Harmo, Mobetto Wazama Hoteli Moja Masaa 7
KUMEKUCHA tena! Msanii Rajab Abdul ‘Harmo’ na Hamisa Mobeto, wameonekana wakizama hoteli moja iliyopo eneo la Oysterbay – jijini Dar es Salaam.
Chanzo kutoka kwenye hoteli hiyo (jina linahifadhiwa) kililitonya Risasi Mchanganyiko Novemba 30, mwaka huu, saa mbili asubuhi kuwa:
“Njooni haraka Harmo na Hamisa wameingia hotelini.”
HABARI KAMILI
Baada ya wito huo muhimu kutoka kwa chanzo chetu, waandishi wetu walifika haraka eneo la tukio na kukuta gari analomiliki Harmo ambalo picha yake imetumika ukurasa wa mbele likiwa limebaki nje ya hoteli hiyo.
“Harmo na Mobeto walifika hotelini kwa kutumia gari moja?” Lilikuwa swali la kwanza kutoka kwa mwandishi wetu kwa chanzo ambacho hata hivyo kilisema kila mtu aliingia kivyake.
“Hapana hawakuja wote, alitangulia Hamisa (Mobeto) baadaye ndiyo akaja Harmo,” chanzo kilidai.
MAVAZI WALIYOKUWA WAMEVAA
Habari kutoka chanzo chetu kilisema kuwa, siku hiyo Mobeto alifika hotelini hapo akiwa amevaa gauni refu la rangi ya njano huku Harmo yeye akiwa ‘ametupia’ jinzi na tisheti nyeusi na kichwa alikifunika kwa kitambaa chenye madoa meusi mchanganyiko na kahawia.
WALIINGIA CHUMBA KIMOJA?
Kama ambavyo wewe una hamu ya kujua wawili hao walishea chumba kimoja, ndivyo ilivyokuwa kwa waandishi wetu ambao walitafuta ukweli wa swali hilo bila majibu.
“Siwezi kuthibitisha kama wote wamo chumba kimoja kwa sababu sikuwafuatilia kwa ndani lakini kuingia nina uhakika wameingia,” chanzo kilisema.
WAANDISHI WAZAMA MAPOKEZI
Baada ya majibu hayo waandishi wetu waliingia mapokezi katika hoteli hiyo yenye eneo zuri la kupumzikia wageni ambapo waliketi na kuagiza vinywaji.
Hatua hiyo ililenga kuanza safari ya kuwavizia mastaa hao wakati wakitoka hotelini kwa kuwa uwezekano wa kuwafuata ndani haukuwepo.
Toka saa 2 asubuhi waandishi wetu waliweka mtego hotelini hapo hadi saa 1:46 jioni wakisubiri bila mafanikio kuziona sura za Harmo na Mobeto.
HARMO ATOKA HOTELINI
Kama wasemavyo Waswahili ‘subira huvuta heri’ ndivyo ilivyokuwa kwa waandishi wetu ambao walikuwa wakiwasubiri mastaa hao watoke ambapo muda huo wa saa tisa alasiri, Harmo alitoka vyumbani hadi mapokezi walipokuwepo waandishi wetu.
Harmo alikutana ana kwa ana na waandishi wetu lakini hakuwafahamu na hivyo kuelekeza maongezi yake kwa wahudumu.
Hata hivyo, maongezi kati ya msanii huyo na wahudumu si ya msingi kuyaandika lakini baadaye staa huyo alibonyeza simu yake na kucheza wimbo wake wa Uno kwa sekunde chache kisha kusepa zake nje.
AONDOKA HOTELINI
Mara baada ya kutoka nje ya hoteli hiyo, Harmo alielekea lilikokuwa limepaki gari lake ambako alionekana akizungumza na kijana mmoja kisha baadaye kuondoka.
MOBETO AZIDI KUSUBIRIWA
Aidha, baada ya waandishi wetu kumshuhudia Harmo akiondoka, kiu ilikuwa ni kumuona Mobeto naye akitoka huku mpango ukiwa ni kufanya naye mahojiano laivu.
Yawezekana chale zilimcheza staa huyo wa kike ambaye pia ni mwanamuziki na mwanamitindo maarufu nchini, hakuonekana kutoka nje ingawa chanzo kiliendelea kudai kuwa bado angali ndani kwa vile hakuna mlango mwingine wa kutokea zaidi ya ule waliokuwa wameweka mtego waandishi wetu.
WAANDISHI WAONDOKA
Hadi giza linaanza kutanda, hakukuwa na dalili za mtu kutoka jambo lililowafanya waandishi wetu waondoke kwenye hoteli hiyo kwa hofu ya kushtukiwa kwa sababu walikuwa wamekaa hapo kwa muda mrefu.
Hata hivyo, asubuhi siku iliyofuata chanzo chetu kiliibuka na madai mapya kwamba, Mobeto alilala hotelini hapo na kusherehesha uwepo wa tukio lingine ambalo nalo linashughulikiwa kitaaluma.
HARMO ATAFUTWA
Maadili yanataka uwepo usawa wa habari kwa pande mbili, ndivyo ambavyo waandishi wetu walifanya kwa kumtafuta Harmo ili kujua alikwenda hotelini hapo kwa shughuli gani ambapo majibu yake baada ya kusimuliwa tukio yalikuwa:
“Unasema nini wewe? Acha upumbavu,” alijibu Harmo kisha kukata simu ambapo baada ya dakika kadhaa mtu aliyejitambulisha kuwa ni mtu wa habari wa Harmo alipiga simu na kuomba habari isitoke.
“Kama mna ushahidi wa picha sawa, lakini kama hamna mkiandika tutafikishana pabaya.”
MOBETO HUYU HAPA
Kwa upande wake Hamisa Mobeto alipotafutwa kuhusiana na madai hayo ya kuwepo hoteli moja na Harmo siku hiyo ya Jumamosi alisema:
“Unaota au una uwendawazimu?”
Kwake hakukuwa na zaidi ya kukata simu na alipopigiwa mara kadhaa hakupokea simu.
STORI: MWANDISHI WETU, RISASI