The House of Favourite Newspapers

HAMIENI FASTA, HUKU LIGI YA SERENGETI LITE KUMENOGA KINOMA

LIGI Kuu ya Wanawake maarufu kama Serengeti Lite Premier imeenda mapumziko kupisha ratiba za kimataifa lakini kumenoga kwelikweli.

Imefikia mzunguko wa 14, huku JKT Tanzania akibaki kileleni na pointi zake 42 baada ya kushinda michezo yote. Wanapepea kwelikweli msimu huu.

 

Mapinduzi Queens wao mambo hayaendi kabisa,kila wakikaza huku kule panatoboka. Wamebana mkiani mwa msimamo. Wanazibeba timu zote 12 kwani wamekusanya pointi 2 tu, kwenye mechi zote 14.

Mambo yanazidi kuwa matamu kunako ligi hiyo, huku rekodi na viwango vya wachezaji vikizidi kuongezeka kila siku, ambavyo vinachagizwa na mdhamini mkuu ambaye ni bia tamu ya Serengeti Lite.

 

Spoti Xtra ambalo linaongoza kwa mauzo Tanzania kila Alhamisi na Jumapili, limekuandalia mambo kadhaa ambayo ulikuwa hauyafahamu na kwa kiasi fulani yameweka rekodi na historia kadhaa kunako ligi hiyo.

 

MABAO
Yamefungwa 306 mpaka sasa, washambualiaji wa JKT Queens, Fatuma Mustapha na Asha Rashidi (Mwalala) wakichuana vikali kwenye mbio za ufungaji, Fatuma akifunga 24, Asha amefunga 22

WACHEZAJI
Zaidi ya wachezaji 286, wamesajiliwa kwenye timu tofauti na kushiriki kwenye ligi hiyo inayojumuisha vikosi vya timu 12.
Kikosi chenye wachezaji wengi zaidi ni 28 ambacho ni Alliance huku kile chenye namba ndogo ya wachezaji ni 18 ni Panama ya Iringa.

 

MAPEMA SANA
Thadea Aidan (Pogba) wa Yanga ndiye mchezaji anayeshikilia rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi kwenye msimu huu.

Alitupia sekunde ya 22, kwenye mchezo wa raundi ya 13 dhidi ya Marsh Queens ya Kigoma kwenye ushindi wa mabao 3-2, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Karume.

 

HAT TRICK
Kinara wa ufungaji kunako ligi hiyo, Fatuma Mustapha ndiye bingwa wa kufunga mabao matatu (Hat trick).

Hadi sasa Fatuma, ameshafunga Hat Trick tano, huku akiweka rekodi ya kufunga mabao 15 kwenye mechi tatu,kila mechi alikuwa anatupia tanotano.

Akifuatiwa na Asha Hamza wa Sisterz mwenye Hat trick mbili,Donisia Minja JKT amefunga mbili, Asha Rashid (Mwalala) JKT Hat trick mbili.

Wengine wenye Hat trick moja moja ni Mwanahamisi Omari (Simba Queens), Fausta Thomas (Yanga Princess), Amina Ramadhani (Simba Queens), Stumai Abdallah (JKT Queens) na Asha Hamis wa Alliance Queen.

 

UMEME
Kuna wachezaji watatu wamekula kadi nyekundu mpaka sasa, uswahili wanasema wamekula umeme.

MAFAZA
Flora Kayanda na Grace Toni wa Yanga Princess wanaoneka kuwa wachezaji wenye umri mkubwa zaidi kwenye ligi hiyo achilia mbali, uzoefu wao na ukongwe kwenye soka la Wanawake.

 

YANGA NA SIMBA
Siyo kwa wanaume pekee, bali hata kwenye timu za Wanawake kumekuwa na ule upinzani wa Simba na Yanga.

Lakini kwa upande wa Wanawake zimeonekana kuwa na utofauti mkubwa wa ubora, Simba Queens wakionekana kuwa bora zaidi na uzoefu mkubwa kwenye soka la Wanawake.

 

Matokeo yao Uwanjani yanajieleza yanajionyesha. Walipokutana raundi ya kwanza, Yanga walikula mabao 7-0. Lakini hata kwenye ishu ya usajili Simba wameonekana kuwa mbele, wakisajili hadi mchezaji wa kigeni kutoka Burundi.
Kwenye msimamo Simba wapo nafasi ya tatu na Yanga Princess wakiwa nafasi ya 7.

 

MASTAA
ASHA Rashidi (Mwalala), Fatuma Mustapha na Dionisia Minja kutoka JKT, wanaonekana kuwa mastaa kwenye timu hiyo na wameikamata ligi yote.

Wanaupiga sana. Fatuma ana mabao 24, Mwalala 22 na Dionisi anayo 15. Wamekamata ligi yote.
Wanafuatiwa na wachezaji kama Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ (Evergreeen), Joelle Bukuru, Mwanahamisi Omari Gaucho (Simba Queens), Asha Hamza (Sisterz Fc) Aisha Juma (Yanga Princess) na Jamila Kassim (Mlandizi).

 

KOCHA MKALI
Ally Ally ni kocha anayekinoa kikosi cha JKT Queens, hadi sasa anaonekana kuwa ndiye kocha mwenye mafanikio zaidi. Anapiga tu wenzie hajui kufungwa maana yake ni nini.
Kumbuka pia, Ally anashikilia rekodi ya kunyakua ubingwa wa msimu uliopita akiwa na JKT Queens pasipo kupoteza mchezo wowote, kwa hali ilivyo anaweza akairudia tena.

Stori na Issa Liponda | Spoti Xtra

 

Comments are closed.