, alipokuja mwinyi nikawa “nipo” akaja Mkapa pia “nipo”, akaondoka na kumwacha Kikwete “nipo”, Kikwete akaondoka na kumwacha Magufuli pia “nipo”, nimezipitia awamu zote hizi, kwa kiasi fulani ninaweza kutofautisha.

 

Kipindi cha Mwalimu Nyerere mambo yalikuwa magumu, ingawa mzee yule kwa moyo wake safi na imani alitaka usawa, akihubiri na kuendesha Siasa za Ujamaa na Kujitegemea! Kama kuna kipindi Watanzania tumewahi kuwa na chawa kichwani, kwenye nguo na kila sehemu za mwili ni wakati wa Hayati Baba wa Taifa.

 

Tulipanga mistari kununua sukari au sabuni kwenye duka la ushirika, wakati mwingine ili upate sukari ulilazimishwa uchukue na bidhaa ambayo ilikuwa haitoki dukani kama vile jembe n.k. Ni katika kipindi cha Mwalimu ndiyo uliweza kukuta kabati ya vyombo ina vyombo vya udongo vimeandikwa “Made in China” lakini huwa havitumiki, ni mapambo tu, mpaka wageni waje.

 

Khanga na sabuni za magendo ndiyo kilikuwa kipindi chake, mipaka ya nchi yetu ilikuwa imefungwa, nia ya baba wa taifa ilikuwa njema, alitaka Siasa ya Ujamaa ishamiri na tutengeneze vitu vyetu wenyewe na kujitosheleza ndani kwa ndani! Hakika maisha yalikuwa magumu, ingawa amani na utulivu wa taifa letu ulistawi, hatukuwa na tatizo la ukabila kama ilivyo kwa majirani zetu.

 

Mwalimu Nyerere akamaliza kipindi chake na kuondoka, akiwa amefanya mazuri, lakini pia makosa, hivyo ndivyo ilivyo katika uongozi, huwezi kufanya kila kitu kwa usahihi, akaingia Ali Hassan Mwinyi. Huyu aliona baadhi ya mambo hayakuwa sawa, hakupenda watu wake waendelee kuvaa ‘kaunguza’ ambazo leo hii tunaziita batiki, waogee magwanji (sabuni za kutenengeza nyumbani), wafulie majani ya mipapai, mara moja akaamua kufungua mipaka na kuruhusu watu wafanye biashara, kipindi chake kiliitwa ‘Ruksa’ na Tanzania ikabadilika, ndiyo ulikuwa mwanzo wa mitumba kuingia nchini mwetu. Watu wengi wakapata mafanikio makubwa kifedha katika kipindi cha mzee huyu, ingawa ukweli wa mambo serikali ilikuwa maskini na Ikulu haikuheshimiwa kama ilivyopaswa.

 

Leo hii ukiongea na matajiri wengi nchini mwetu watakuambia walipata utajiri wao katika kipindi cha ‘Mzee Ruksa’, msanii kutoka Kongo, Kanda Bongoman aliwahi kuja kutumbuiza hapa na watu wakalipa kiingilio cha shilingi laki moja, ukumbi ukajaa! Kiingilio ambacho leo hii miaka zaidi ya 25 baadaye hakilipiki. Mwinyi akaondoka madarakani akiwa amefanya mazuri yake na m

 

abaya pia, akimwacha Mzee Benjamin William Mkapa aongoze taifa letu katika zama zake za Ukweli na Uwazi.
Huyu kitaaluma ni Mwandishi wa Habari, alipoingia tu cha kwanza alichokifanya ni mageuzi ya kiuchumi, akabadilisha yale ambayo mzee Mwinyi hakuyafanya sawasawa, akasema serikali haiwezi kufanya biashara, kazi yake ni kukusanya kodi! Viwanda na mashirika mengi ya umma yakabinafsishwa katika sera iliyoitwa ya Ubinafsishaji, akaleta uhuru mkubwa zaidi wa watu kufanya biashara, uingizaji wa bidhaa kutoka Dubai na China ukaongezeka, Watanzania wakaanza kuchuana kibiashara na watu wa mataifa ya Afrika Magharibi, Dar es Salaam ikageuka kuwa soko kubwa la nchi jirani za Kongo, Zambia, Msumbiji, Malawi, Rwanda na Burundi, kila mfanyabiashara akawa anataka kusafiri kwenda China.

 

Hoteli za Kariakoo zikawa zinajaa wageni kupindukia kutoka nchi jirani, mzunguko wa fedha ukaongezeka nchini mwetu, kwa wanaokumbuka ni katika kipindi cha Rais Mkapa hata shirika la usambazaji la umeme, Tanesco liliwekwa chini ya uongozi wa kampuni binafsi, mengi aliyafanya mzee Mkapa, mazuri na mabaya, akamaliza muda wake na kuondoka akimwacha Jakaya Mrisho Kikwete aongoze taifa. Huyu akaja na Maisha Bora kwa Kila Mtanzania, akaangalia mabaya ya Mkapa na kuyaacha au kuyarekebisha, huku akiendeleza mema yote na pia kuanzisha mengine mapya! Ndani ya kipindi cha Kikwete biashara zilizidi kukua, watu wakawa na fedha nyingi, halikuwa jambo la ajabu kwa mtu kuuza nyumba maeneo ya Sinza kwa shilingi milioni mia saba hadi mia nane! Zama za Kikwete hizo, fedha ilikuwepo mtaani.

 

Hayo yakiendelea na watu wakifurahia fedha mitaani, kulikuwa na upotevu mkubwa wa fedha za Umma, wizi wa maliasili za taifa, jambo ambalo waziri wake wa ujenzi, John Pombe Magufuli lilimkera, akaapa moyoni mwake; “Hiiiiiiiii! Siku nikiingia, hakyanani…” Kama wanavyosema vijana,
‘Mara Paaap!’ Magufuli kasomeka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, la kwanza alilolifanya ni kudhibiti matumizi mabaya ya serikali, safari zote za nje na semina zisizokuwa na tija ambazo wakati wa mtangulizi wake zilishamiri zikapigwa stoooop! Wizi wa mali za Umma na ufisadi ukadhibitiwa, ukusanyaji wa kodi ukaongezeka. Mara Paap! Acacia wakasomeka wezi wa madini yetu, wakabanwa mpaka wakakubali kulipa, mambo yakabadilika nchini Tanzania, mzunguko wa fedha ukashuka, biashara zikaanza kufungwa!

 

Hayo yakitokea rais alikuwa akielekeza nguvu zake nyingi kwa wananchi wanyonge; elimu bure, madawa hospitalini, mikopo kwa wanafunzi, ujenzi wa reli mpya, ununuzi wa ndege mpya za Shirika la Ndege la Tanzania na mambo mengine mengi mazuri akiyafanya kwa fedha za ndani. Yote haya yakiendelea kelele na malalamiko yalikuwepo mitaani, wananchi walikuwa wakilia maisha magumu, wengine wakidai walitoka kulikuwa kuzuri kuliko walipo! Nchi ya ahadi waliyoahidiwa ilikuwa imechelewa kuwadia, hiki ndicho kinachoendelea Tanzania kwa sasa, wapo wanaolia, lakini wapo wanaofurahia.

 

Ninachokusudia kusema hapa ni kwamba, hakuna mafanikio au mabadiliko yaliyokuja bila maumivu! Lazima tutaumia kabla mambo hayajakaa vizuri, kifaranga hakiwezi kutotolewa bila yai kuvunjika, mbegu haiwezi kuota bila kuoza! Lazima tuumie kidogo, lazima tukosee mahali fulani, lakini kama tukiendelea kujifunza kutokana na makosa yetu na kubaki kwenye njia ileile, ipo siku tutafika kwenye hatma yetu.

 

Mwingereza mmoja aliwahi kusema; “However slow is the move, if you keep moving forward one day you will reach your destiny!” Akimaanisha hata kama unatembea kwa mwendo wa taratibu kiasi gani, ukiendelea kwenda mbele ipo siku utafika kwenye hatma yako! Hiki ndicho tunachotakiwa kukifanya Watanzania, kuendelea kusonga mbele, hata kama tutafanya makosa, hali itakuwa ngumu kiasi gani, ili mradi tunalo tumaini lazima tutafika kwenye Tanzania mpya!

 

Jambo moja muhimu tunalotakiwa kufanya ni kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake, unapoona jambo fulani haliendi sawa, fungua mdomo wako, zungumza, hiyo ni haki yako ya kikatiba. Tuelewe tu kwamba haitakuwa rahisi kiasi hicho, itachukua muda, tupunguze malalamiko na kuendelea kusonta vidole serikali, tutimize wajibu wetu na vivyo hivyo serikali itimize wajibu wake kwa wananchi, rais ayaone machozi ya watu wake na Mungu ampe hekima ya kubadilisha anapopaswa kufanya hivyo. Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki Watanzania wote, Ahsanteni kwa kunisoma. Itaendelea wiki ijayo…

NA ERIC SHIGONGO


Loading...

Toa comment