The House of Favourite Newspapers

Hans Poppe, msikie Tambwe

0

AmissTambwe2

Straika hatari wa Yanga, raia wa Burundi, Amissi Tambwe.

Mwandishi Wetu Dar es Salaam
BAADA ya kuifunga Simba kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka, straika hatari wa Yanga, raia wa Burundi, Amissi Tambwe, amekataa kujibu kejeli za Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, badala yake amesema ataendelea kumjibu kwa vitendo uwanjani.

Tambwe alifunga bao moja wakati Yanga ikiwanyoosha Simba kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, juzi.

Hans Poppe amekuwa akitoa maneno ya kejeli kwa Yanga kwa muda mrefu baada ya timu yake kuwatawala watani wao hao kwa kipindi cha miaka miwili.

Moja ya kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na kiongozi huyo mwenye mvuto katika klabu hiyo ni kama: “Tunawaandalia supu ya mawe na kachumbari ya misumari.”

Pia Hans Poppe inadaiwa kuwa ndiye aliyeshinikiza Tambwe aachwe Simba, akidai hana kiwango na ni mchezaji ambaye anafunga kwa kuvizia tu.

Lakini Tambwe amesisitiza atakuwa akijibu kwa vitendo uwanjani.
“Kipindi kile (Hans Poppe) alisema mambo mengi sana, lakini mimi sina hata neno la kumueleza zaidi atakuwa akiyaona mambo kwa vitendo uwanjani.

“Mimi nitakuwa ninapambana kama mwanasoka, kazi yangu ni kucheza, kufanya vizuri na kuisaidia timu yangu. Maneno nitamuachia yeye,” alisema Tambwe ambaye ameuanza msimu huu kwa kasi. Hadi sasa katika mechi nne za ligi, amefunga mabao manne na kutoa pasi za mabao nne.

Wakati huohuo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa, amesema: “Leo (juzi) supu ya miiba na mawe wameinywa wenyewe, mpishi wakati anaipika akawa anaionja mwisho akanogewa akainywa yote.”

Msemo huo ni kama dongo kwa Hans Poppe ambaye amekuwa akitumia kauli hiyo mara kadhaa inapotokea Simba imeifunga Yanga ambapo safari hii umemrudia mwenyewe na kuamua kuutolea ufafanuzi.

“Yanga hawana la kuongea, kuhusu supu ya mawe na miiba hiyo ni ya kwao na walishaila mata nyingi sana labda safari hii wameamua kuitema lakini hiyo ni ya kwao hata wafanyeje,” alisema Hans Poppe.

Leave A Reply