The House of Favourite Newspapers

Hali Mbaya Mauaji ya Kutisha Kila Kona, Sababu Aaanikwa

0

NDANI ya muda mfupi kumekuwa na mlolongo wa mauaji ya kutisha karibu kila kona ya nchi, jambo linaloashiria hali ni mbaya, IJUMAA lina ripoti kukutoa machozi.

Kwa mwezi Januari pekee kumeripotiwa matukio yasiyopungua 20 ya mauaji wa watu wa kada mbalimbali kama watoto, vijana, wazee, wake na waume.

Baadhi ya mauaji hayo yametekelezwa na watu wa karibu hasa ndugu wa damu huku wengine wakiwaua wazazi wao kwa tamaa ya kurithi mali.

 

SABABU ZA MAUAJI

Kufuatia hali hiyo, watetezi mbalimbali wa haki za binadamu waliozungumza na Gazeti la IJUMAA juu ya sababu za mauaji hayo wanasema miongoni mwa sababu ni kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kulevya, mmomonyoko wa maadili katika jamii, vijana kupenda utajiri wa harakaharaka na kutopenda kufanya kazi.

Mambo mengine, ni kutosimamiwa kwa sheria za kazi hasa kwa wafanyakazi wa ndani na kesi za mirathi kuchukua muda mrefu.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini Tanzania, Anna Henga ameliambia IJUMAA kuwa, ni muhimu kesi za mirathi zikamalizika kwa wakati kwa sababu wasimamizi wa mirathi huchukua muda mrefu bila kugawa mali, jambo linalozua changamoto.

“Mambo matatu nadhani yanaweza kuchangia, kwanza huwenda kuna matumizi ya dawa za kulevya, suala la mirathi kuchukua muda mrefu au tatizo la kumomonyoka maadili,” anasema.

 

Anasema kuwa, kumekuwa na tatizo la kisheria kwa sababu watu sasa hivi huajiri wafanyakazi wa kada mbalimbali bila kupeana mikataba wala kufuata sheria, hali inayochangia kutopatikana kwa suluhu unapotokea migogoro na muhusika huamua kufanya lolote ili haki yake ipatikane.

Naye Mtaalam wa Saikolojia ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Chris Mauki anasema kuwa, ili kumaliza tatizo la mauaji, wazazi wanapaswa kuwalea watoto kimaadili ili kuwaepusha na tabia za ajabu.

“Haya matukio ni ya kukomeshwa, lakini ni muhimu kuyadhibiti mapema, unapoona mtoto anatumia dawa za kulevya ni muhimu kutoa taarifa ili adhibitiwe na wanaomuuzia wabainike,” anasema.

 

VIONGOZI WA DINI, IGP SIRRO

Wengi waliozungumza na IJUMAA wameitaka jamii, wazazi na viongozi wa dini kusaidia suala la malezi na maadili katika jamii ili kukomesha matukio hayo ya mauaji.

Kwa upande wake, juzi Jumatano, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro kukomesha mauaji ya kikatili yanayoendelea nchini.

Naye Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, SACP David Misime anasema kuwa, jeshi hilo lipo kwenye mikakati mizito ya kuhakikisha linakomesha mauaji hayo huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano.

 

MAUAJI YALIYOTIKISA

Yapo matukio ya mauaji ambayo yametikisa mno kutokana na namna yalivyotokea kama ifuatavyo;

MAUAJI YA BARKE RASHID

Mwanamke Barke Rashid alidaiwa kuuawa Januari Mosi, 2022 katika nyumba ya kulala wageni ya (gesti) Maridadi iliyopo Tabata-Segerea jijini Dar.

Ukubwa wa tukio hilo ni namna lilivyofanyika ambapo mmoja wa watuhumiwa aliyesemekana alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Barke alidaiwa kukubaliana kumlipa mtuhumiwa mwenzake, John Cena shilingi milioni 1.7 ambapo alimtangulizia milioni 1.2 ili kutekeleza mauaji hayo.

 

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar, Muliro Jumanne, watuhumiwa wawili wanashikiliwa na Polisi ambapo uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.

 

MFANYABIASHARA WA MADINI MTWARA

Katika tukio lingine lililotikisa, Polisi saba mkoani Mtwara, wanatuhumiwa kufanya mauaji na kuutupa porini mwili wa mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamisi aliyekuwa na umri wa miaka 25 baada ya kumpora kiasi cha pesa.

 

MFANYABIASHARA WA MADINI ARUSHA

Katika mauaji mengine, Jeshi la Polisi jijini Arusha, bado linamshikilia kijana Patrick Mmasi (24) mkazi wa Njiro, Kontena jijini humo kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi, Ruth Mmasi (40) ambaye alikuwa mfanyabiashara maarufu wa madini kisha mwili wake kuutumbukiza kwenye chemba la choo katika nyumba yake.

 

MAUAJI MENGINE YA KUTISHA

Mauaji mengine ni ya aliyekuwa mfanyabishara maarufu Alice Matafu mkazi wa Mwika-Kaskazini, Moshi ambaye aliuawa kwa kukatwa na mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kupoteza maisha huku mlinzi wa familia hiyo akiumizwa kwa kukatwa na mapanga na watu wasiojulikana na kuondoka na simu ya marehemu ambayo walikuwa wakiitumia kufanya utapeli.

 

Edmund Matafu ambaye ni kaka mkubwa wa familia hiyo anasema Alice aliuawa kwa ukatili mkubwa na watu wasiojulikana.

Kutoka Kilimanjaro, tukio lililotikisa mwezi Januari ni lile la binti kudaiwa kumuua mama yake mzazi ili kurithi mali.

 

Usiku wa Januari 17 na 18, 2022, mwanamke anayefahamika kwa jina la Teresia Maliya mkazi wa Ilboru wilayani Arumeru jijini Arusha alibakwa na kunyongwa hadi kufa ambapo mwili wake ulikutwa pembezoni mwa nyumba ya jirani yake huku mpangaji wake aliyetajwa kwa jina la Baraka akituhumiwa kuhusika na tukio hilo.

 

Kutoka jijini Dodoma kumeripotiwa mauaji ya kikatili yaliyotokea Januari 10, 2022 eneo la Miches ambapo muuguzi wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Rufina Komba alikutwa ameuawa nyumbani kwake na watu wasiojulikana.

Tukio lingine la mauaji lililovuta hisia za wengi ni la hivi karibuni ambapo mtoto Elsie Akeza alidaiwa kuuawa kinyama na mama yake wa kambo kisha kutumbukiza mwili wake kwenye tenki la maji.

 

Mkoani Mwanza matukio kadhaa ya mauaji ya kikatili yaliripotiwa Januari, 2022 huku baadhi yakihusishwa na wivu wa kimapenzi na wizi.

Kutoka jijini Mbeya kuliripotiwa tukio la mtoto ambaye ni mwanajeshi kudaiwa kumuua baba yake.

Kutoka Mara watu wawili walidaiwa kwa kukatwa na vitu vyenye ncha kali na watu wasiojulikana.

Kutoka Tabora, Januari 4, 2022, mtu mmoja aliripotiwa kuuawa kwa tuhuma za kushirikiana na mganga wa kienyeji kumtorosha mke wa mtu.

Kutoka mkoani Morogoro kuliripotiwa mauaji ya mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) aliyefahamika kwa jina la Magreth Mashue. Tukio hilo lilifanywa na watu wasiojulikana.

STORI; WAANDISHI WETU, DAR NA MIKOANI

Leave A Reply